September 29, 2024

Faida za kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti Tanzania

Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wamesema ongezeko hilo ni ishara muhimu kwa Watanzania kufaidika na fursa mbalimbali za mtandaoni ikiwemo biashara na elimu.

  • Watumiaji wa intaneti nchini Tanzania wamefikia milioni 29.1 Machi mwaka huu.
  • Idadi hiyo imechangiwa na ongezeko la watumiaji wa simu na mabadiliko ya teknolojia.
  • Wadau wasema ongezeko hilo linafungua fursa za kibiashara, elimu na mapato kwa Serikali.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kubainisha kuwa watumiaji wa intaneti nchini wamefikia zaidi ya milioni 29, wachambuzi wa masuala ya teknolojia wamesema ongezeko hilo ni ishara muhimu kwa Watanzania kufaidika na fursa mbalimbali za mtandaoni ikiwemo biashara na elimu. 

TCRA katika takwimu za mawasiliano za robo ya kwanza ya mwaka 2021 imeeleza kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka hadi kufikia milioni 29.1 mwezi Machi mwaka huu kutoka milioni 27.9 waliorekodiwa Septemba 2020. Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji milioni 1.1 (asilimia 4.1 ) katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Hadi Desemba 2020, watumiaji wa intaneti Tanzania walikuwa milioni 28.47, ikiwa ni ongezeko la watumiaji zaidi ya milioni 11 ndani ya miaka mitano. Desemba 2015 kulikuwa na watumiaji milioni 17.26.  

Hata hivyo, ripoti hiyo haijaweka wazi ni aina gani ya intaneti inayotumiwa zaidi na Watanzania kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka iliyopita, ambapo intaneti inayohamishika isiyo ya waya  (mobile wireless) imekuwa ikitumiwa zaidi kuliko ile isiyohamishika ya waya.

Intaneti inayohamishika ambayo hutolewa na kampuni za simu hutumika zaidi na simu za mkononi, tableti na kompyuta mpakato.  

Ripoti hiyo imeeleza kuwa hata matumizi ya mabando ya intaneti (Data Traffic in MBs) yameongezeka hadi kufikia megabaiti bilioni 117 (117 bilioni MB’s) kutoka megabaiti bilioni 91 zilizotumika Septemba 2020. 

Ongezeko la watumiaji wa intaneti limekuwa likishudiwa kila mwaka jambo linaloashiria kuwa Watanzania wanavutiwa na huduma hiyo ambayo imekuwa ikisaidia kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi mtandaoni.

Huenda ongezeko la watumiaji wa intaneti nchini limechangiwa na kuongezeka kwa watu wanaomiliki laini za simu za mkononi ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo wamefikiwa milioni 52.8 ambapo milioni 15.9 wanatumia mtandao wa Vodacom sawa na asilimia 30.2 ya watumiaji wote.

Zaidi ya nusu ya wamiliki hao wa simu, wanatumia huduma ya intaneti kwenye simu zao, jambo linalowaweka karibu na fursa za mtandaoni.

Ongezeko la watumiaji wa intaneti linamaanisha nini?

Wadau wa masuala teknolojia wameiambia Nukta Habari kuwa ongezeko la watumiaji wa intaneti nchini siyo la bahati mbaya kwa sababu duniani inaenda kasi na shughuli nyingi zinafanyika mtandaoni, hivyo kuwalazimisha watu kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Mwanafunzi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknoloji cha Mbeya (MUST) Elisha Lameck amesema intaneti imerahisisha utendaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo kuweka mifumo na majukwaa ya kidijitali ambayo hayazuiwi na mipaka ya nchi au jamii.

“Haya mabadiliko hayaepukiki, kwa sasa karibu kila kitu kinafanyika mtandaoni hata mawasiliano watu wanafanya mtandaoni. Sasa ukibaki nyuma unapitwa na vitu vingi na unajicheleweshea maendeleo yako mwenyewe,” amesema mdau huyo wa teknolojia.


Zinazohusiana:


Mkuu wa Bidhaa na Suluhu wa kampuni inayotoa huduma ya intaneti ya Raha Liquid Telecom, Boniface Mbwambo amesema kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti Tanzania ni fursa inayowaweka watu karibu na fursa za mtandaoni ambazo siyo rahisi kuzipata kama mtu hana intaneti.

Amesema kwa sasa shughuli nyingi zinafanyika mtandaoni zikiwemo biashara, mawasiliano na hata usimamizi wa taasisi na kampuni mbalimbali, hivyo ni rahisi kwa Watanzania kufaidika na mifumo hiyo.

“Inteneti inaunganisha biashara na masoko mbalimbali, watu hawaishii kuwasiliano tu mtandaoni bali wanafanya biashara na kuendesha maisha yao kwa kujipatia kipato. Yote hiyo ni kuongezeka kwa matumizi ya intaneti,” amesema Mwambo. 

Aidha, amesema intaneti imerahisisha shughuli za huduma za kifedha kwa njia ya simu kwa sababu kwa kutumia intaneti mtu anaweza kufanya miamala kokote alipo na kufanikisha malipo na huduma zake mbalimbali bila kuhitaji kwenda benki.

Kuongezeka kwa intaneti kunasaidia Serikali kupata mapato ya kikodi ambayo hutumika katika utoaji na uboreshaji wa huduma za kijamii. 


TANGAZO:


Kibarua kilichopo

Licha ya idadi ya Watanzania wanaoutumia intaneti kuongezeka, bado kilio kimekuwa katika bei za vifurushi vya data ambavyo vimekuwa vikiisha haraka huku gharama yake ikiwa juu na wakati mwingine watoaji wa huduma hizo hufanya mabadiliko ya mara kwa mara. 

Ili kukabiliana na changamoto hizo, TCRA ilianza kutekeleza kanuni ndogo za kuratibu utoaji wa huduma za vifurushi vya mawasiliano ya simu Aprili 2 mwaka huu ikiwa ni hatua ya kutatua malalamiko ya makato yasiyo sahihi ya gharama za matumizi ya vifurushi vya simu za mkononi.

Hata hivyo, kuanza kutumika kwa kanuni hizo zinazosimamia vifurushi vya dakika za kupiga simu, bando la intaneti na meseji zinazotumwa kwenye simu za mkononi, bado hakujaleta ahueni kwa watumiaji wa intaneti.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndungulile katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 amesema Serikali itaendelea kufuatilia na kudhibiti gharama za vifurushi, promosheni na ofa maalum zinazotolewa na watoa huduma simu  ili kulinda maslahi ya watumiaji.