October 6, 2024

Kuna nini jukwaa la Clubhouse?

Wabunifu kutoka kampuni ya teknolojia ya Alpha Exploration ya nchini Marekani wameingiza sokoni app ya Clubhouse ambayo huenda watu wengi bado hawaifahamu licha ya kuja kwa mfumo tofauti na mitandao mingine ya kijamii.

  • Ni app ambayo inaruhusu mijadala kwa njia ya sauti kwa watu ambao hawafahamiani.
  • App hiyo inaweza kuwa ya manufaa kwa waandishi wa habari kukusanya maoni ya watu na wanafunzi kufanya majadiliano ya masomo.
  • Hadi sasa, app hiyo inapatikana katika simu za iPhone tu.

Dar es Salaam. Kila kukicha, wabunifu wa teknolojia wanaamka na programu tumishi za simu (apps) mbalimbali zinazoingia sokoni na kuanza kupakuliwa na watumiaji wanaohitaji huduma zinazokuja na app hizo ili kurahisisha maisha

App hizo zinagusa kila nyanja ya maisha ikiwemo michezo, elimu, afya, jamii, mawasiliano, kilimo, unaweza kutaja kadiri uwezavyo na ni chaguo lako utumie ipi kulingana na mahitaji yako.

Hivi karibuni, wabunifu kutoka kampuni ya teknolojia ya Alpha Exploration ya nchini Marekani wameingiza sokoni app ya Clubhouse ambayo huenda watu wengi bado hawaifahamu licha ya kuja kwa mfumo tofauti na mitandao mingine ya kijamii iliyopo sokoni.

Tofauti na Instagram na mitandao mingine ambayo inahusisha picha, kupigiana simu za video na sauti na hata “kulike” na “kucomment”, Clubhouse ni app ambayo inaruhusu mawasiliano kwa njia ya sauti na mawasiliano hayo yanafanyika kwa njia ya mijadala.

Kwa sasa app hiyo inaweza kupakuliwa na kutumiwa na watu wanaomiliki simu za iPhone pekee. 

Nini kipya ndani ya Clubhouse? 

Mijadala ya sauti na watu mbalimbali

Katika mitandao mingine, kuingia katika makundi ni hadi upate mwaliko ili uwe mmoja wa makundi hayo na utalazimika kujiunga nayo ili uendelee na mazungumzo yaliyomo ndani humo. 

Kwa Clubhouse inayopatikana katika maduka mbalimbali ya mtandaoni likiwemo la Google Play Store, wakati wa kujiunga unapata nafasi ya kuchagua vitu ambavyo unafurahia katika sekta za michezo, burudani, elimu, mtindo maisha na kadhalika.

Katika vipengele hivyo, mada zinapoanzishwa zinazogusa vipengele unavyovipenda, utaziona ukifungua app hizo hivyo unaweza kujiunga na kusikiliza na hata kupata nafasi ya kuchangia kwa kunyoosha mikono kama ilivyo katika video za Zoom na Google Meet.

Kwa sasa app hiyo inaweza kupakuliwa na kutumiwa na watu wanaomiliki simu za iPhone pekee. Picha| YouTube.

Burudani na habari za sekta unazopenda

Kupitia app hiyo utafahamu yanayoendelea katika sekta unazopenda ambazo utachagua wakati unajiunga na app hiyo. Mbali na kufahamu, unaweza kupata nafasi ya kusikia maoni ya watu wengine juu ya sekta hizo.

Vipo vyumba vya mijadala katika app hiyo ambavyo aliyeanzisha anaweza kusikilizisha waliojiunga muziki, maigizo na kadhalika. Pia wapo ambao wanaanzisha vyumba vya mijadala kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa mada kadha wa kadha. Ni wewe uingie chumba unachotaka. 

Hivi ndivyo unavyoweza kutumia app hiyo

Utahitaji kupakua app ya Clubhouse katika duka la programu mtandaoni na kisha kuweka taarifa zako ikiwemo jina, namba ya simu na jina unalohitaji kutumia (handle).

Baada ya hapo utahitaji kumpata mtu ambaye yupo katika mawasiliano yako ambaye anaitumia app hiyo ili akutumie mwaliko kwani tofauti na hapo, hautoweza kuitumia app hiyo.

Baada ya kupokea mwaliko, utaingia katika kiunganishi atakachokutumia rafiki yako na kisha utaanza kutumia mtandao huo kadiri upendavyo. 


Soma zaidi:


Nani anafaa kutumia app ya Clubhouse?

  1. Waandishi wa habari

Wanaweza kutumia app hiyo kuendesha mijadala kuhusu mada mbalimbali au pia kupata maoni juu ya jambo fulani bila udhibiti wa muda, mipaka ya nchi kwani watu kutoka nchi mbalimbali wana uwezo wa kujiunga na mijadala unayoanzisha.

  1. Wanafunzi kwa ajili ya masomo

Kwa sasa wanafunzi wanatumia WhatsApp kuwasiliana lakini changamoto kubwa ni kuwa baadhi hushindwa kuchangia wakati mijadala inaendelea.

Ndani ya Clubhouse, utaona kila mtu ambaye yupo mtandaoni (online) na kama mwanzilishi au muendesha kipindi, unaweza kumpatia nafasi mtu yeyote aliyepo mtandaoni kuchangia mawazo yake.

Nguvu ya kutoa nafasi kwa mzungumzaji ipo kwa waendesha kipindi (moderators) na mwanzilishi wa chumba cha mjadala na hivyo inakuwa rahisi kuendesha mijadala hiyo.

  1. Watu wanaofanya mikutano

App ya Clubhouse pia inaweza kuruhusu watu kufanya mikutano yao lakini huenda pasiwe na faragha kwani mtu yeyote anaweza kuingia na akasikiliza maongezi yenu.

Katika kipindi hichi ambacho, watu wanaonana kwa nadra ili kujikinga na corona, jukwaa hili linaweza kuwa sahihi kufanya vikao, warsha, semina na mikutano rasmi na isiyo rasmi. 

Ndani ya Clubhouse, utaona kila mtu ambaye yupo mtandaoni (online). Picha| PC Mag.

Jipange kwa haya kabla hujaanza kutumia app hiyo

Kama app zingine, ClubHouse  inatumia intaneti kufanya kazi hivyo huenda ikawa ni changamoto kwa watu ambao intaneti ni shida. 

Kwa sasa mtandao huo unapatikana katika simu za iPhone tu huku taarifa za ujio wake katika simu za Android ukiwa bado haufahamiki.

Tuambie wewe unatumia app ipi kuwasiliana na kufanya mijadala ukiwa mtandaoni?

Usiache kufuatilia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kwa habari za teknolojia zinazokuhusu.