Magufuli asogeza mbele muda wa mwisho wa kusajili laini kwa alama za vidole
Rais John Magufuli ameongeza siku 20 kwa watu watakaoshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole ifikapo Desemba 31 na ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima laini ambazo hazijasajiliwa baada ya muda huo kupita.
- Ameongeza siku 20 kuanzia Januari 1 hadi 20, 2020.
- Amefanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole akiwa Chato.
- Baada ya muda huo kupita, TCRA haitaongeza muda mwingine.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameongeza siku 20 kwa watu wote watakaoshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole ifikapo Desemba 31 na ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima laini zote ambazo hazijasajiliwa baada ya muda huo kupita.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo (Desemba 27, 2019) mara baada ya kusajili laini yake kwa kutumia alama za vidole akiwa katika mapumziko nyumbani kwake Chato mkoa wa Geita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo, Rais Magufuli ameongeza siku 20 kuanzia Januari 1 hadi 20, 2020 kwa watu wote ambao watakaokuwa bado hawajasajili laini zao ifikapo mwisho wa mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuugua na kukamilisha kupata namba za vitambulisho vya Taifa.
“Rais Magufuli amesisitiza kuwa baada ya muda huo hakutakuwa na kisingizo chochote kitakachokubalika na ameagiza TCRA kuhakikisha laini ambazo hazijasajiliwa zinazimwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Amewasisitiza Watanzania wote wahakikishe laini zao za simu zinasajiliwa kwa alamu za vidole kama ilivyoelekezwa na TCRA.
— Gerson Msigwa (@MsigwaGerson) December 27, 2019
Ameongeza kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi ikiwemo kudhibiti vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu wa mali za wananchi ikiwemo fedha.
Mfumo wa kusajili laini kwa kutumia laini za vidole (Biometric Registration) ulizinduliwa Machi 1, 2018 na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya kuwapo vitendo vya watumiaji wa huduma hiyo kugushi vitambulisho au kutumia vitambulisho vya watu wengine.
Mfumo huo ilifanyiwa majaribio katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Tanga, Singida, Pwani, Iringa na Zanzibar ambapo kila mkoa ulikuwa na kituo kimoja cha usajili.
TCRA wanatekeleza mfumo huo kwa kushirikiana na watoa huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ambapo utasaidia kupata takwimu sahihi za watumiaji wa simu za mkononi na huduma za fedha kwa ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na uchumi wa Taifa.