July 8, 2024

Programu zitakazokuongezea furaha wakati wa mapumziko ya wikiendi

Zinasaidia kupata chakula, usafiri na maeneo ya kutembelea.

  • Programu hizo ni pamoja na Google Maps, AirBnB na Piki.
  • Zinasaidia kupata chakula, usafiri na maeneo ya kutembelea.

Dar es Salaam. Wikiendi ndiyo inaanza leo. Huenda umejipanga kwa ajili ya mapumziko ukiwa nyumbani au kwenda sehemu tulivu kufurahia na wale uwapendao. 

Kama hutaki kuuumiza kichwa uende wapi, utapataje chakula na hata vinywaji. Basi teknolojia inakurahisishia kila kitu katika viganja vyako kupata kile unachohitaji. 

Jaribu kutumia programu hizi wikiendi hii kurahisisha mambo yako hasa kama unapanga kutoka mtoko: 

Google Maps

Ni programu tumishi inayoweza kukusaidia kupata ramani sahihi ya mahali unapotaka kwenda ukiwa kwenye mizunguko yako ya wikiendi. 

Programu hii inaendeshwa na kampuni ya Google inayopakuliwa kwenye simu zilizo na mfumo wa Android pamoja na iOS ili kusaidia urahisi wa kupata eneo unalokwenda hasa kama hujui liko wapi na jinsi ya kufika.

Kwa kutumia, Google Maps, utaweza kufahamu njia na mitaa unayopaswa kupita ili kufika unakokwenda. Lakini pia inakupa machaguo ya migahawa, baa na maeneo tulivu yaliyo karibu na eneo unaloishi.

                  Programu hii inaendeshwa na kampuni ya Google inayopakuliwa kwenye simu zilizo na mfumo wa Android pamoja na iOS. Picha | Mtandao.

AirBnB

Programu hii tumishi ambayo nayo unaweza kuipata kwenye kiganja chako, inakurahisishia kupata hoteli, nyumba za kupanga au kukaa kwa muda mfupi ambazo zina huduma zote muhimu za nyumbani. 

Kama umechoshwa na mazingira ya nyumbani kwako, AirBnB inakupa orodha ndefu ya nyumba au hoteli kwa gharama tofauti kulingana na mahitaji yako. 

Nyumba hizo zenye usalama na utulivu, zinaweza kukuondolea msongo wa mawazo na kukuwezesha kuiona dunia kwa namna ya tofauti. 

Otapp

Huenda ukawa mpenzi wa kutembelea kumbi za sinema kama Century Cinemax zilizopo maeneo mbalimbali jijini, wakati wa wikiendi kwa kuangalia sinema mbalimbali zilizotoka.

 Programu tumishi ni nzuri kwaajili ya kufanya manunuzi ya tiketi za kuangalia movie katika kumbi mbalimbali za sinema nchini. 

Ikiwa na faida ya kukutunzia tiketi na kupata nafasi pale unapokuwa umebanwa na mambo mengi kabla ya kwenda kwenye kumbi maalum kulipia mlangoni.

Lakini kama utaamua kukaa nyumbani ili kupunguza gharama za mtoko, unaweza kutumia programu tumishi ikiwemo ya Piki na Yamee kuagiza chakula ukipendacho. 

Hii itakuwasaidia kula chakula ambacho kimepikwa na mtu mwingine, wakati huo ukisoma vitabu au kuangalia filamu na mambo mengine unayofikiri yatakamilisha wikiendi yako. 


Zinazohusiana:


Tovuti 

Tovuti ni teknolojia nyingine inayoweza kukusaidia kutafuta na kujifunza mambo mbalimbali  uwapo katika mapumziko ya mwisho wa wiki kwa lengo la kugundua mambo mapya na kujifunza vitu vinavyoweza kukuvusha kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Unaweza kutumia tovuti za mambo mbalimbali unayopendelea kama Travel & Leisure, world reader, many books na nyingine nyingi zinazoweza kukuongezea maarifa juu ya mambo mengi unayopenda kusomea.