November 24, 2024

Matumizi ya simu za mkononi yazidi kuchangia maendeleo Tanzania

Ripoti ya mapinduzi ya kidijitali imeeleza kuwa simu zimesaidia kuboresha huduma katika sekta ya kilimo, elimu na afya.

  • Ripoti ya mapinduzi ya kidijitali imeeleza kuwa simu zimesaidia kuboresha huduma katika sekta ya kilimo, elimu na afya.
  • Watumiaji wa simu za mkononi wazidi kuongezeka, jambo linalofungua fursa mbalimbali kibiashara na kujiajiri. 

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya utafiti wa mapinduzi ya kidijitali Tanzania ya mwaka 2019, imeeleza kuwa ongezeko la watumiaji wa simu za mkononi na ushindani wa makampuni ya mawasiliano ya simu umesaidia kuboresha huduma zinazotolewa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na kilimo.

Uchambuzi  wa takwimu za robo ya mwisho ya mwaka 2018 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018 kulikuwa na watumiaji 43.6 milioni wa simu za mkononi. 

Ripoti hiyo ya mapinduzi ya kidijitali Tanzania ya taasisi ya  GSMA iliyozinduliwa jana (Machi 18, 2019) jijini Dar es Salaam, inaeleza kuwa teknolojia ya dijitali inaweza ikasaidia kutatua matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii katika jamii ikiwa itapewa msukumo wa aina yake.  

Mchambuzi mkuu kutoka GSMA Kenechi Okeleke ameeleza namna simu imeweza kuwa njia ya kufikia mafanikio na maendeleo ikitumiwa vizuri. Picha| Zahara Tunda.

Imebainisha baadhi ya sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika teknolojia ikiwemo sekta ya afya ambayo kupitia kampeni za Vodafone Moyo, Wazazi Nipendeni na ‘Tigo’s CCBRT Partnership’ ambazo zimesaidia kuboresha afya ya wanawake na watoto. 

Sekta nyingine ni elimu ambapo kampuni ya Airtel Tanzania inaendesha kampeni ya Airtel FURSA inayolenga kuwaongeza vijana ujuzi katika shughuli za ujasiriamali; ‘Tigo e-Schools’ (intaneti mashuleni) na Vodafone Foundation ambayo imejikita kuisaidia jamii kupata fursa za kujifunza.

Sekta ya kilimo nayo haijaachwa nyuma ambapo kampeni ya ‘Tigo Kilimo’ na ‘Linda Mbegu’ zinasaidia kuwapatia wakulima taarifa sahihi za kilimo cha kisasa katika maeneo yao kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno. 


Inayohusiana: Mfumo wa malipo wa QR Code unavyosaidia kupunguza gharama za maisha


“Ripoti inatupa faraja na kuona jinsi gani tumeweza kusaidiana, na inatoa picha halisi tunavyoweza kusaidia jamii,” amesema Mkurugenzi wa mwasiliano Airtel, Beatrice Singano  kwa niaba ya umoja wa mtandao wa makampuni za simu Tanzania (TAMNOA).

Singano amesema kampuni hizo zinaangalia uwezekano wa kutengeneza programu jumishi ambazo zitahusisha watumiaji wote wa huduma za simu bila kujali kama wanafikiwa na intaneti au la, ili kuwafikia watumiaji kulingana na mahitaji yao.