July 8, 2024

Kutana na shirika linalosaidia wanafunzi wa Tanzania kujifunza kwa teknolojia ya kisasa

Mpaka sasa, shirika hilo imewafikia wanafunzi zaidi ya 100,000 na walimu zaidi ya 3,000 Tanzania wanaofundishwa namna ya kutumia teknolojia katika kujifunzia na kufundisha.

  • Mpaka sasa, shirika hilo imewafikia wanafunzi zaidi ya 100,000 na walimu zaidi ya 3,000 Tanzania. 
  • Linawasaidia wanafunzi na walimu kupata mafunzo yatakayowasaidia kurahisisha mchakato wa kujifunza katika masomo mbalimbali na kutoa vifaa vya dijitali.

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu yakianza kushika kasi nchini, Shirika  la Kimataifa kutoka Uingereza limeongeza nguvu katika kufanikisha  jitihada hizo kwa kuboresha mazingira rafiki ya ufundishaji na kujifunzia kwa kutumia Tehama. 

Shirika hilo la kiraia liitwalo Camara Education linatumia teknolojia kuboresha elimu kwa kupeleka vifaa vya kidigitali kujifunzia kama Kompyuta, kutoa elimu kwa walimu na wanafunzi juu ya matumizi ya vifaa hivyo katika shule za msingi na sekondari za serekali na binafsi. 

Ili kuhakikisha uendelevu katika matumizi ya tehama katika shule hizo, shirika hilo pia hutoa huduma za urekebishaji wa vifaa hivyo vya kielektroniki pindi vinapopata hitilafu.

Camara Education linaungana na wadau wengine wanaohamasisha matumizi ya teknolojia katika elimu kama Jenga hub, Ndoto hub, Shule Direct na wengineo ambao ama wanatumia teknolojia kuongeza ufanisi wa kujifunza ama kuwafundisha wanafunzi na walimu teknolojia mbalimbali za sasa ili waweze kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa.

Utoaji wa vifaa hivyo unaenda sanjari na usambazaji wa maudhui mbalimbali yanayoendana na mitaala iliyopo katika vifaa vinavyopelekwa shuleni itakayowasaidia wanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi.

Ili kuhakikisha lengo lao linatimia, wanafanya kazi kwa ukaribu na walimu kuhakikisha elimu ya matumizi ya vifaa hivyo vya Tehama inatumika kwa wanafunzi katika mifumo yao ya kujifunza wanapokuwa shuleni. Picha | Camara Education.

Afisa Programu msaidizi wa shirika hilo nchini, Asia Bonanga ameiambia www.nukta.co.tz amesema wanataka kuongeza matumizi ya teknolojia katika mfumo wa elimu ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa zana za kisasa na elimu juu ya matumizi sahihi ya teknolojia katika elimu. 

Mpaka sasa, shirika hilo imewafikia wanafunzi zaidi ya 100,000 na walimu zaidi ya 3,000 Tanzania wameliopewa mafunzo juu ya matumizi ya vifaa hivyo vya kidigitali.

Sanjari na elimu kwa wanafunzi na walimu, shirika hilo limezifikia shule na taasisi za elimu zaidi ya 700 kutumia teknolojia katika elimu huku ikitoa vifaa zaidi ya 5000 nchini kote. 

Ili kuhakikisha lengo lao linatimia, wanafanya kazi kwa ukaribu na walimu kuhakikisha elimu ya matumizi ya vifaa hivyo vya Tehama inatumika kwa wanafunzi katika mifumo yao ya kujifunza wanapokuwa shuleni.

“Tunafanya kazi na shule nchi nzima, tumefikia shule kuanzia Pemba mpaka Sumbawanga. Lengo letu ni kufikia shule nyingi zaidi ya tulizofikia na kuona elimu ya Tanzania inaendeshwa kidigitali,” amesema Asia.


Zinazohusiana:


Mbali na kutoa elimu na vifaa, Asia amesema wanaendelea kufanya kazi na taasisi mbalimbali za elimu kuhakikisha mitaala inaboreshwa ili kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu nchini. 

Katika kipindi kifupi tangu Shirika hilo lianze kufanya kazi mwaka 2012 Tanzania, Moja ya changamoto inayowakumba ni pamoja na miundombinu isiyo rafiki kama upatikanaji wa umeme katika shule wanazozihudumia zilizopo vijijini.

Mbali na changamoto hiyo, Shirika litatakiwa kukabiliana na uhaba wa vyumba vinavyoweza kutumika kujifunzia masomo ya kompyuta katika shule mbalimbali zinazokusudia kupatiwa elimu hiyo.

Matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu yamekuwa yakihamasishwa zaidi ulimwenguni kwa sasa ili kuhakikisha wanafunzi wanaongeza ufanisi katika masomo yao na walimu kuwa na mazingira rafiki yatakayowasaidia kufundishia na kuwa bora zaidi katika teknolojia miaka ijayo.