July 8, 2024

Kamera inayoendeshwa na roboti kuingia sokoni Februari

Kampuni ya Canon ya nchini Japan imetangaza kuwa inatarajia kuingiza sokoni kamera inayoendeshwa na mfumo wa roboti ili kuwawezesha watumiaji kupata picha za mnato ambazo ni vigumu kupatikana kwa njia ya kawaida ya upigaji picha.

  • Itakuwa na uwezo wa kupiga picha zisizoweza kupigwa kwa njia ya kawaida.
  • Itasaidia kupunguza gharama na matumizi ya kamera nyingi kwa wakati mmoja.
  • Inawafaa zaidi waaandishi wa habari na wanaochukua picha za michezo.

Dar es Salaam. Kampuni ya Canon ya nchini Japan imetangaza kuwa inatarajia kuingiza sokoni kamera inayoendeshwa na mfumo wa roboti ili kuwawezesha watumiaji kupata picha za mnato ambazo ni vigumu kupatikana kwa njia ya kawaida ya upigaji picha.

Ujio wa kamera hiyo ( The robotic Camera System CR-S700R) umechagizwa  na kuongezeka kwa mahitaji ya wataalam wa kupiga picha za mbali hasa zile zinazohitajika na vyombo vya habari na michezo.

Taarifa ya kampuni hiyo inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa vya kupiga picha iliyotolewa Januari 7, 2020 inaeleza kuwa kamera hiyo na mifumo yake inatarajia kuingia sokoni katikati ya mwezi Februari mwaka huu. 

“Picha za michezo na vyombo vya habari hutumia upigaji picha wa mbali sana kuchukua picha kutoka pembe tofauti ambazo haziwezi kufikiwa na njia za kawaida za upigaji picha,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kamera hiyo ni muendelezo wa ubunifu na uvumbuzi wa mifumo ya kidijitali inayorahisisha utendaji kazi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, licha ya kuwa inaweza kuleta matokeo hasi hasa kuchukua nafasi ya watu ambao wanapiga picha za kawaida. 


Zinazohusiana: 


Sifa za kamera hiyo

Nukta (www.nukta.co.tz)  inakuletea uchambuzi wa sifa za kamera hiyo ambapo itakuwa msaada mkubwa kwa wapiga picha na waandishi wa habari kupata picha wanazozihitaji hata katika maeneo ambayo hawawezi kufika kirahisi.

Kamera hiyo inafanya kazi kwa kuwekwa kwenye kifaa kinachoendeshwa na kompyuta ili kupata picha nzuri kutoka kona yoyote ya eneo analotaka mpiga picha kwa kutumia remoti (remote control) ambayo ina uwezo wa kufanya kazi na kamera zaidi ya moja.

Pia inatumia mfumo wa kompyuta kuangalia picha zilizokwisha kupigwa na kamera iliyopo kazini kwa muda husika ili kupata matokeo yaliyokusudiwa. Ina uwezo wa kurekodi au kupiga picha ya tukio fulani kwa haraka na kwa urahisi.

Faida kubwa ya kamera hiyo ni kuwa Itakuwa inatatua changamoto ya muda na gharama kwa kupata picha nyingi kwa wakati mmoja kwa kutumia teknolojia ya kuendesha kamera nyingi.