October 6, 2024

Huu ndiyo mtandao ghali zaidi wa intaneti Tanzania

Ni Vodacom Tanzania unaotoza Sh205 kwa MB 1 ya intaneti ukifuatiwa na Zantel kwa wateja wanaotumia intaneti nje ya vifurushi kabla ya kodi.

  • Ni Vodacom Tanzania unaotoza Sh205 kwa MB 1 ya intaneti ukifuatiwa na Zantel
  • Tozo hizo ni kwa watumiaji wa simu janja ambao hawajiungi na vifurushi vya intaneti wanapokuwa mtandaoni. 
  • Vodacom yasema kuna changamoto ya tafsiri isiyo sahihi ya takwimu zilizotolewa na TCRA za tozo za intaneti kuhusu kampuni hiyo. 

Dar es Salaam. Ni bayana kuwa watumiaji wa intaneti ya kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania ndiyo wanaotozwa kiwango kikubwa zaidi cha pesa kulipia huduma hiyo wakiwa nje ya mfumo wa bando (kifurushi) kuliko kampuni zingine za mawasiliano nchini, ripoti mpya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebanisha. 

Takwimu za mawasiliano za robo ya tatu ya mwaka 2019 zilizotolewa na TCRA hivi karibuni zinaonyesha kuwa Vodacom inawatoza wateja wake Sh205 kwa kila megabaiti 1 (MB) kabla ya kodi.  

Hiyo ni sawa na kusema kama mtumiaji wa simu janja ataweka vocha ya Sh500 na akaruhusu intaneti itumike bila kujiunga na kifurushi cha intaneti, basi atapata MB2.43 pekee kabla ya kodi. 

Hata hivyo, Vodacom imeiambia Nukta Tanzania (www.nukta.co.tz) kuwa “kuna changamoto ya tafsiri” katika takwimu hizo za TCRA na kwamba ni asilimia 0.03 ya wateja wake hutumia intaneti nje ya vifurushi huku zaidi ya asilimia 99.9 wakitumia vifurushi. 

Kiwango hicho cha tozo ni kwa wateja ambao wanatumia intaneti ya vocha wanazoweka kwenye simu zao bila kujiunga na vifurushi vya internet (internet bundles) vinavyotolewa na mitandao ya simu za mkononi. 

Tozo hizo zinazotozwa na kampuni hizo kwenye intaneti hazijumuishi kodi ya Serikali (Tax Exclusive).

Tozo za intaneti za Vodacom ni kubwa zaidi ya zile zinavyotozwa na makampuni mengine ya simu nchini ambayo hayazidi Sh100 kwa MB 1.

Takwimu hizo za TCRA za kati ya Julai hadi Septemba 2019 zinaonyesha kuwa mteja wa Vodacom anayetumia intaneti kwa vocha ya simu yake bila kifurushi anatozwa mara 41 zaidi ya yule wa Smile ambaye mtandao wake unamtoza Sh5 kwa MB 1.

Smile ndiyo mtandao wenye kiwango cha chini cha tozo za intaneti kwa wateja wake  miongoni mwa kampuni za simu Tanzania. 

Mtandao ambao unafuata kwa viwango vikubwa vya tozo za intaneti baada ya Vodacom ni Zantel ambao unakata Sh93 kwa MB 1 ikifuatiwa kwa mbali na Tigo na Airtel ambazo zote zinatoza Sh29.

Halotel wao wanatoza Sh22 kwa MB 1 huku TTCL ambayo inamilikiwa na Serikali inawatoza watumiaji wake Sh10 tu kwa MB 1 ikiwa wataweka vocha na kuruhusu intaneti itumike katika simu zao bila vifurushi. 

Hata wakati Vodacom ikiwatoza viwango vya juu watumiaji wa intaneti wasiojiunga na vifurushi, ni tofauti na waliopo kwenye mfumo wa vifurushi ambao hutozwa Sh31 kwa kila MB 1 bila kodi wakiwa mtandaoni na Sh52 wakiwa nje mtandao. 

Huduma ya intaneti kwa njia ya simu (mobile internet) imekuwa ni biashara ambayo inazipatia faida kubwa kampuni za simu, ikizingatiwa kuwa watu wengi wenye simu janja wanatumia intaneti kuperuzi vitu mbalimbali mtandaoni. 

Mathalani, Ripoti ya awali ya kifedha kwa mwaka ulioishia Machi 2019 iliyotolewa na kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania PLC imeeleza kuwa mapato yake yatokanayo na huduma katika mwaka ulioishia Machi 31, 2019 yalifikia Sh1.018 trilioni ambapo asilimia 17.9 ya mapato hayo yalitokana intaneti (data). 


Soma zaidi:


Vodacom yazungumzia intaneti yao

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Huduma za Wateja wa Vodacom Tanzania, Celvin Mmasy ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kuna changamoto ya tafsiri isiyo sahihi ya takwimu zilizotolewa na TCRA za tozo za intaneti kuhusu kampuni hiyo. 

Amesema tafsiri iliyotolewa haijajumuisha taarifa zote muhimu kwa watu kuelewa tofauti iliyopo ya tozo zilizotolewa na TCRA na tozo halisi ambazo wateja wa Vodacom wanakatwa kwenye intaneti ya mfumo wa bando (vifurushi). 

“Tozo zilizochapishwa na TCRA ni zile zilizo nje ya makato ya bando ambazo ni asilimia 0.03 ya wateja wanaotumia intaneti yetu, na asilimia 99.9 ya wateja wanatumia bando (vifurushi). 

 “Bei yetu ni Sh1.45 kwa megabaiti moja (bila kodi). Ni muhimu ieleweke kuwa asilimia 99.9 ya wateja wetu wanatumia intaneti ya bando (vifurushi). Kwa minajili hiyo, unaweza ukaona jinsi bei zetu kwa megabaiti moja zilivyo nafuu,” amesema Mmasy.