October 7, 2024

Magufuli azuia fomu za maadili kurejeshwa mtandaoni

Asema wadukuzi ni wengi na faragha za wajazaji fomu zinaweza kupotea.

  • Asema wadukuzi ni wengi na faragha za wajazaji fomu zinaweza kupotea.
  • Awataka viongozi kujaza fomu hizo kabla ya Desemba 30, 2020.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameizuia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutumia mfumo wa Tehama kurejesha fomu zilizojazwa na viongozi kwa ajili ya kutunza faragha za wahusika akieleza kuwa siku hizi kuna “mahackers” (wadukuzi) wengi.

Dk Magufuli amemweleza Kamishna mpya wa Maadili Jaji Sivangilwa Mwangesi Alhamis (Desembea 24, 2020) jijini Dodoma kuwa matumizi ya mtandao katika mchakato wa ujazaji wa fomu hizo yanaweza yakatumika tu katika utoaji wa fomu hizo lakini si urejeshaji.

Kiongozi huyo wa juu wa nchi amesema kuwa alishakuwa amezungumza na aliyekuwa Kamishna wa Maadili marehemu Jaji mstaafu wa mahakama ya rufani Harold Nsekela na kukubaliana kuwa fomu zilizojazwa zisirejeshwe mtandaoni.

Jaji Mwangesi aliyeteuliwa na Rais Magufuli Desemba 23 mwaka huu amechukua nafasi ya marehemu Jaji Nsekela aliyefariki dunia hivi karibuni.

“Unaweza kufanya mambo mengine yote kwa njia ya mtandao lakini ajaze fomu kwa mfano Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) ndani ya fomu aeleze alichonacho na labda hata awe na nyumba ndogo aseme nina nyumba ndogo ambayo sijaitangaza kwa mke wangu halafu aiweke kwenye mtandao…halafu mtu awe anaijua ile ‘password’ (nywila), ule usiri na utakatifu wa idara hiyo mnaupoteza,” amesema Dk Magufuli baada ya kumwapisha

Rais Magufuli amesema baada ya kuzijaza fomu hizo ni vyema kila kiongozi akazirejesha mwenyewe mahali anapotakiwa kuzipeleka badala ya kuziskani na kuzituma mtandaoni.

“Ninajua wasaidizi wako watakuwa wamenielewa na inawezekana mheshimiwa marehemu Jaji Nsekela alikwishawapa hayo maelekezo kuwa ‘We are not supposed to be open that way’ (hatutakiwi kuwa wazi kiasi hicho) na ni lazima pawe na usiri wa fomu hizi.


Zinazohusiana: 


Katika hotuba yake fupi Ikulu, Chamwino, Rais Magufuli amesema mtu akishajua programu husika anaweza kuhariri kilichotumwa katika mtandao husika kwa kuwa “‘mahackers’ (wadukuzi wapo wengi).”

“Umejaza una milioni 10 akakujazia una milioni 100 halafu baadaye unakuja kuulizwa ulijaza una milioni 100 ‘signature’ (sahihi) yako ipo hapa…na originality (uhalisia) inapotea, kitu kilichopigwa photocopy (nakala), kikawa scanned (kikanakiliwa kielektroniki) hakiendani na kile kilichokuwa presented originally (kilichowasilishwa).

“Na saa nyingine aliyepokea akiiindorse (akithibitishe) pale chini kuwa amepokea. Hii tu ndiyo observation ninapenda niitoe kwa tume ya maadili, kamwe msikubali fomu hizi zirudishwe kwa njia ya mtandao,” amesema Dk Magufuli.

Hii ni mara ya pili ndani ya mwezi mmoja Rais Magufuli anasisitiza kupunguza matumizi ya mtandao katika baadhi ya masuala ya Serikali.

Mapema mwezi huu wakati akiwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri, Dk Magufuli aliwataka watumishi wa umma kupunguza matumizi ya mitandao ya kijamii kama makundi sogozi ya Whatsapp katika kutumia taarifa nyeti.