October 6, 2024

Kutana na kijana aliyedhamiria kupanda miti milioni 20 ifikapo Januari 2020

Mr Beast ambaye alianza safari hiyo Oktoba 25, 2019, alifanikiwa kupanda miti 300 kwa siku moja akishirikiana na marafiki zake wasiopungua 10.

  • Ni baada ya kufikisha wafuasi milioni 20 kwenye mtandao wa YouTube.
  • Ameanza na kupanda miti 300 kwa siku moja.
  • Wadau mablimbali wamshika mkono.

Dar es Salaam. Wakati vijana wengi wanaomiliki simu janja hutumia mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Youtube kwa ajili ya kusambaza  picha zao au matukio mbalimbali yanayowazunguka na wakati mwingine fursa.

Hali hiyo ni tofauti kabisa kwa kijana wa Marekani, Jimmy Donaldson maarufu kama Mr Beast  ambaye kupitia mtandao wa YouTube alikuwa anaweka maudhui ya kutisha, sasa amebadidilisha mtazamo wake  kuhusu mitandao ya kijamii baada ya kuamua kupanda miti milioni 20 hadi ifikapo Januari 2020.

Mr Beast ambaye alianza safari hiyo Oktoba 25, 2019,  alifanikiwa kupanda miti 300 kwa siku moja akishirikiana na marafiki zake wasiopungua 10 ambapo watapanda miti hiyo katika maeneo mbalimbali duniani wakishirikiana na wana mazingira kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Safari hiyo itakayochukua miezi minne ilianza kuonekana kama haiwezekani lakini sasa imepata hamasa baada ya  wadau mbalimbali kujtokeza kuungana na mtumiaji huyo wa mitandao ya kijamii. Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Beast #teamtrees kampeni hiyo imefanikiwa kukusanya takribani Sh18.4 bilioni.

Jimmy Donaldson (wa kwanza kushoto) akiwa na wenzake wakati kueneza kampeni ya upoandaji miti kwa hamasa ya channeli yake ya Youtube. Picha| Mr Beast. 

Katika kuunga mkono kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Youtube,  Susan Wojcicki amechangia  Sh460.6 milioni kuhakikisha kampeni hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa. 

Uendeshaji wa kampeni hiyo ni wa njia ya kuchangishana fedha ambapo kila mtu mwenye nia ya kuchangia anatakiwa kutoa Sh2,303 ili kumwezesha  Mr Beast na wenzake wa #teamtrees  kupanda miti kwa kusaidiana na wana mazingira mbalimbali ulimwenguni.

Wadau wengine waliomuunga mkono Beast ni Tobias Lutke ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya manunuzi ya mtandaoni ya Shopify (@tobi) ambaye amechangia kiasi ambacho kitawezesha Beast na wenzake kupanda miti ipatayo milioni 1 huku Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Twitter akiungana na timu hiyo kwa kuchangia kiasi ambacho kitasaidia kupanda miti ipatayo 150,000.

Hadi kufikia leo (Novemba 1, 2019) saa 6:52 mchana, takwimu mubashara za tovuti ya #teamtrees zinaonyesha kuwa miti milioni 11.3 imepandwa kwa michango iliyotolewa.


Zinazohusiana


Fahamu zaidi

Mr Beast ni kijana wa umri miaka 21, alizaliwa mwaka 1998  huko Greenville Kaskazini mwa Carolina nchini Marekani. Alifikia maamuzi ya kupanda miti kama hisani baada ya kufikisha wafuasi  milioni 20 kwenye mtandao wa Youtube.

Wafuasi hao ni wapenzi wa video zake  ambazo amekuwa  akirekodi vitu vya ajabu ikiwemo kusimama juani siku nzima, kukaa kwenye mvua na hata kushinda jangwani kisha kusambaza video hizo.

Wafuasi hao walimtaka kupanda miti kwenye video yake atakayoifanya na Beast aiitikia wito huo na kuanza kampeni hiyo. Hadi kufikia leo Novemba 1 ,2019 mtandao wa Youtube wa Mr Beast umefanikiwa kuwa na wafuasi wapatao milioni 29.  

Wadau mbalimbali wa mtandao akiwemo Kennedy William ambaye anasomea masomo ya sayansi ya mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) amesema hatua hiyo ni hatua nzuri hasa ikizingatiwa kuwa Beast anatumia mtandao kufanya shughuli za kijamii. 

“Ni matumizi mazuri ya mtandao. Sasa  hivi tabianchi imebadilika na hali ya hewa haitabiriki kabisa. Hii yote ni kutokana na uchafuzi wa mazingira na ukataji wa miti kiholela,” amesema William.