November 24, 2024

Instagram yawezesha wafanyabiashara kusaka wateja mtandaoni

Imewawekea kipengele cha “Instagram Business” kinachowasaidia kuwafikia wateja wengi mtandaoni kwa muda mfupi.

  • Imewawekea kipengele cha “Instagram Business” kinachowasaidia kuwafikia wateja wengi mtandaoni. 
  • Wafanyabiashara wa Tanzania nao wachangamkia teknolojia hiyo kukuza biashara zao.

Ni wazi kwamba mtandao wa instagram umekua moja ya majukwaa ya mtandaoni yanayotumiwa na wafanyabiashara katika kutafuta wateja na kukuza biashara zao katika nchi mbalimbali duniani. 

Wafanyabiashara wengi wamekua wakionyesha bidhaa zao na kupokea oda za wateja kupitia kipengele maalum cha biashara (Instagram business) ambacho kinafanya kazi kama jukwaa la kuwakutanisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma. 

Instagram imeweka utaratibu huo kwa mfanyabiashara kuonyesha bidhaa yake na kuifanya iwafikie watu wengi kwa muda mfupi na kupata watu wanaoweza kuinunua.

Hata hivyo, huduma hiyo ni kuyalipia kulingana na muda unaotaka kuitangaza bidhaa au huduma yako katika mtandao huo wenye watumiaji takribani bilioni 1 kila mwezi.


ZinazohusianaInstagram yaja na mbinu mpya kudhibiti uzalilishaji mtandaoni


Baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania ambao wanatumia huduma hiyo, wameiambia www.nukta.co.tz imewasaidia kukuza biashara zao kwa sababu wanaweza kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja bila kutumia gharama kubwa. 

John Dach ni mfanyabiashara wa viatu Jijini Dar es Salaam anasema teknolojia hiyo imemuongezea wateja wengi na kumfanya awe maarufu katika biashara yake ya viatu. 

“Teknolojia hii imenisaidia sana kwa upande wa kupata wateja kwani sikujua kama naweza kutengeneza kundi zuri la wateja kwa muda mfupi,” amesema Dach. 

Huduma kama hiyo inatolewa na mitandao mbalimbali kama WhatsApp na Facebook ambayo ina wafuasi wengi duniani.