October 6, 2024

Halotel kuboresha mawasiliano ya simu maeneo ya utalii

Inakusudia kuboresha mtandao wa mawasiliano ili kuongeza idadi ya wateja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

  • Inakusudia kuboresha mtandao wa mawasiliano katika maeneo ya utalii nchini ili  kuongeza idadi ya wateja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.  
  • Wajipanga kuwekeza katika mtandao wa 4G nchi nzima.
  • Bado suala la kutokuwa na umeme vijijini inawaletea changamoto ya uendeshaji wa mitambo.

Dar es Salaam. Wakati inaadhimisha miaka mitatu ya kuwepo katika soko la mawasiliano ya simu, Kampuni ya Halotel inakusudia kuboresha mtandao wa mawasiliano katika maeneo ya utalii nchini ili  kuongeza idadi ya wateja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.  

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa Halotel, Mhina Simwenda amesema ndani ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo wamehakikisha huduma ya 3G na mitandao ya mawasiliano inapatikana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye vivutio vya kitalii

“Kwasasa hivi, mtanzania au mtalii akiwa eneo la Ngorongoro Creta au maeneo ya kitalii anaweza akatumia huduma ya Halotel 3G katika maeneo yote,” amesema Simwenda.

Kampuni hiyo imejipanga kuboresha mtandao wa mawasiliano katika maeneo yote ya  utalii nchini na maeneo mengine ili kuongeza wigo wa kuwafikia wateja wengi hasa wale wanaoishi vijijini.

Amesema ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kuchangia uchumi wa Taifa kupitia utalii na mawasiliano wanalenga kuboresha huduma  za simu na kuongeza ubunifu wa teknolojia.

“Tunataka kuboresha huduma ya 4G nchi nzima, ambayo itaboresha huduma zetu za mawasiliano pamoja na kuongeza kasi ya intaneti yetu,” amesema.


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa Simwenda, kwasasa Halotel ina wateja milioni nne sawa na ongezeko la wateja milioni 1.2 kwa mwaka na wanatarajia kuongeza wateja wengi zaidi hadi kufikia mwaka 2020.

Licha ya mafanikio hayo ya Halotel na uwekezaji mkubwa waliofanya hasa maeneo ya vijijini, bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo wizi wa vifaa katika maeneo ya minara kutokana na wananchi kutokuwa na uelewa wa utunzaji wa miundombinu ya mawasiliano.

“Ukipita katika barabara zote kuu, tumepitisha nyaya zetu, kuunganisha mkoa mmoja hadi mwingine kuna wakati mwingine zinakatika na wakati mwingine watu sio waaminifu wanazikata,” amesema.

Vilevile tatizo la ukosefu wa umeme maeneo ya vijijini umekuwa changamoto  kwasababu ya kutumia gharama kubwa za uendeshaji wa mitambo ukilinganisha na gharama ya matumizi ya wateja wa eneo husika.

Hata hivyo,  Halotel imedhamiria kuwa moja ya kampuni inayofanya vizuri katika sekta ya  mawasiliano ambapo mpaka sasa imelipa kodi zaidi ya bilioni 208 Serikalini.