November 24, 2024

Jinsi ya kukabiliana na mambo yanayozuia wasichana kuwa wabunifu Tanzania

Ni pamoja na kuondoa tamaduni zinazokwamisha ubunifu kwa wasichana na wasichana wenyewe kuamka.

  • Ni pamoja na kuondia vikwazo vya kitamaduni na wasichana waanze waamke na kujitoa.
  • Wadau watakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa sahihi kwa wasichana.
  • Pia wametakiwa kutatua changamoto za jamii yao. 

Kilimanjaro. Licha ya juhudi mbalimbali za Serikali na wadau wa maendeleo kuwawezesha wasichana wengi kuingia katika fani ya sayansi, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kuwa wabunifu. 

Changamoto hizo zikiwemo za mifumo na utamaduni zinawazuia wasichana kuonyesha uwezo na kutoa suluhu za teknolojia zitakazosaidia kuboresha maisha ya jamii. 

Mei 21 mwaka huu wadau wa ubunifu walikusanyika mkoani Kilimanjaro ili kujadili changamoto zinazokwamisha ubunifu miongoni mwa wasichana na namna ya kuwasaidia kujikwamua na wakatumia ubunifu huo kutoa suluhu zitakazosaidia kuboresha maisha ya jamii. 

Mwanzilishi mwenza wa jamii ya wadau wa ubunifu ya Startup Grind Kilimanjaro, Dorcas Mgogwe amesema ubunifu miongoni mwa wasichana upo chini kutokana na changamoto ambazo tayari zinajulikana na ni wimbo wa wadau wengi kila kukicha.

Mgogwe amesema wasichana wana mawazo mazuri ambayo yanatosha kutatua suluhu zinazoikumba jamii lakini hawapati nafasi.

“Kuna mawazo mengi miongoni mwa wasichana. Yanayotatua changamoto zao, yanayotatua changamoto za jamii na mengine, tatizo ni nafasi na uthubutu,” amesema Mgogwe katika mdahalo wa masuala ya ubunifu uliofanyika Mei 21, 2021 mkoani Kilimanjaro.

Licha ya kuwa wadau wanapigania haki sawa za mwanamke katika fursa mbalimbali, kwa baadhi ya jamii, mwanamke bado anarudishwa nyuma na tamaduni. Picha| Global Environment Facility.

Baadhi ya wadau wamesema mifumo iliyopo bado haiwapi fursa sawa wasichana kuonyesha uwezo wao, jambo linalokwamisha wao kukua na kuboresha maisha ya jamii. 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika linalojishughulisha na kutengeneza vifaa vya hedhi na kutoa elimu ya masuala ya afya ya uzazi la Femme International, Florence Akara amesema mifumo ikiwemo familia, shule na wadau wa teknolojia ikuruhusu ubunifu kwa wasichana watafanya mambo makubwa.

“Mifumo isiseme yenyewe inawezesha wanawake, wanawake tayari wanaweza hivyo mifumo hiyo itoe nafasi ya mambo ambayo wanawake wanafanya yaonekane,” amesema Akara.

Tamaduni zatajwa kuwa kikwazo

Wadau wa ubunifu wamesema tamaduni za Kitanzania pia ni kikwazo cha wasichana kuingia katika masuala ya ubunifu kwani msichana akionekana anazungumzia teknolojia, uvumbuzi na ubunifu anaonekana mjuaji.

Afisa Mradi na Mkuu wa Utawala kutoka shirika linalojishughulisha na afya ya watoto la White Orange Youth (WOY), NoelaRebecca Mnyawa amesema jamii tayari ina vitu ambavyo imetenga kwa ajili ya wasichana ikiwemo malezi, kupika na vinginevyo na ubunifu siyo kimoja wapo.

Mnyawa amesema ni muda wa jamii kuhamia katika jamii jumuishi na kufanya utamaduni kutokuwa kikwazo kwa ubunifu hasa kwa wasichana ambao wana uwezo kama walivyo wavulana.

“Jamii inatakiwa kuruhusu wasichana wabuni kwani wanaweza. Wapo wasichana wengi tu ambao wanafanya mambo makubwa na iliwachukua changamoto nyingi za kitamaduni kufikia walipo,” amesema Mnyawa.


Soma zaidi:


Nafasi zipo, uthubutu ndio changamoto

Licha ya kuwa kuna nafasi mbalimbali za wasichana kujihusisha na ubunifu ikiwemo viota vya ubunifu (innovation hubs) na wadau mbalimbali wa teknolojia wasichana, baadhi ya wadau wamesema muamko wao kuchangamkia hizo fursa uko chini. 

Mkurugenzi wa programu ya Asante Africa, Gloria Mushi amesema vijana wengi hawapo tayari kupitia hatua zote zinazohusisha kurasimisha kazi zao za ubinifu. 

Mushi amesema, kuna mikopo ya vijana, wanawake na walemavu halmashauri lakini vijana wanapotakiwa kukamilisha masharti yanayotolewa, baadhi wanakimbia.

“Ili biashara yako irasimike, kuna sehemu mbalimbali ambazo unatakiwa kufikia ikiwemo mashirika mbalimbali  ya kiserikali, kwa vijana wengi inakuwa changamoto,” amesema Mushi kutoka shirika hilo linalojishughulisha na  kujenga mazingira chanya na uongozi kwa wasichana.

Vijana wakubali kupatiwa mafunzo

Ili kuepukana na changamoto hizo, wasichana wameshauriwa kujitambua, kupata taarifa sahihi na kuhakikisha wanakuwa wathubutu kwani hiyo ni njia sahihi kufikia malengo yao.

Mshauri wa maendeleo ya biashara kutoka Shirika linalowasaida wajasiriamali wanaochipukia kibiashara kufikia malengo yao la Anza, Steven Mallya amesema wasichana wanatakiwa kuchangamkia fursa ambazo zipo kwani wapo wadau wengi wanaotoa mitaji, elimu na maarifa ya teknolojia na ujasiriamali.

Amesema fursa hizo zinaweza kuwafanya wawe wabunifu na kufanikiwa katika shughuli zao wanazofanya. 

“Mara nyingi tumeandaa mafunzo kwa ajili ya vijana lakini wengi wamekuwa wakiachana na mafunzo hayo njiani wakidai ni magumu,” amesema Mallya.

Fursa za kibunifu na kiteknolojia kwa wanawake zipo na zinatolewa mara kwa mara. Ni wakati wasichana waamke na kuzichangamkia. Picha| Africa Energy Portal.

Wasichana na vijana wajitambue

Wadau mbalimballi katika mdahalo huo wamesema wasichana wanahitaji kujitambua na kuamka ili kuziona fursa ambazo zipo tayari katika jamii.

Mwalimu wa vijana kutoka shirika la kutoa mafunzo ya wasichana la GLAMI, Lightness Godwin amesema wasichana wanatakiwa kuunganishwa na watu ambao tayari wameanza kufanya kazi wanazotamani kuzifanya ili wapate mtu wa kumtazama kama mfano.

Amesema jambo hilo litawezesha mtu kuwa na mwalimu wa kumsaidia pale anapokwama.

“Kwa vijana, tusikae ndani kama una kitu unafanya nenda nje kakifanye na tangaza biashara yako. Hauwezi kupewa lifti kama umekaa nyumbani, toka nje watu wakione,” amesema Godwin.