October 6, 2024

Fanya haya ukigundua umeweka mafuta yasiyo sahihi kwenye gari lako

Ikitokea hali hiyo imekukuta, huna haja ya kuhofia kuhusu uharibifu wa gari yako. Fanya haya kuliokoa gari lako ikitokea umeweka mafuta yasiyohitajika.

  • Unashaulriwa kutokuliwasha gari lako na kulisukuma mpaka gereji ili mafuta hayo yaondolewe.
  • Kama mafuta yamesambaa sana, basi inatakiwa injini kusafishwa kuzuia uharibifu zaidi.

Dar es Salaam. Siyo jambo geni kwa wamiliki wa gari na hata wale wanaoazima magari kukosea kuweka aina ya mafuta yanayotumika na gari wanaloliendesha.

Kama bado hujaelewa ni kuwa badala ya kuweka petroli, mtu akaweka mafuta ya dizelil kwenye gari kwa kutokujua na hata kujisahau.

“Mara nyingi inatokea kwa gari zinazotumia mafuta ya dizeli kuwekewa petroli kwani pampu za sheli nyingi ni za petroli. Wale wahudumu usipowaambia, wengi huwaza petroli kwani wateja wao wengi ni wa mafuta hayo,” amesema Duma. 

Ikitokea hali hiyo imekukuta, huna haja ya kuhofia kuhusu uharibifu wa gari yako. Fanya haya kuliokoa gari lako ikitokea umeweka mafuta yasiyohitajika. 

Hatua ya kwanza, zima gari yako mara moja. Na kama upo sehemu ambayo unahitaja kusogeza gari, ni bora ukaita huduma za kusogeza gari (break down) ikusaidie kufanya hayo. 

Endapo huduma hiyo itakuwa mbali, unaweza kuitoa gari yako kwenye gia ya kupaki na umuombe mtu akusaidie kusukuma.

Duma amesema kufanya hivyo kutaepusha mafuta hayo kwenda kwenye injini na sehemu za ndani zaidi na kufanya uharibifu mkubwa.

Kama umegundua baada ya gari kutembea umbali fulani basi peleka gereji kwa ajili ya kuondoa mafuta hayo uliyoyaweka kimakosa.

Ni muhimu kufahamu kuwa unahitaji kuondoa mafuta yote na kusafisha injini na tenki la mafuta kwani mzunguko wa mafuta hayo kwenye gari lako unaweza kusababisha hitilafu kwenye gari.


Zinazohusiana


Utajuaje kama umeweka mafuta ambayo siyo?

Huenda hakuna uwezekano wa wewe kushtuka juu ya mafuta uliyoyaweka lakini zipo dalili ambazo unaweza kufikiria kuwa huenda umekosea kuweka mafuta sahihi kwenye gari yako.

Kati ya dalili hizo ni gari kutikisika wakati unaendesha na mwisho wake gari kuzima kabisa.

Tsukasa Azuma ambaye ni mwandishi wa makala kuhusu magari kutoka Car from Japan amesema kwa wataalamu wa magari, wanaweza kutoa mafuta hayo wenyewe kwa kufungua koki ambayo mara nyingi inakuwa chini ya gari na kisha kuyakinga mafuuta hayo kwenye kontena.

Hata hivyo, koki hiyo haipo kwenye magari mengi lakini mtu anashauriwa kulipeleka gari kwa watalamu ili waweze kupima kiasi cha uharibifu uliofanyika.