November 24, 2024

Hivi ndivyo unavyoweza kupata simu mpya kwa bei rahisi

Wapo wauzaji ambao wanapokea simu zilizotumika ambazo ziko katika hali nzuri na kukupa simu mpya kwa bei rahisi.

  • Ni kwa kuwasilisha simu uliyotumia dukani na kupewa simu mpya kwa kuongezea kiasi kidogo cha fedha.
  • Aina hiyo ya biashara inakusaidia kuokoa fedha kila ununuapo simu mpya.
  • Mfumo huo utakusaidia kupata simu mpya kila zinapoingia sokoni.

Dar es Salaam. Hata wakati baadhi ya watu wakitumia simu zao hadi pale zinapoharibika au kupotea, wapo ambao hununua simu mpya kila toleo jipya linapotoka.

Mwaka huu utawaona na iPhone X na pale iPhone 11 tu inapotoka, tayari wameipata. Ni watu wanaoenda na wakati, hawataki kupitwa.

Siyo kuwa wako vizuri kiuchumi lakini wameamua kuchangamkia fursa ili kuwa na teknolojia mpya kila inapotoka. Kama bado hujagundua huo ujanja, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) inakufumbua macho.

Wapo wauzaji ambao wanapokea simu zilizotumika ambazo ziko katika hali nzuri na kukupa simu mpya kwa bei rahisi. 

Mathalan, kwa mtu ambaye anatumia iPhone 11 Pro Max iliyo na GB256 (uwezo wa uhifadhi wa vitu) anaweza kupata iPhone 12 Pro Max yenye GB 256 kwa bei ya kuanzia Sh2.3 milioni badala ya Sh4.5 milioni kwa mujibu wa bei za duka la simu la ShopifyTz lililopo Mlimani City jijini Dar es Salaam. 

Muuzaji wa duka la Shopify, Mohamed Bakari amesema unapobadilisha simu ili upate mpya unakuwa umeokoa takriban nusu ya fedha yako endapo simu yako ina hali nzuri na haijachakaa.

“Watu wengi wanapenda kununua simu zilizotumika hivyo pale unapoleta simu yako dukani kwetu, utachukua mpya kwa bei rahisi,” amesema Bakari.

Simu aina gani hubadilishwa?

Siyo kila simu inaweza kubadilishwa. Bakari amesema ili mtu apate simu mpya anatakiwa kuwa na simu inayofanana au yenye toleo la simu mpya. 

“Ni Samsung chache ambazo unaweza kuibadilisha na iPhone mfano note 20,” amesema Bakari.


Soma zaidi


Changamoto za mfumo huu kwa wauzaji

Mfumo huo wa uuzaji hutumika kwa baadhi ya simu ikiwemo Samsung na iPhone ambapo hauwezi kutumika kwa simu za Techno, Huawei, Infinix na zinginezo.

Wakati mwingine, njia hiyo ya uuzaji wa simu huingilia na matapeli wenye nia ovu ambao huiba simu za watu na kuzipeleka dukani ili wapate mpya, jambo ambalo huwaletea usumbufu kwa wauzaji ikiwemo kutiwa hatiani.

Muuzaji wa simu kutoka duka la Eshop lililopo soko la Dar Free Market (DFM) aliyefahamika kwa jina la Shigela amesema kutokana na changamoto hizo, imewafanya wachukue uamuzi wa kukubali simu ambazo zimewahi kununuliwa katika duka lao na si vinginevyo.

“Endapo mtu amewahi kununua simu kwetu, anaileta dukani tunaangalia hali ya simu hiyo kisha tutamuambia ataogezea shilingi ngapi apate simu mpya,” amesema Shigela.

Unasubiri nini? Kama wewe ni mdau wa Samsung, au iPhone, usisubiri ikufie mkononi. Peleka kwa wenyewe ili upate mzigo mpya.