October 7, 2024

Hivi ndivyo televisheni ya Instagram itakavyowanufaisha watumiaji wake

Furaha ya Maston imeanza baada ya kusikia kuwa mtandao wa kijamii wa Instagram una mpango wa kuwawezesha watumiaji wake kuhifadhi maudhui ya mubashara katika kipengele chake cha televisheni (IGTV).

  • Maudhui ya mubashara yatakuwepo kwa muda mrefu zaidi na sio kwa siku moja kama awali.
  • Wadau wa maudhui wamesema itasaidia kutengeneza maudhui mengi zaidi.
  • Itaondoa ulazima wakukimbizana kutazama maudhui ya mubashara mengi kwa wakati mmoja.

Dar es Salaam. “Nitafurahi wakifanya hivyo. Hiyo inamaanisha kuwa ninaweza kutengeneza maudhuii mengi zaidi na sitakuwa na ulazima wa kuhifadhi video hizo kwenye simu,” amesema Frankie Maston ambaye ni mwanamuziki na mtengeneza maudhui kupitia mtandao wa Instagram.

Furaha ya Maston imeanza baada ya kusikia kuwa mtandao wa kijamii wa Instagram una mpango wa kuwawezesha watumiaji wake kuhifadhi maudhui ya mubashara katika kipengele chake cha televisheni (IGTV).

Mtandao huo unaoruhusu kupakia (upload) maudhui yaliyo kwenye mfumo wa video na picha zenye urefu wa dakika moja kwenye kipengele cha “Instagram Feed”.

Pia maudhui ya video yenye urefu wa zaidi ya dakika moja, huweza kupakiwa kwenye IGTV huku vipengele vingine kama Insta Live vikimuwezesha mtu kutengeneza maudhui mubashara kwenye mtandao huo.

Awali, maudhui hayo baada ya mtu kuruka mubashara yalikuwa yakihifadhiwa kwenye Instagram Stories ambapo yalikaa kwa saa 24 tu na kutoweka mazima.

Huenda furaha ya Maston ambaye ni mwanamuziki wa miondoko ya AfroPop ikawa ni ya watengeneza maudhui wote ulimwenguni kwani baada ya maboresho hayo maudhui mubashara yatabaki na kuishi kadri muandaaji apendavyo.


Zinazohusiana


Mkurugenzi wa kampuni ya J Sisters ambaye pia ni Mwamuziki wa nyimbo za injili, Jessica Msama amesema pia hutengeneza maudhui ya kutoa motisha kwa vijana kupitia Instagram.

Kinachokuwa kinamkwamisha kufikia watu wengi ni kufutika kwa maudhui hayo baada ya kumaliza.

“Unapokuwa mubashara,inamaanisha wewe una nafasi na siyo kila mtu  anakuwa na nafasi ya kukuangalia. Kuna wengine wanakuwa hawana bando kwa muda huo. Wanakuwa wamekukosa,”  amesema Jessica.

Kwa mujibu wa mhamasishaji huyo, maboresho hayo yatasaidia maudhui kuwepo na mtu kuangalia kwa muda wake anapokuwa na nafasi.

Zaidi, maboresho hayo yataondoa ulazima wa kukimbizana kutazama vipindi hivyo na kumpatia mtu uhuru wa kuchagua hasa pale chaneli zaidi ya moja zinaporusha matangazo yao mubashara.