October 6, 2024

Huu ndiyo mwisho wa matumizi ya chaja za simu za waya?

Ilianza simu kuondoa antena, tundu la jack port 3.5 mm na sasa, huenda mfumo wa kuchaji kwa waya ukafuata.

  • Hivi sasa, simu nyingi zinazouzwa kwa bei kubwa (high end smart phones) zina mfumo wa kuchaji bila waya.
  • Licha ya juhudi hizo kuanza tangu mwaka 2012, bado muitikio siyo mkubwa kwenye jamii lakini baadaye itashika kasi sana. 
  • Ilianza simu kuondoa antena, tundu la jack port 3.5 mm na sasa, huenda mfumo wa kuchaji kwa waya ukafuata.

Dar es Salaam. Mabadiliko katika teknolojia ni kitu cha kawaida na huenda yanafanyika kila siku sababu kuu ikiwa ni kufanya maboresho ya teknolojia ya zamani na kuweka urahisi katika matumizi ya teknolojia mpya.

Mathalan, miaka 15 iliyopita, simu nyingi ziliingia sokoni zikiwa na sehemu kwa ajili ya kuchomeka vifaa vya kusikilizia sauti (earphones) maarufu kama “Jack port 3.5mm”. Kazi yake kuu ni kusikilizia muziki, kupiga simu na kufanya kazi kama antena kwa kuwezesha redio kwenye simu.

Hata hivyo, kuanzia mwaka 2010, kampuni kadha wa kadha za kutengeneza simu janja ikiwemo ya Oppo, Apple  na Samsung zilitoa matoleo ya simu yaliyoiruka teknolojia hiyo maarufu. 

Siyo kuondoka kwa sehemu ya earphone peke yake bali hata simu zingine kuachana kabisa na zana hiyo ya kusikilizia muziki kwa njia ya waya na badala yake kutumia zana isiyotumia waya amarufu kama “earphones za bluetooth”.

Kuanzia mwaka 2010, kampuni kadha wa kadha za kutengeneza simu janja ikiwemo ya Oppo, Apple  na Samsung zilitoa matoleo ya simu yaliyoiruka teknolojia ya sehemu ya kuchomekea earphones za “Jack 3.5mm”. Picha| Google Images.

Mabadiliko hayo ndiyo sababu ya uchambuzi huu unaofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuhusu chaja za simu zisizotumia waya. 

Simu ya kwanza kufanya mapinduzi hayo ilikuwa ni Nokia Lumia 920 ambayo ilizinduliwa mwaka 2012 ambapo mfumo wa kuchaji bila waya uliwekwa kama mfumo mbadala. Baada ya Lumia, simu zingine ikiwemo simu za Samsung Galaxy Note 4 mwaka 2014 na kampuni zingine zilifuata. 

Hata hivyo, kwa simu janja zilizo na gharama ya juu ambazo zimeingia sokoni mwaka 2020/21 nyingi zimewekewa mfumo wa kuchaji bila waya.

Kuanzia Samsung Galaxy S20, S20+, S20 Ultra, Samsung Galaxy Note10, Note10+, Samsung Fold, S10e, S10, S10+ zinaruhusu kuchajiwa bila waya huku matoleo ya simu za Apple (iPhone) kuanzia iPhone8 pia yakiruhusu teknolojia hiyo.

Mbali na ushindani wa sokoni, huenda dhumuni kubwa la simu kufanya ivyo ni kuondoa matundu katika simu moja kwa moja ili kuzipatia simu muonekano ang’avu. Pia ni njia ya kuzipunguzia simu changamoto ya kuharibika pale zinapoingiwa na maji.


Soma zaidi:


Hata hivyo, endapo hilo litatokea, itakuwaje kwa ambao hubeba chaja zao katika vibegi na mikoba kwa ajili ya kuchaji pale wanapokuwa mbali na nyumbani?

Mabadiliko ya teknolojia hayaepukiki. Kuhamia katika mfumo wa kuchaji simu pasipo nyaya kutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kurahisisha maisha kwa watumiaji wa simu.