Kwa nini mkalimani amezua gumzo mtandaoni Tanzania?
Ni aliyekosea kutafsiri sehemu ya hotuba ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wakati wa kuaga mwili wa hayati Magufuli jijini Dodoma.
- Ni aliyekosea kutafsiri sehemu ya hotuba ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wakati wa kuaga mwili wa hayati Magufuli jijini Dodoma.
- Baadhi ya watu wasema aliteleza ulimi huku wengine wakisema amekosa umakini na weledi wa kazi yake.
Dar es Salaam. Mkalimani ambaye alikuwa akifanya kazi ya kutafsiri hotuba za viongozi mbalimbali wakati wa kuagwa mwili wa Hayati Rais John Magufuli amezua gumzo mtandaoni baada ya kukosea kutafsiri sehemu kadhaa za baadhi ya hotuba za viongozi ikiwemo Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Mkalimani huyo alikuwa akitafsiri lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili katika shughuli hiyo iliyohudhuliwa na wananchi na viongozi mbalimbali iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Machi 22, 2021.
Licha ya kuwa alifanya vizuri katika kutafsiri hotuba zilizotolewa na marais tisa wa nchi za Afrika lakini alijikuta katika wakati mgumu wakati akitafsiri sehemu ya hotuba ya Ramaphosa ambayo alikuwa akiisoma kwa Kingereza.
Katika hotuba hiyo Ramaphosa amesikika akisema “… I say we were honoured because President Magufuli was not a traveller, he didn’t like travelling very much…”
Hata hivyo, mkalimani akatafsiri kwa Kiswahili kuwa “…nilijisikia kuheshimiwa sana kwa sababu Mheshimiwa Magufuli alikuwa ni mtu imara mwenye upendo ambaye alipenda kusikiliza na kuweza kutoa mwongozo kwa wenzake…”
Minong’ono ya watu waliokuwepo uwanjani hapo ilisikika kuashiria kuwa mkalimani huyo ameteleza ulimi katika tafsiri yake.
Kimsingi Rais Ramaphosa alimaanisha kuwa “Rais Magufuli hakuwa msafiri, hakupenda sana kusafiri. Alipendelea kukaa Tanzania.”
Hata hivyo, baadaye aliomba msamaha kuwa hakusikia vizuri alichokisema Rais Ramaphosa.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
Kutokana na kosa hilo la kiufundi kwenye tafsiri, jambo hilo limezua gumzo kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter huku wengine wakohoji umakini na weledi wa mkalimani huyo.
Wengine wamesema changamoto kama hizo zinatokea kwenye kazi lakini umakini wa hali ya juu unahitajika kupunguza makosa.
Nini cha kuzingatia wakati ukalimani?
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia ana taaluma ya ukalimani, Faraja Lugome amesema inawezekana mkalimani alipewa hotuba kabla akawa anasoma kutoka kwenye hotuba, jambo ambalo ni kosa kubwa kwa sababu mkalimani hutakiwi kusoma kwani mzungumzaji anaweza kubadilisha alichoandika au kuandikiwa.
“Lakini pia yawezekana mkalimani alihisi alichoongea mzungumzaji hakifai kusikika kwa hadhira ile ikabidi abadilishe. Bahati mbaya akashtukiwa,” Lugome wakati aliiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Mtaalamu huyo wa lugha katika Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya UDSM amesema pia inawezekana mkalimani alichoka akili ingawa hilo halina mantiki sana.
“Ila sitaki kuamini kuwa uelewa wake wa lugha ni mdogo,” amesema Lugome na kubainisha kuwa kikubwa kwenye kazi hiyo kinachohitajika ni umakini wa kusikiliza na kufikisha ujumbe upande wa pili kama ulivyosemwa na mzungumzaji.
“Hutakiwi kukalimani ukiona akili imechoka. Ndiyo maana wanatakiwa kuwa wakalimani wawili ili wapokezane,” ameshauri mtaalam huyo.