Kipaji chamuwezesha kumiliki kampuni iliyoajiri wafanyakazi 17
Alisomea taaluma ya uhasibu lakini akaamua kutumia kipaji chake kuanzisha kampuni ya teknolojia.
- Ni mwanzilishi wa kampuni ya Magilatech, Godfrey Magila.
- Alisomea taaluma ya uhasibu lakini akaamua kutumia kipaji chake kuanzisha kampuni ya teknolojia.
- Amefanikiwa kuajiri wafanyakazi 17 wanaotoa huduma ya utengenezaji wa mifumo endeshi na ulinzi mtandaoni.
Dar es Salaam. Huenda ukawa miongoni mwa watu walio na fikra ya kufanyia kazi kile tu ulichosomea chuoni ili kujipatia kipato kuendeleza maisha yako.
Wakati mwingine fikra hizo zinakuwa sahihi kama taaluma ya ujuzi na maarifa uliyoyapa shuleni yanakidhi matarajio na haja ya moyo wako.
Lakini kuna kila sababu pia, kutoa nafasi kwa vipaji tulivyozaliwa navyo vijidhihirishe ili vilete matokeo chanya hasa katika kutatua changamoto za jamii kwa namna mbalimbali.
Jambo la muhimu ili vipaji vyetu vilete matokeo chanya, vinatakiwa vinolewe na kuhuishwa kwa mafunzo na maarifa mbalimbali.
Mwanzilishi wa kampuni ya teknolojia ya Magilatech, Godfrey Magila ni moja ya vijana walionufaika na vipaji walivyozaliwa navyo kuliko taaluma walizosomea wakiwa shuleni.
Magila aliyesomea masomo ya uhasibu katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) mara baada ya kumaliza masomo yake hakwenda kuwa Mhasibu licha ya kuwa fursa ilikuwepo kuingia katika kazi hiyo.
Badala yake akaamua kufanya kile anachokipenda ambacho kilianza kujidhirisha tangu akiwa mdogo. Alipenda sana masuala ya teknolojia hasa mifumo ya kompyuta. Bila hiana ameingia huko na faida inaonekana.
“Nimejifunza mwenyewe kila kitu. Toka niko mdogo shule ya msingi, toka zamani nilikuwa mtundu napenda masuala ya teknolojia, japo nilichukua masomo ya ziada baadae.” amesema Magila.
Magila ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo amefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 17 wanaofanya kazi katika kampuni hiyo.
Kampuni ya Magilatech iliyoanzishwa mwaka 2012 inahusika na utengenezaji wa mifumo endeshi (Software development) na ulinzi wa mifumo ya mtandaoni (Cyber security) ya kampuni mbalimbali nchini Tanzania.
Mpaka sasa, Magilatech imefanikiwa kufanya kazi na makampuni mbalimbali zikiwemo za simu za mkononi za Tigo na Airtel katika kuwatengenezea mifumo endeshi inayoweza kutatua changamoto za wateja wake ikiwemo wizi wa simu na taarifa za wateja.
Makampuni na taasisi nyingine ambazo zimefanikiwa kufanya kazi na Magilatech ni pamoja na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), VETA na taasisi mbalimbali nje ya Tanzania.
Kutokana na uwezo wa Magila kugusa maisha ya watu kupitia mifumo endeshi na usalama mtandaoni, imekuwa ikitambuliwa na taasisi kubwa duniani ambapo mwaka 2017 ilishinda tuzo ya “Africa Business Leaders Awards” (AABLA Innovator of the Year) inayotolewa na kampuni ya CNBC Africa ya Afrika Kusini.
Katika kujiimarisha zaidi siku zijazo, Magilatech inalenga kuongeza wigo wa kuwafikia watu na kampuni mbalimbali zinazokabiliwa na changamoto ya mifumo endeshi na usalama mtandaoni.
“Moja ya vipaumbele vyetu ni kuwafikia Watanzania kama soko letu, kuna changamoto nyingi bado hazijatatuliwa ndiyo tunalenga kuzitatua kwanza ndipo tutaenda nje,”amesema Magila.