Idadi ya wasichana kwenye sayansi yazidi kuongezeka Tanzania
Wengi kwa sasa wanaona sayansi ni kama fursa hivyo wanachangamkia masomo hayo.
- Idadi ya wanafunzi wanaotaka kushiriki maonnyesho ya wanasayansi chipukizi imeongezeka kutoka maombi 604 mwaka jana hadi maombi zaidi ya 670 mwaka huu.
- Maonyesho hayo huibua miradi mbalimbali ya kisayansi iliyofanywa na wanafunzi.
Dar es Salaam. Miaka kumi iliyopita ilikuwa ni ngumu kukuta wanafunzi wengi wakike katika masomo ya sayansi.
Mwamko wa wanafunzi kuchangamkia masuala yakisayansi ulikuwa ni mdogo ikilinganishwa na masomo mengine ikiwemo biashara na sanaa. Wengi walisema “sayansi ni ngumu.”
Hata hivyo, jambo hilo limebadilika baada ya kuwapo mwamko mkubwa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo hayo shukran kwa serikali, wadau, wazazi na walimu waliotoa hamasa kubwa kwa mabinti wa Tanzania.
Mwanzilishi Mwenza wa Shirikisho la Wanasayansi chipukizi Tanzania (YST), Dk Gozibert Kamugisha amesema kwa sasa wanafunzi wameona masomo ya sayansi kama fursa na “wanayachangamkia vilivyo.”
Dk Kamugisha amesema Shirikisho la YST limefanya kazi ya kuamsha chachu ya kisayansi kwa wanafunzi wa shule za sekondari kupitia kuhamasisha wanafunzi kufanya tafiti na kugundua vitu vinavyoisaidia jamii.
“Zamani mwalimu alikuwa akifundisha kwa kutumia vitabu yaani anafundisha sayansi kwa chaki ubaoni. Lakini kwa sasa walimu wanatumia njia za vitendo na wanafunzi wanaelewa zaidi na kuyapenda masomo ya sayansi,” amesema Dk Kamugisha.
Kwa mujibu wa mdau huyo wa masuala ya sayansi, jambo hilo ndiyo sababu ya maonyesho ya wanasayansi chipukizi ya mwaka huu kupata washiriki wengi kutoka mikoa yote Tanzania.
Idadi ya wanafunzi wanaotaka kushiriki maonnyesho ya wanasayansi chipukizi imeongezeka kutoka maombi 604 mwaka jana hadi maombi zaidi ya 670 mwaka huu.
Maonesho ya wanasayansi chipukizi yatafanyika mwezi Oktoba mwaka huu yakijumuisha kazi za kisayansi 150. Picha| YST.
Dk Kamugisha amesema, mwaka jana walipokea maombi yenye miradi ya kisayansi 604 ambayo ilichuujwa na kubakisha miradi 123 iliyochuana kitaifa. Mwaka huu, YST imepokea zaidi ya maombi 670 inayojumisha wasichana na wavulana ambayo imechuujwa kupata miradi 579.
“Yalikuja maombi ya miradi zaidi ya 670 tumeyachuuja kupata miradi 579 ambayo wanafunzi wamefundishwa kuboresha mawazo yao,” amesema Dk Kamugisha.
Mtazamo wa watoto wa kike juu ya ugumu wa masomo ya sayansi nao unabadilika taratibu jambo linaloonyesha siku zijazo kutakuwa na wanawake wengi katika masomo hayo muhimu kwa katika ukuaji wa uchumi kupitia sayansi na teknolojia
Mwenyekiti wa Taasisi ya KJF inayodhamini maonyesho hayo, Yusuph Karimjee amesema inatia hamasa kuona sayansi siyo jambo gumu miongoni mwa wanafunzi.
Karimjee amesema wakati wanaanza kudhamini maonyesho ya wanasayansi, ni shule nne pekee ndiyo zilijitolea kufanya maonyesho hayo hivyo kwa sasa kufikia hatua ya maonyesho hayo kufanyika kimkoa katika mikoa 25 inatia moyo.
“Wanafunzi walioshiriki katika kila mwaka programu za YST wameendelea na kuwa madaktari, wauguzi, wahandisi na wafamasia. Kila mmoja hufanya tofauti na kuchangia katika maendeleo ya uchumi,” amesema Karimjee.
Soma zaidi:
- Mabinti Watanzania wang’ara kwa kubuni teknolojia ya kupambana na ukame
- Wasichana, wavulana 10 bora matokeo kidato cha nne 2020
- Kutana na mwanadada wa miaka 26 anayeongoza taasisi ya kuwainua wasichana kiuchumi Tanzania
Naye Makamu wa Rais na Mwenyekiti wa kampuni ya nishati, Shell Tanzania, Jared Kuehl amesema Maonyesho ya YST yanakuza sayansi, teknolojia, uhandisi na elimu ya hisabati na kusaidia wanafunzi kuwa wabunifu, wadadisi na kukuza utamaduni wa sayansi.
Kama mdhamini, Kuehl amesema kwa mwaka huu matarajio yake ni kuona tafiti za sayansi zenye ubunifu kutoka shule mbalimbali.
Kwa mwaka huu, maonyesho hayo yataanza kufanyika Julai 19 hadi Julai 30 kwa ngazi ya mikoa ambapo kila mkoa utatoa gunduzi za kisayansi 6 ambazo zitachuana kitaifa mwezi Oktoba kumpata mshindi mmoja atakayenufaika kuendelezwa kielimu na kimradi.
Kwa mwaka jana, maonyesho ya YST yaliibua mradi unaotumia eneo dogo kwa ajili ya kutengenezea chakula cha kulisha wanyama wengi hasa wakati wa ukame ambao kwa kitaalamu unaitwa “Hydroponic Fodder for Animal Feeding and Health” uliobuniwa na Glory Joseph na Martha Machumu, wanafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ngaza iliyopo jijini Mwanza.