Mashine za kisasa zaleta ahueni kwa wagonjwa wa saratani Ocean Road
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imesema kununuliwa na kusimikwa kwa mashine mbili za kisasa za uchunguzi na tiba za saratani zenye thamani ya Sh9.5 bilioni kumesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba ya mionzi kutoka wiki sita hadi kufikia
- Zimesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba ya mionzi kutoka wiki sita hadi kufikia wiki mbili.
- Pia Serikali imeokoa takriban Sh10.4 bilioni za kuwasafirisha wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.
- Mashine hizo aina ya “Linear Accelerator” (LINA) zinazotumia teknolojia ya 3D kutibu saratani.
Dar es Salaam. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imesema kununuliwa na kusimikwa kwa mashine mbili za kisasa za uchunguzi na tiba za saratani zenye thamani ya Sh9.5 bilioni kumesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba ya mionzi kutoka wiki sita hadi kufikia wiki mbili.
Mashine hizo aina ya “Linear Accelerator” (LINA) zinazotumia teknolojia ya 3D zina vifaa vya kisasa vya kutambua saratani kwa haraka katika mwili wa binadamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage amewaambia wanahabari leo (Desemba 2, 2019) Jijini Dar es Salaam kuwa tangu mashine hizo zianze kutoa huduma za uchunguzi na tiba Septemba 2018 tayari wagonjwa 1,141 wamepatiwa matibabu.
Amesema kabla ya kununuliwa kwa mashine hizo, taasisi yake ilikuwa inatumia mashine za LINA zinazotumia teknolojia ya 2D jambo lililokuwa likiwafanya wagonjwa wasubiri wiki sita kupata tiba hiyo.
“Tumepata mafanikio mengine kutoka na mashine kuwepo, tumeweza kupunguza wa wagonjwa kusubiri tiba kutoka wiki sita hapo awali lakini sasa hivi ni ndani ya wiki mbili,” amesema Dk Mwaiselage.
Amesema tangu kufungwa kwa mashine hizo kumeongeza kasi ya matibabu ya saratani na kupunguza rufaa za wagonjwa waliokuwa wanapelekwa kutibiwa nje ya nchi ikiwemo India.
“Tangu mashine hizi zimefungwa na kuanza kutoa huduma Septemba, 2018 mpaka Novemba mwaka huu tumeweza kuhudumia wagonjwa 1,141. Hao ni wagonjwa walioingia kwenye zile mashine kupata tiba hizo,” amesema Dk Mwaiselage.
Soma zaidi:
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- Wagonjwa wa saratani wahakikishiwa tiba ya kisasa ya mionzi
Amebainisha kuwa katika miaka ya nyuma karibu wagonjwa 208 wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kufanya tiba ya namna hiyo, lakini mashine zimesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa hao na sasa wanatibiwa hapa Tanzania.
Wagonjwa hao wanapokuwa nje nchi huwagharimu kati ya Sh50 milioni hadi Sh75 milioni kwa kila mgonjwa mmoja kupata tiba ya saratani hasa ya mionzi.
“Karibu Sh10.4 bilioni zimeweza kuokolewa kwa kuwa na hizi mashine za kisasa katika taasisi yetu ya Saratani ya Ocean Road,” amesema.
Kwa mujibu wa mwongozo wa taasisi ya Hesperian Health Guides, matibabu ya saratani hutegemea aina ya saratani inayomsumbua mgonjwa. Njia za matibabu zinaweza kuwa tiba kwa njia moja moja au kwa pamoja. Njia nyingine ya matibabu inaweza kutumika kama njia ya kwanza haikufanikiwa vizuri.
Mwongozo huo unaeleza kuwa kuna aina nne za matibabu ya saratani; upasuaji, tibakemikali, tibamionzi na tiba ya homoni ambayo hutumia dawa kusimamisha uzalishaji wa baadhi ya homoni mwilini.