October 6, 2024

Huyu ndiye shujaa wa watu wenye ulemavu Tanzania

Anatumia majukwaa ya mtandaoni kurahisisha mawasiliano kwa walemavu na kuwaunganisha na fursa za ajira na masomo.

  • Ni Gwaliwa Mashaka ambaye anawasaidia walemavu kupata fursa za elimu na ajira.
  • Anatumia majukwaa ya mtandaoni kurahisisha mawasiliano kwa walemavu na kuwaunganisha na fursa.
  • Mdau huyo wa teknolojia amedhamiria kutengeneza mazingira jumuishi katika jamii.

Dar es Salaam. Kuzaliwa au kupata ulemavu siyo jambo ambalo mtu yeyote anatarajia kukutana nalo au anapenda limtokee. Baadhi huzaliwa na hali hiyo huku wengine maswaibu ya maisha yakiwaacha na hali hiyo ambayo hubadili mtindo wa maisha yao.

Kwa baadhi, maisha hubadilika baada ya kuhusika katika ajali mbalimbali zikiwemo za barabarani na hata nyumbani huku wengine changamoto za kiafya yakiwemo magonjwa ya saratani na mengineyo yakiwasababishia kupata ulemavu.

Wakati maisha ya Watanzania hao yanapoanza kuwa na tofauti, mazingira hubaki kama yalivyo ikiwemo watu wanaowazunguka, miundombinu na kwa baadhi, ndoto, malengo, na mahitaji hubadilika.

Takwimu kutoka hospitali inayohudumia wagonjwa wenye ulemavu Tanzania, (CCBRT), zinasema, kuna watu milioni 4.2 milioni ambao wanaishi na ulemavu nchini.

Na kati ya watu hao, wengi hubaki katika umaskini huku wakishindwa kujiendeleza kielimu na kiuchumi.

CBRT inasema, idadi ya watu wenye ulemavu ambao hawajui kusoma na kuandika inafika asilimia 48 au  takriban watu watano kati ya 10 miongoni mwa walemavu.

“Matibabu ya watu wenye ulemavu yanaigharimu nchi zaidi ya Sh1.11 trilioni kila mwaka ambayo ni sawa na asilimia 3.76 ya pato la taifa,” inaeleza  CCBRT.

Pia, kati ya watoto walio na ulemavu, takriban nusu yao hawahudhurii shule kwa sababu ya kukosamiundombinu rafiki na hivyo kuzuiliwa kuhudhuria masomo kutokana na hali yao.

Hata hivyo, kumeibuka wada mbalimbali wanaotafuta njia za kuweka ujumuishi miongoni mwa jamii kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu kupata elimu, ajira na kuwaunganisha na fursa mbalimbali.

Kati yao ni Mhandisi na Mwanasayansi wa takwimu Gwaliwa Mashaka (35), ambaye ameamua kutafuta suluhu ya fursa za ajira, elimu na mawasiliano kwa kuwahusisha watu wanaopatwa na hata waliozaliwa na ulemavu.

       

Mashaka amesema, kipindi anasomea shahada yake ya uhandisi wa kompyuta na teknolojia ya habari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alipata ajali ambayo ilimlazimu kusitisha masomo yake ili kutafuta msaada wa matibabu.

Ajali hiyo ndiyo ilimfanya kuanza kufikiria namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu hasa wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali.

Mashaka alibuni majukwaa ambayo yanawaunganisha watu wenye ulemavu na fursa na kuwasaidia kuwasiliana ikiwemo wasioona, walio na ulemavu wa kusikia na hata watu wanaoishi na usonji.

“Wazo hili lilikuja baada ya kupata ajali nilipokuwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kutokana na kukosa msaada na makazi, ilinibidi nisitishe masomo yangu ili nitafute msaada wa kiafya. Iliniamsha kutafuta suluhu kwa watu waliona mahitaji pale wanapopata ulemavu wa muda mfupi na hata wa maisha,” anasema Mashaka.

Mjasiriamali huyo aliyeanzisha majukwaa hayo miaka mitatu iliyopita ameyataja majukwa hayo kuwa  ‘Employable Africa’, jukwaa linalowapatia watu ujuzi wa kidijitali kwa ajili ya kuwawezesha kupata ajira.


Soma zaidi:


Pia  anamiliki jukwaa la ‘Rafiki Connect’ ambalo huwezesha mawasiliano kati ya watu walio na ulemavu wa kusikia, kuona na walio na changamoto zingine za kiafya zinazosababisha uhitaji wa mawasiliano maalumu kwa njia ya ukalimani mubashara.

“Ukalimani mubashara kupitia Rafiki Connect ni bidhaa mpya barani Africa. Tanzania na nchi nyingi Africa zina ukalimani wa alama ambao sio rafiki kwa wengine ambao wana ulemavu na changamoto za kiafya ikiwemo saratani na usonji,” amesema Mashaka.

Mashaka amesema wapo wengi ambao hawaelewi lugha ya alama wakiwemo waliopata ulemavu wakiwa ukubwani hivyo huduma ya Rafiki Connect inayotoa ukalimani mubashara huweza kueleweka na mtu yeyote mwenye ulemavu na kumpatia nafasi ya kutoa mrejesho papo kwa hapo.

Rafiki Connect na Employable Africa zinavyofanya kazi

Mara nyingi katika semina mbalimbali za kujenga uwezo, walimu hawana uwezo wa kuwasiliana na watu walio na mahitaji maalumu hivyo kitu hicho huwanyima watu walio na ulemavu wa kusikia, kuona na usonji nafasi ya kupata elimu hiyo.

Mashaka kupitia huduma ya Rafiki Connect hutoa huduma ya ukalimani mubashara ambapo kunakuwa na mkalimani anayeelezea mafunzo yanayotolewa kwa watu wenye changamoto za mawasiliano ana kwa ana.

“Inahitaji mkalimani alie na uwezo mkubwa wa kuendana na kasi ya mwalimu na pia husaidia mwalimu kupata maswali kutoka kwa mawanafunzi alie na changamoto ya mawasiliano. 

“Huduma hii hugharimu Sh266,600 kwa saa moja” ameeleza Mashaka akisema huduma hiyo imepata muitikio mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Pia, Kupitia Employable Africa, Mashaka anatoa huduma za kuandaa wasifu (CV) kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu, kuwapatia kozi za kuwajengea uwezo pamoja na kuwapatia ujuzi.

Huduma anazozitoa Gwaliwa zinawafikia watu wenye ulemavu na wale wasio na ulemavu. Picha| PFP-IDE.

Kati ya kozi zinazotolewa ni pamoja na namna ya kujiandaa na kipindi cha mahojiano kwa ajili ya ajira, kuandaa wasifu nakadhalika. Pia, Mashaka huwaunganisha walemavu na fursa za ajira na pamoja na za masomo.

“Katika huduma zetu tumewafikia vijana takriban 600 wakiwemo walio na ulemavu na wasio na ulemavu,” amesema Mashaka aliye na malengo ya kufanya huduma ya ukalimali ipatikane kwa njia ya kidijitali (app) ili wazazi waweze kuitumia nyumbani kwao na watoto au ndugu wenye ulemavu.

Mashakaa amesema, “kwa kozi za kuwajengea uwezo ambazo huchukua wiki tatu hadi mwezi mmoja kulingana na kasi ya uelewa wa mtu, zinatolewa kwa Sh30,000,” amesema Masanja aliyesema kozi hizo zipo kwa wote wakiwemo walio na ulemavu na wasio na ulemavu.

Ada hiyo inayotolewa inatumika kwa ajili ya kuwapatia vifaa vya kujifunzia 

Hadi sasa, Huduma za Gwaliwa zimewafikia wateja wa kimataifa wakiwemo kutoka Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Rwanda na Marekani.

“Hatutabaki Tanzania pekee, tunahitaji kuwafikia Waafrika wote. Huduma tunayotoa Afrika ni mpya kwasababu kwa muda mrefu barani Afrika kumekosekana ujumuishi katika jamii,” amesema Mashaka.

Wadau wasema ni zaidi ya ubunifu

Hata wakati wabunifu wakiendelea kuibuka na suluhu za changamoto mbalimbali nchini, wadau wamesema wabunifu wanaoangazia changamoto za watu walio na mahitaji maalumu bado ni wachache.

Mkurugenzi wa tafiti na ubunifu kutoka Tanzania Data Lab (dLab) Agapiti Manday ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa “bunifu nyingi zinahitajika kwenye eneo hili (la watu walio na mahitaji maalumu) na wabunifu watahitaji sana kupewa ushirikiano na Serikali na wadau wa teknojia. 

Mdau huyo wa teknolojia amesema anachokifanya Mashaka ni kitu kizuri kwani kinaangazia watu wanaohitaji msaada mkubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania.

Kwa sasa Gwaliwa anaendelea kutafuta wafadhili mbalimbali wakitaifa na kimataifa ikiwemo kupitia jukwaa la Accelerator linaloendeshwa na dLab ambapo ni miongoni mwa Watanzania wengi wanaotafuta ufadhili huo ili kuhakikisha huduma zake zinawanufaisha watu wengi zaidi.