October 6, 2024

Jinsi app ya sheria kutoka Tanzania ilivyopenya tuzo Afrika 2019

Ni baada ya kufanya uwekezaji wa teknolojia ya matumizi ya simu kutoa huduma za msaada wa kisheria.

  • Ni baada ya kufanya uwekezaji wa teknolojia ya matumizi ya simu kutoa huduma za msaada wa kisheria. 
  • Pia uwezo wa kutumia lugha ya Kiswahili na kuwakutanisha kidijitali pamoja mawakili na wananchi.
  • Tuzo hizo zitafanyika Septemba 6, 2019 Johannesburg, Afrika Kusini. 

Dar es Salaam. Programu tumishi ya simu (App) ya Sheria Kiganjani imechaguliwa kuingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za Afrika za sheria mwaka 2019 zinazotarajiwa kufanyika Septemba 6 mwaka huu Johannesburg, Afrika Kusini.

Sheria Kiganjani ni app ya Tanzania inayotoa msaada wa kisheria kwa njia ya mtandao ikiwemo elimu ya sheria na kuwaunganisha wananchi na mawakili katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha haki inakuwa sehemu ya jamii ya Watanzania. 

App hiyo ambayo inamilikiwa na kampuni ya uwakili ya vijana ya Extent Corporate Advisory (ECA) imechaguliwa kuingia katika tuzo hizo (The African Legal Awards 2019) katika kipengele cha kampuni za sheria zinazotumia teknolojia kutoa huduma za msaada wa sheria. 

Katika kipengele hicho, ECA inashindanishwa na makampuni mengine matano ya Anjarwalla & Khanna (A&K) ya nchini Kenya, Epoq Legal – JusDraft na LAW FOR ALL (Afrika Kusini), JUDY Innovative Technologies Limited (Nigeria), na SchoemanLaw Inc (Afrika Kusini).

Kampuni hizo sita ni miongoni mwa kampuni zaidi 100 zinazohusika na shughuli za kisheria Afrika katika vipengele 26 zinazochuana kuchukua tuzo hizo. 


Soma zaidi: 


Mambo manne yaliyoibeba Sheria Kiganjani

Mmoja wa Wabia wa ECA, Nabiry Jumanne ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kuchaguliwa kwao katika tuzo hizo ni heshima kubwa hasa katika kuthamini msaada wa kisheria wanaoutoa kupitia teknolojia ya simu za mkononi. 

“Tuzo hiyo inaashiria nini kwetu, kwanza ni mafanikio makubwa katika sekta ya IT (Tehama) hususan sheria. Mara nyingi tumeshuhudia IT katika maeneo mengine labda kiuchumi na kibiashara lakini suala la sheria hatuko juu sana tuko nyuma. 

“Lakini kuwa kampuni mojawapo inayotoka Tanzania miongoni mwa kampuni sita Afrika hili ni suala kubwa kwetu,” amesema Jumanne.

Jumanne, ambaye ni Wakili kitaaluma, amesema kilichowabeba kuingia katika tuzo hizo ni uwekezaji wa teknolojia waliofanya katika shughuli za uwakili na sheria nchini ambao umesaidia kuwafikia na kutatua changamoto za kisheria kwa watu wengi kwa muda mfupi. 

Amebainisha kuwa licha ya app kuwa na miezi tisa tu tangu ianze kutoa huduma imeweza kuwafikia watu takriban 10,000 na kufanikiwa kutatua migogoro ya awali ya kisheria ya watu 2,700. 

Timu ya vijana wanaoiwezesha App ya Sheria Kiganjani  kuwafikia watu wengi wanaohitaji msaada wa kisheria. Picha|Nabiry Jumanne.

Matumizi ya lugha ya Kiswahili kutoa msaada wa kisheria yamechangia kuivusha app hiyo na kuwarahisishia Watanzania kuelewa masuala ya sheria kwa lugha nyepesi wanayoielewa haraka.   

“Kwa hiyo tumewaonyesha wale watu wakathibitisha kupitia mfumo wetu lakini zaidi mfumo wetu umekuwa kwa Kiswahili. Mara nyingi tumeshuhudia sheria nyingi zikiandikwa kwa Kiengereza ambazo watu wengi wameshindwa kuelewa na kutambua lakini sisi tulienda mbali na kuanzisha mfumo ambao utahusika na Kiswahili tu,” amesema Jumanne.  

Sheria Kiganjani pia inawafikia Watanzania wa kawaida ambao hawana simu janja, na kuwawezesha kupata huduma za kisheria kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kupiga simu popote walipo Tanzania. 

Jumanne anaeleza kuwa tuzo hizo, zimewaongezea shauku ya kuendelea kubuni teknolojia rahisi ili kuendelea kuwafikia watu wengi ikiwemo wale wanaopendelea kutumia Kiingereza.

Tuzo za Afrika za sheria za kila mwaka huandaliwa na kampuni ya Legal Week na Chama cha Ushauri wa Mashirika cha Afrika Kusini (CCASA) ili kutambua mchango wa taasisi za umma na binafsi zilizobobea katika shughuli za kisheria Afrika.