Sababu za Twitter kusitisha matangazo ya kisiasa Novemba 22
Maamuzi hayo yamefikiwa ili kupunguza vurugu na usambazaji wa taarifa zisizo za ukweli katika mtandao huo.
- Itasitisha matangazo yanayohusu siasa kuanzia Novemba 22.
- Maamuzi hayo yamefikiwa ili kupunguza vurugu na usambazaji wa taarifa zisizo za ukweli katika mtandao huo.
- Wadau wa siasa, mitandao ya kijamii watoa maoni mchanganyiko.
Twitter inakusudia kuondoa na kutoruhusu tena matangazo ya kisiasa katika mtandao wake huku ikitoa sababu mbalimbali za uamuzi huo ikiwemo kuwaongezea wapiga kura uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka.
Uamuzi huo utaanza kutekeleza rasmi Novemba 22, 2019 ambapo sheria na taratibu zitakazoongoza utaratibu wa kuondoa matangazo hayo zitatolewa kuanzia Novemba 15.
Hata hivyo, marufuku hiyo haitahusu taasisi na watu wanaowajulisha wapiga kura juu ya taratibu za kufuata wakati wa zoezi la kujiandikisha au kupiga kura katika chaguzi mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Jack Dorsey ametoa tamko hilo jana (Oktoba 30, 2019) kwenye ukurasa wake wa Twitter na kueleza sababu nyingine ambazo zimewafanya wafikie uamuzi huo ambao umeibua mjadala kwa watu wengi mtandaoni.
“Tumeamua kusitisha matangazo yote yanayohusu siasa kwenye mtandao wa Twitter ulimwenguni. Siasa ni za kufikiwa na sio kununuliwa”, amesema Dorsey.
Dorsey amesema wamefanya tathmini ya vurugu na wingi wa taarifa zisizokuwa za kweli katika mitandao huo hasa wakati wa uchaguzi na kuona kuna kila sababu ya kusitisha matangazo hayo licha ya kuwa yanaingiza fedha nyingi.
Amezitaja sababu nyingine kuwa ni haki waliyonayo watazamaji katika kupenda na kusambaza matangazo hayo na siyo kununua kwa asilimia kubwa.
- Twitter kuwawekea watumiaji wake muonekano mpya
- Facebook kuzuia matangazo ya ‘uponyaji wa miujiza’ mtandaoni
- Maboresho: Kupitia Twitter utatazama video mubashara
Huenda, maamuzi haya yatasaidia kuwepo kwa utulivu katika mtandao huo na kuepukana na vurugu zozote zinazoweza kujitokeza katika mitandao hiyo ya kijamii inayotumika na watu wengi.
Twitter wamechukua hatua hiyo wakifuata nyayo za Facebook walionza kusitisha matangazo ya kisiasa kwenye mtandao wao.
Mwanzilishi wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg ametetea sera ya kampuni yake kwamba, “kwenye demokrasia, sio sawa kwa makampuni binafsi kuratibu siasa au habari zihusuzo siasa.”
Mara baada ya Twitter kutangaza uamuzi huo, watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa wameelezea hisia zao kuhusu uamuzi huo na jinsi utakavyoathiri mwenendo wa siasa duniani.
Meneja kampeni wa Rais wa Marekani, Donald Trump amesema uamuzi huo ni moja ya hatua za kumnyamazisha Trump pamoja na wafuasi wake wa chama cha Republican.