Idris alamba shavu Uber
Anakuwa msanii wa kwanza nchini kuingia kandarasi ya ubalozi wa chapa ya Uber takribani miaka miwili tangu kampuni hiyo ilipoanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam.
- Anakuwa msanii wa kwanza nchini kuingia kandarasi ya ubalozi wa chapa ya Uber takribani miaka miwili tangu kampuni hiyo ilipoanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Aprili huenda ikawa ni moja ya miezi ya neema kwa mshindi wa Shindano la Big Brother Afrika mwaka 2014, Idris Sultan baada ya kupata kandarasi ya kuwa balozi wa kampuni ya usafiri ya Uber kwa mwaka 2018.
Kampuni hiyo kubwa duniani, inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola billion 72 za Marekani ilitangaza rasmi mkataba wake na Idriss mbaye ni mchekeshaji, muigizaji wa tamthilia, na mtangazaji wa vipindi vya redio, jioni ya Aprili 20 jijini hapa.
Kwa dili hilo, Idriss anakuwa msanii wa kwanza hapa Tanzania kuwa balozi wa kampuni hiyo ambayo ilianza biashara zake katikati ya mwaka 2016 jijini Dar es Salaam.
Idris ametangazwa katika halfa iliyofanyika katika mgahawa wa kifahari wa Akemi Dar es salaam iliyobeba dhima ya #IdrisnaUber ambayo ilihudhuriwa na wageni wachache na wanahabari wa humu inchini.
Meneja wa Masoko wa Uber Kanda ya Afrika Mashariki, Elizabeth Njeri amesema zoezi la kumpata balozi huyo lilifanyika kwa umakini na ufanisi mkubwa ili kumpata balozi atakayeiletea Uber ufanisi nchini Tanzania.
“Ni msanii ambaye hafanyi mambo yake kwa mazoea, pia anaheshimika katika tasnia ya uchekeshaji, tamthlia, na utangazaji wa vipindi vya redio. Tuna imani kwamba Idris atailetea Uber tija kubwa kwa sababu ni mzalendo kweli kweli, yeye ni kielelezo cha Utanzania na anawasiliana na mashabiki wake kupitia mitandao ya jamii kila wakati,’’amesema Njeri.
Zinazohusiana: Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknoloji
Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify
Idris, ambaye kwenye mtandao wa Instagram ana wafuasi takribani milioni 2.4 wakati akiingia dili hilo, amesema ni heshima kubwa kwake kupata fursa adimu ya kushirikiana na Uber kwa kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa mapinduzi yaliyoletwa katika sekta ya usafiri kupitia kwa mfumo wake kote duniani.
‘’Nimefurahi kuona jinsi Uber inavyopata umaarufu jijini Dar es Salaam. Binafsi mara nyingi mimi hutumia usafiri wa UberX nikiwa na marafiki zangu kwenye mitoko yetu ya jioni na sasa wamaleta huduma nyingine ya bajaji; uberPOA ambayo nina hamu sana kuitumia. Utaniona hivi karibuni,” amesema Idris.
Idris ameingia kandarasi hiyo siku chache tu baada ya kutangazwa na Jarida la Forbes la Marekani kuwa ni moja ya vijana 30 wenye miaka chini ya 30 wajasiriamali wanaofanya mambo makubwa katika umri mdogo barani Afrika.
Kwa takriban miaka miwili ya huduma zake nchini hususan jijini Dar es Salaam, Uber imekuwa mkombozi wa ajira kwa madereva na abiria ambao wamekuwa wakipata usafiri kwa bei rahisi. Uber hutumia teknolojia ya programu ya simu na compyuta kuwaunganisha wateja na madereva na gharama zake zote hukokotolewa na programu husika.