July 5, 2024

Huduma za fedha kwenye simu za mkononi zashika kasi Tanzania

Thamani ya miamala ya fedha inayofanywa kwenye simu za mkononi imefikia Sh10.6 trilioni mwezi Juni mwaka huu huku watumiaji wa huduma hizo nao wakiongezeka.

  • Thamani ya miamala ya fedha inayofanywa kwenye simu za mkononi imefikia Sh10.6 trilioni mwezi Juni mwaka huu. 
  • Idadi ya miamala na watumiaji wa huduma za fedha kwa njia simu nao waongezeka. 
  • M-Pesa inayomilikiwa na Vodacom Tanzania yatawala soko la huduma za kifedha kwa njia ya simu. 

Dar es Salaam. Kasi ya Watanzania kutumia huduma za fedha jumuishi inazidi kupaa baada ya ripoti mpya ya mawasiliano kuonyesha kuwa thamani ya miamala ya fedha inayofanywa kwenye simu za mkononi imefikia Sh10.6 trilioni mwezi Juni mwaka huu. 

Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kuwa miamala inayofanywa kupitia huduma za kifedha za simu za mkononi imekuwa ikiongezeka kwa miezi mitatu mfululizo katika robo ya pili ya mwaka 2020. 

Ripoti hiyo ya robo ya pili ya mwaka 2020, inabainisha kuwa mwezi Aprili pekee thamani ya miamala ya fedha iliyofanywa katika simu za mkononi ilifikia Sh8.4 trilioni, ikaongezeka hadi Sh9.5 trilioni mwezi uliofuata kabla haijavuka zaidi ya Sh10 trilioni Juni mwaka huu.

Huduma za kifedha kwenye simu zinasaidia kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kutatua changamoto mbalimbali za kibenki ikiwemo kuweka fedha, kukopa na kulipia huduma na bidhaa mbalimbali.

Pia zinasaidia kuchochea shughuli za kibiashara kwa njia iliyo rahisi na haraka zaidi.


Soma zaidi:


Wakati thamani ya miamala ya fedha hizo ikiongezeka, pia idadi ya miamala ya fedha nayo imekuwa ikiongezeka kila mwezi katika kipindi hicho cha robo ya pili ya mwaka 2020.

Katika mwezi huo wa Juni, watumiaji wa huduma hiyo walifanya miamala milioni 272.4 ikiwa ni juu kidogo kutoka miamala milioni 257.5 ya Mei na Aprili ambapo ilifanyika miamala milioni 247.8.

 

Watumiaji wa simu benki nao waongezeka

Ripoti hiyo inaonyesha pia watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi imeongezeka hadi kufikia milioni 29.6 Juni 2020 kutoka milioni 28.6 mwezi Mei. 

Idadi ya watumiaji wa huduma hizo ni sawa na asilimia 61.6 ya watumiaji milioni 48.2 wa simu za mkononi Tanzania waliorekodiwa Juni mwaka huu.

Hata hivyo, karibu nusu ya watumiaji wa huduma hizo, wanatumia huduma ya M-Pesa inayosimamiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania. 

Hadi Juni, M-Pesa ilikuwa na watumiaji milioni 11.5 (asilimia 39 ya soko lote) ikifuatiwa na Tigo Pesa (milioni 8.8) na Airtel Money watumiaji milioni 5.8.