Makosa yanayoweza kukosesha pesa YouTube
Kulipwa na mtandao huo unatakiwa kwanza ukubali na kufuata sera ya malipo ya mtandao huo (YouTube monetization program) ambayo inakuhitaji uwe na walau wafuasi 1,000 kwenye chaneli yako.
- Hautakiwi kuweka maudhui yanayokinzana na sera za YouTube ikiwemo video za chuki, ukatili wa kijinsia na uchochezi.
- Pamoja na hayo ni maudhui yanayochochea ngono na ubaguzi wa rangi, kabila na Taifa.
- Unatakiwa kujiunga na mfumo wa malipo wa Youtube ili kupata pesa.
Dar es Salaam. Hakuna furaha kwa mtengeneza maudhui kama kupata tija ikiwemo fedha kutokana na kazi yake pale inapokubaliwa vizuri na wadau wa mtandaoni.
Mtandao wa YouTube umekuwa ni moja ya majukwaa muhimu ya mtandaoni ambayo watengeneza maudhui wakiwemo wanamuziki hutumia kutangaza kazi zao na kuwafikia watu wengi duniani ili kujipatia kipato.
Hata hivyo, baadhi ya watengeneza maudhui wa Youtube hawafaidiki na jukwaa hilo kwa sababu wanashindwa kufuata masharti ambayo mtandao huo umeweka.
Kulipwa na mtandao huo unatakiwa kwanza ukubali na kufuata sera ya malipo ya mtandao huo (YouTube monetization program) ambayo inakuhitaji uwe na walau wafuasi 1,000 kwenye chaneli yako.
Hata baada ya kufika hapo, siyo kila maudhui utakayoyaweka yatakuwezesha wewe kulipwa na mtandao huo kwa kila video, vipindi mubashara au picha utakazoweka.
Pamoja na vigezo hivyo, ukifanya makosa haya wakati wa kutumia mtandao huo hautaweza kufaidika au kupata mapato yatokanayo na matangazo ya mtandao huo:
Video zenye lugha ya matusi
YouTube imesema kuwa video zote zenye lugha chafu hazitoweza kuwekewa matangazo.
Mtandao huo umesema matumizi ya matusi kama “Fu**” mwanzoni mwa video na kubadilisha maandishi ya tusi kwa makusudi kwenye video na picha ya utambulisho (thumbnail) hakutoiweka video hiyo kwenye nafasi ya kuwekewa matangazo.
Hata hivyo, sheria hiyo haitozikuta video za muziki ambazo zimetumia maneno hayo mara moja moja.
Hautakiwi kuweka maudhui yanayokinzana na sera za YouTube ikiwemo video za chuki, ukatili wa kijinsia na uchochezi. Picha| Google Play.
Video zinazohamasisha fujo na uchafu
Hizi ni pamoja na video zinazoonyesha matendo ya fujo kama milipuko ya mabomu, uchafu, damu za watu na vinavyoendana na hivyo na matumizi ya silaha.
“Maudhui ambayo yamedhamiria kuonyesha damu, fujo au majeraha yanapowasilishwa bila kitu kingine hayafai kwa matangazo.
“Lakini kama unaonyesha hayo kwenye taarifa ya habari, maudhui ya kielimu, sanaa au makala hiyo inakubalika,” imeeleza Youtube.
Video zenye maudhui ya ngono
Maudhui hayo ni pamoja na video zinazochochea ngono na watu wanaoonyesha sehemu za siri kama matiti na makalio.
Hayo ni pamoja na kupakia video zilizovuja za ngono na video zinazotoa elimu ya ngono.
“Maudhui yanayohusisha dhima za ngono kwa kiasi kikubwa hazifai kwa matangazo. Hii inaweza isihusishe video za muziki na video za elimu ya ngono zenye grafiki,” imeeleza Youtube.
Zinazohusiana
- Hawa ndiyo wanamuziki wa kike wanaotikisa dunia kwa wafuasi wengi Youtube
- Teknolojia ilivyoibua wimbo wa “Mkono wa Bwana” wa Zabron Singers
- Programu za mauzo zinazoweza kuwatoa wanamuziki wa Tanzania
Maudhui yanayohamasisha chuki na ubaguzi
Maudhui yote ya video yanayohamasisha chuki. ukabila, ubaguzi wa rangi, utaifa, ulemavu, unyanyasaji wa kijinsia na dini.
“Maudhui ya mlengo huo yanayolenga kuchekesha yanaweza yasizingatiwe lakini endapo ucheshi wako haujakidhi vigezo, hautopata mtangazo,” imesema YouTube.
Pamoja na kundi hilo ni maudhui yanayolenga kukashfu mtu au kikundi fulani kwenye jamii, zinazolenga kuonea baadhi ya watu na zinazohamasisha matumizi ya dawa za kulevya na sigara yakiwemo matangazo yake.
Video zinazokinzana na maadili
Video hizo ni zile zenye maudhui ya ndoa za utotoni, udhalilishaji wa watoto na kijinsia, kujidhuru na utoaji mimba.
“Endapo maudhui hayo ni ya zamani na yakawasilishwa kwa mfumo wa makala na mijadala, yanaweza kufanyiwa matangazo,” imeandika YouTube.
Kama umekuwa ukitengeneza maudhui yenye mlengo wa makosa hayo hapo juu, angalia namna ya kurekebisha ili kuendelea kufaidika na mtandao huo.
Video zote zinazowekwa kwenye matandao wa YouTube zinatakiwa kufuata vigezo na masharti na maelekezo ya YouTube.