October 8, 2024

Namna ya kuepuka matangazo ya mtandaoni kwenye simu yako

Soma maelezo kabla ya kupakua programu kwenye simu yako na pendelea kutumia apps zilizopo kwenye duka la programu za simu linalotambulika.

Ili kuepukana na matangazo hayo ambayo mara kadhaa hukera na kukuchelewesha kufanya baadhi ya vitu, pendelea kutumia app ambazo hazina matangazo na mara zote, zinakuwa hazina alama ya “Ad” wakati wa kuzipakua. Picha|Mtandao.


  • Soma maelezo kabla ya kupakua programu kwenye simu yako.
  • Pendelea kutumia apps zilizopo kwenye duka la programu za simu linalotambulika. 
  • Nunua app kama una uwezo huo ili kuepuka matangazo.

Dar es salaam. Huenda ni mara  nyingi umekuwa ukitumia simu janja yako na matangazo yakajitokeza kusikojulikana na ukabaki na mshangao ni wapi yanatokea.

Ni vema ukafahamu kuwa, matangazo hayo yanakufikia kutokana na roboti kusoma tabia yako ukiwa mtandaoni na hivyo kukuletea matangazo ya bidhaa ama programu ambazo ya vitu unavyopendelea kuperuzi mara kwa mara ukiwa mtandaoni.

Hali hii imenitokea na mimi.Kkwa takriban siku tatu zilizopita, nilikuwa natafuta maduka ya nguo kwenye mtandao wa Instagram. Nilitafuta na kutafuta nikiingia ukurasa baada ya ukurasa. Utafutaji wangu ulikuwa wa ziada kiasi cha kwamba nilinunua bando mara mbili ndani ya siku moja, kitu kisicho cha kawaida kwangu.

Baada ya kupata nilichokuwa nakihitaji, siku zote zilizofuata, matangazo yote yanayolipiwa kwenye mtandao wa Instagram ambayo yananifikia ni yale ya kurasa za wafanyabiashara wa nguo.

Instagram na mitandao ya kijamii ni mada ya siku nyingine. Leo tuzungumzie ni namna gani unaweza kuepuka kupata matangazo pale unapotumia programu tumishi (apps) kama kamera, magemu na zinginezo ama pale ukiwa kwenye mtandao kwa watumiaji wa simu zinazotumia mfumo endeshi wa “Android”.

Umeyaruhusu kwenye programu ya “settings”

Huenda umewahi kupakua app nje ya duka la manunuzi ya programu za simu (Play Store) na ikakulazimu kuruhusu simu yako kuikubali app hiyo licha ya kukupa onyo juu ya madhara yake.

Kuacha kuondoa ruhusa hiyo, kunaupa mtandao uwezo wakukuletea matangazo hata usiyoyahitaji ikiwemo kukupakulia programu za michezo na zinginezo bila ruhusa.

Kuepukana na hili, zima ruhusa hiyo na pendelea kutumia programu zilizopo kwenye duka la Play Store.


Zinazohusiana: 


Epuka kupakua programu zinazohusisha matangazo

Hata play store, kuna apps ambazo zinahusisha matangazo (in app adds) kuzitambua app hizo, utaona alama ya tangazo pembeni (Ad). Hivyo pale utumiapo app hiyo, mara kadhaa unakuwa unapata matangazo ambayo mengine ni sekunde tano na mengine sekunde 10.

Ili kuepukana na matangazo hayo ambayo mara kadhaa hukera na kukuchelewesha kufanya baadhi ya vitu, pendelea kutumia app ambazo hazina matangazo na mara zote, zinakuwa hazina alama ya “Ad” wakati wa kuzipakua.

Lipia apps zako kama una uwezo

Siku hizi kumekuwa na App ambazo zinahitaji uzilipie pale ukitaka umiliki kamili, mfano wake ni app za kamera na zile za kutengenezea maudhui ya video ili kudhibiti matangazo yasikusumbue.

Endelea kusoma www.nukta.co.tz kwa dondoo muhimu zitakazokusaidia kwenye maisha yako ya kila siku.