October 6, 2024

Kijana anayetikisa mitandao ya kijamii kwa utamaduni wa Kimasai

Licha ya kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake, kijana huyo ameamua kuitafuta ndoto yake akibaki na uhalisia wake.

  • Ni Kili Paul ambaye hivi karibuni video zake zimevuma katika mtandao wa Instagram akiwa anacheza muziki huku amevalia mavazi ya Kimasai.
  • Licha ya kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake, kijana huyo ameamua kuitafuta ndoto yake akibaki na uhalisia wake.
  • Imani ya kijana huyo ni kuishi maisha ya furaha kwa kufanya kitu unachokipenda.

Dar es Salaam. Matumizi ya mitandao ya kijamii ni kitu cha kawaida miongoni mwa vijana. Wengine huitumia kwa ajili ya kuwasiliana, burudani na wengine kibiashara ili kujiingizia kipato huku wengine wakiitumia mitandao hiyo kwa ajili ya kuongeza maarifa na ujuzi.

Miongoni mwa vijana wanaotumia mitandao ni Kilimanjaro Kimesera (26) anayefahamika kama @kili_paul katika mtandao wa Instagram ambaye ameamua kutumia mitandao ya kijamii kutangaza utamaduni wa Kimasai na kufuata ndoto yake ambayo alishindwa kuifikia hapo awali.

Huenda umekutana  na moja ya video za Kili katika mtandao wa Instagram na TikTok siku za hivi karibuni. Tofauti na wengi wanaopakia maudhui ya kucheza muziki katika mitandao ya kijamii, Kili anaonekana akiwa amevalia mavazi kamili ya kimasai huku tabasamu lake likikulazimisha kutaka kufahamu zaidi kupitia ukurasa wake.

Powered by embedinstagramfeed pt &

Nyuma ya tabasamu la Kili ni simulizi ambazo huenda zikawafumbua macho baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakisubiria muujiza kujikwamua kimaisha huku kisingizio kikiwa ni kukosa ujuzi na elimu.

Mbegu iliyozikwa ardhini

Ni tamaduni miongoni mwa kabila la Kimasai kwa mvulana kuwa sehemu ya jamii na kusaidia shughuli za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuchunga na kusimamia mifugo.

Hata hivyo kwa Kili ambaye ni mkazi wa Lugoba mkoani Pwani, hali ilikuwa tofauti kwani mama yake alichagua kumpeleka shule badala ya kubaki nyumbani. 

Siyo kuwa mama Kili alimiliki kundi kubwa la mifugo kufanikisha elimu ya mtoto wake, alikuwa akijihusisha na biashara ya dawa asili za kimasai na pesa aliyoipata, aliiwekeza katika elimu ya mtoto wake.

“Baba yangu ni mtu makini sema ana kunywa pombe kiasi cha kutokuweza kuniendeleza kielimu. Mama ndiyo alikuwa nguzo yangu kielimu,” amesema Kili.

Wakati akiwa na miaka mitano Kili alianza kusoma shule ya msingi Lugoba ambapo alisoma hadi darasa la nne na mama yake alimhamishia Mkoa wa Dodoma katika Shule ya Msingi Uhuru kwa miezi mitatu na kisha kuhamishiwa Shule ya Msingi Amani mkoani humo ambapo alipohitimu darasa la saba na kufauru na kuchaguliwa kwenda Shule ya Sekondari Hazina ya Dodoma.

“Nilipoanza elimu ya sekondari, mama alifariki hivyo nililazimika kuacha shule na kurudi nyumbani kuchukua nafasi yangu katika jamii,” Kili ameieleza Nukta Habari (www.nukta.co.tz). 

Baada ya msiba wa mama yake, Kili aliamriwa na baba yake kurudi nyumbani kuchukua nafasi yake kama Morani kwa kuangalia mifugo na kuwajibika katika jamii yake kwani hakukuwa na fedha kumuendeleza kielimu.

Kwa Kili, hakuwa na budi bali kukubaliana na ukweli wa kuwa ndoto zake za kuwa mcheza muziki na kuwa muigizaji zimefikia tamati.


Soma zaidi:


Safari ya mapito iliyoamsha ndoto

Hata baada ya kurudi nyumbani, Kili aliendelea na majukumu yake kama Morani ikiwemo kuchunga ng’ombe za familia yake na kuwa sehemu ya ulinzi wa jamii. Alikubaliana na hali kwani hakuwa na namna.

Hata hivyo, umri ulizidi kuenda na alihitji kutengeneza fedha zake mwenyewe na hapo ndipo ilimlazimu aanze kutafuta kazi. 

Alipata ajira Shinyanga kama mlinzi wa mgodini na baadaye aliamua kuanza uchimbaji kutokana na fedha aliyopata kama mlinzi kutokumtosha. 

Baada ya kuachana na uchimbaji, alirudi nyumbani alipokaa kwa miaka mitatu na akaamua kuenda Zanzibar ambapo pia alifanya kazi kama mlinzi na baadaye kugeukia uuzaji wa vinyago ufukweni.

“Mzee hakutaka niendelee na kazi ya uchimbaji kwani ni hatari. Nilirudi nyumbani,” amesema Kili ambaye aliacha na kazi hizo na kurudi nyumbani kusimamia mifugo ya baba yake.

Katika kipindi chote hicho cha mizunguko, alikuwa akijifunza lugha ya Kiingereza na kujifunza mitindo mbalimbali ya kucheza muziki.

Shughuli hizo ziliuwasha moto wa kipaji chake ambacho kilikua kimezimika na kuwa chachu ya kukionyesha kwa dunia kwa njia ya mtandao.

“Nilikusanya fedha na kununua simu ya Sh500,000 ambayo naitumia kurekodi video zangu na kuziweka mtandaoni. Ninaiweka simu yangu kwenye mti na kurekodi video,” amesema Kili ambaye kwa sasa yupo nyumbani Lugoba ambapo anaendelea na ufugaji.

Baada ya kuachana na uchimbaji, alirudi nyumbani alipokaa kwa miaka mitatu na akaamua kuenda Zanzibar ambapo pia alifanya kazi kama mlinzi na baadaye kugeukia uuzaji wa vinyago ufukweni. Picha| Kili Paul.

Mtandao wampokea Kili kwa meno 32

Licha ya kuwa ilikuwa ni ngumu kwa familia yake kukubaliana na uhalisia wa kuwa Kili ameanza kufuata ndoto yake, ilichukua muda na nguvu nyingi kwa kijana huyo kuwaelewesha.

“Familia yangu iliniambia kuwa nimerogwa lakini tangu nianze kuwaelezea uhalisia, wameanza kuheshimu ninachokifanya. Ninawaonyesha pesa ninazozipata TikTok na sasa hawashangai tena,” ameelezea kili ambaye katika mtandao wa Instagram amejizolea wafuasi zaidi ya 42,000.

Kutokana na umaarufu wake katika mtandao wa Instagram, Kili amekuwa akitafutwa na baadhi ya wasanii wakimwambia acheze nyimbo zao ili wamlipe lakini linapokuja suala a pesa, wengi hutokomea kusikojilikana.

Hata hivyo, kijana huyo bado ana hamasa ya kuendelea kuwakilisha vyema kabila la Wamasai huku akiendeleza kipaji chake na akitumaini siku moja kufika pale anapotazamia.

“Ninahamasika sana vile msanii wa nchini Marekani Chris Brown anavyocheza. Pia, Marehemu Michael Jackson ananikosha sana. Mitandao ya kijamii imenikutanisha na mashabiki wengi kutoka Marekani na natazamia kuendelea kufanya vizuri zaidi kukuza kipaji changu.” amesema Kili.

Kwa muda wote akirekodi video zake, Kili huvalia mavazi ya kimasai na kwake ni namna ya kuifikisha ujumbe na asili yake kwa dunia.

“Sina uhakika na jinsi kesho itakavyokuja. Mimi ninaiishi leo na sijui mitandao ya kijamii itanipeleka wapi lakini mimi nipo tayari kwa lolote,” amesema Kili ambaye hupata muda wa kuwafundisha wadogo zake kucheza pale wanapohitaji.

Leo umepata simulizi ya Kili, Je, ni nani mwingine ambaye unafahamu anatumia mitandao ya kijamii kwa matokeo chanya? Mtag ama utuandikie mawasiliano yake kupitia mitandao ya kijamii @NuktaTanzania Facebook, Twiter na @nuktatz Instagram.