October 8, 2024

Mifumo ya kidijitali kuliimarisha shirika bima Tanzania

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji, amesema hakuna ubadhirifu unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kubadili uongozi wa Shirika hilo pamoja na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji

  • Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeachana na malipo ya hundi badala yake linatumia mfumo wa malipo kielektroniki. 
  • Linatumia mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (e-Office) ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji, amesema hakuna ubadhirifu unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kubadili uongozi wa Shirika hilo pamoja na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji mapato.

Dk Kijaji alikuwa  akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, aliyetaka kujua ukweli kuhusu kuendelea kwa ubadhirifu katika Shirika la NIC na mpango wa Serikali wa kulisaidia shirika hilo kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

Dk Kijaji amesema hivi sasa shirika hilo linatumia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali (GePG) hatua iliyoimarisha mapato yake pamoja na kuanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufanya malipo yake yote badala ya kutumia hundi.

“Shirika la NIC lilianza kutumia Mfumo wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali kuanzia Novemba, 2019 na kuondoa ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu pamoja na kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai ikiwemo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya bima za maisha ili kujiridhisha kuhusu uhalali wake,” amesema Dk Kijaji jana (Aprili 3, 2020).

Serikali imechukua hatua ya kuliimarisha Shirika la NIC kitaalam kwa kuliondoa shirika hilo kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani.

Katika kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Shirika, ufungaji wa mfumo wa usimamizi wa shughuli za kihasibu na malipo katika taasisi za umma (MUSE) uko katika hatua za mwisho na kwamba mfumo huo utakapokamilika utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika.


Soma zaidi: 


Amesema kuwa Serikali inaendelea kupitia upya Mpango Mkakati wa NIC ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani, kuongeza uwekezaji katika mifumo ya Tehama ili kuwafikia wateja wengi zaidi, kuongeza ubora wa huduma na kulipa madai, kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

Pamoja na kufanya mabadiliko ya uongozi wa shirika hilo, amesema wamelipatia shirika hilo wataalam katika nyanja za mifumo ya Tehama na mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (e-Office) ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji

Julai 29, 2019, Rais John Magufuli alimteua Dk Elirehema Doriye kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) akichukua nafasi ya Samwel Kamanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Mabadiliko hayo yalikuja takriban mwezi mmoja tangu Rais Magufuli afanye mabadiliko mengine ya uongozi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).

Juni 25 mwaka huo, alimfuta kazi Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Bhagayo Saqware na kumteua Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Mussa Juma kuchukua nafasi hiyo ya kuiongoza taasisi nyeti katika sekta ya fedha na bima nchini.