November 24, 2024

Instagram yazindua akaunti maalum ya kuuza bidhaa mtandaoni

Akaunti hiyo inatumika kuwaleta pamoja wanunuzi na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.

Kuundwa kwa akaunti hiyo ni jitihada za Instagram katika kutanua wigo wa biashara ambapo awali ilikuwa ikitegemea zaidi matangazo kama sehemu ya kupata mapato. Picha|Mtandao. 


  • Akaunti hiyo inatumika kuwaleta pamoja wanunuzi na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.
  • Ni jitihada nyingine ya mtandao huo kuwapa watumiaji vitu wanavyotaka. 

Mtandao wa kijamii wa Instagram umezindua akaunti mpya ya @shop maalum ili kuwahudumia watumiaji wake wanaopendelea kufanya manunuzi mtandaoni. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao huo, @shop imetengenezwa na kuingizwa sokoni kwa ajili ya kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa mtandaoni. 

Akaunti hiyo inaendesha manunuzi kwa kutumia picha za bidhaa mbalimbali zinazochapishwa katika kurasa zake ambapo kwa kuanzia imeweka bidhaa za urembo, mitindo, mapambo ya nyumbani na nguo. 

Haitatumika tu kama jukwaa la kutangaza bidhaa, bali itawawezesha watumiaji wake kufanya manunuzi moja kwa moja pasipo kutumia mifumo mingine mbali na mtandao huo. 

Akaunti hiyo imeanza kujipatia umaarufu mkubwa mara tu baada ya kuzinduliwa ambapo mpaka mchana wa leo (Mei 14, 2019) ilikuwa na wafuasi zaidi ya 50,000 huku ikiwa na machapisho 15 tu yanayonyesha bidhaa mbalimbali.


Zinazohusiana: 


Kuundwa kwa akaunti hiyo ni jitihada za Instagram katika kutanua wigo wa biashara ambapo awali ilikuwa ikitegemea zaidi matangazo kama sehemu ya kupata mapato lakini sasa itakuwa sehemu muhimu kwa watu kupata bidhaa mbalimbali kutoka kona mbalimbali za dunia.  

Biashara ya mtandaoni huusisha uuzaji na ununuzi wa bidhaa kwa kutumia mifumo ya kidijitali ambapo watu hawalazimiki kwenda dukani au sokoni lakini kwa kutumia simu au kompyuta anaweza kupata bidhaa au huduma popote alipo. 

Vichocheo vikubwa vya mfumo wa biashara ya mtandaoni ni maendeleo ya teknolojia hususani ueneaji wa mtandao wa intaneti katika maeneo mbalimbali na uwepo wa makampuni ya simu za mkononi.