October 6, 2024

Sababu zinazowazuia wanawake kujikita kwenye fani ya teknolojia

Ni pamoja na kukosa motisha wanapokuwa shuleni na kutokutambulishwa katika ulimwengu wa teknolojia wakiwa watoto.

  • Ni pamoja na kukosa motisha wanapokuwa shuleni na kutokutambulishwa katika ulimwengu wa teknolojia wakiwa watoto.
  • Sababu nyingine ni sekta ya teknolojia kuwa na wanaume wengi, jambo linalosababisha wanawake kuonekana kama wasindikizaji.
  • Wadau wa teknolojia wamesema kwa sasa wanawake wanaamka lakini bado motisha inahitajika hasa kwa vijana.

Dar es Salaam. Inawezekana ikawa ni ndoto ya wazazi wengi kwa sasa kumuona binti wa kike akifanya vyema katika masomo na hata kufikia ngazi za juu ya elimu katika taaluma yake. 

Wazazi hupenda kusikia “Mhandisi, daktari, mtakwimu” na majina mengine baada ya watoto wao wa kike kumaliza shule. 

Hata hivyo, maono ya wazazi wakati mwingine hayatimii kwa sababu wasichana hushindwa kusomea masomo ya sayansi yanayoweza kufungua fursa ya kubobea katika fani ya sayansi na teknolojia.

Jamii na wadau wanatamani kuona wasichana wa Tanzania wanaonekana katika shughuli mbalimbali za teknolojia, lakini ziko sababu mbalimbali zinazowazuia kuingia huko. 

Wadau wa sayansi na teknolojia wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa zipo sababu mbalimbali zinazoanzia utotoni na hadi ukubwani na kuwafanya wanawake washindwe kujihusisha na masuala ya teknolojia ikiwemo ubaguzi wa kijinsia na hukumu wanayopata pale wanapoomba kazi hizo.

Kwa baadhi ya wadau, mtazamo wao ni kuwa wanawake wanafikiri kujihusisha na masuala ya teknolojia ni hadi uyasomee chuoni, jambo ambalo siyo la kweli.

Mwandishi wa habari za teknolojia wa kujitegemea, Zahara Tunda amesema hakuwahi kusomea uandishi wa habari za teknolojia lakini alijifunza wakati akiwa kazini. 

“Bado wabunifu wanawake hawajajikita zaidi kutafuta mbinu mbadala za matumizi ya technolojia kama wanaume na ndiyo maana unaona wachache au hawapo,” amesema Tunda ambaye ameshauri wanawake kujitambua katika kazi zao na kuona umuhimu wa matumizi ya technolojia kurahisisha kazi au shughuli zao za kila siku.

Masomo  ya sayansi huchukua muda mrefu kuyasoma na kwa baadhi ya wasichana, safari ya matumaini hupotea baada ya kuufikiria muda huo. Picha| freepik.com

Huenda wanawake wengi kushindwa kujihusisha na shughuli za sayansi na teknolojia ni jambo ambalo mizizi yake imeanzia utotoni ambapo wanakosa msingi mzuri kuwawezesha kubobea katika masomo ya sayansi. 

Mtaalamu wa Programu za kompyuta kutoka kampuni ya Code for Africa, Khadija Mahanga amesema endapo angelikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili, angelipenda kukutana na mhandisi ili aongee naye na amshauri juu ya kazi hiyo.

Mahanga amesema kutokuwepo kwa motisha kwa wanafunzi kutoka kwa wanawake ambao wapo katika taaluma za sayansi na teknolojia ni moja wapo ya sababu zinazowafanya wasichana kuona kama masomo ya teknolojia kuwa ni ya wanaume tu.

“Siku hizi kidogo naona wapo watu ambao wanafanya programu za motisha mashuleni. Itasaidia wanafunzi kuona kuwa inawezekana mwanamke kusoma na kufaulu na hata kufikia ngazi za juu za taaluma zinazodhaniwa kuwa ni za wanaume tu,” amesema Mahanga ambaye amesisitiza uwepo wa fursa nyingi za teknolojia zinazowasubiri wanawake.

Kukosa motisha ni kikwazo pia

Kwa upande mwingine, Masomo ya sayansi huhitaji bidii kuyasoma na wengi walioyachukua wanasema hayahitaji lelemama. Yanahitaji kujitoa ikiwa ni pamoja na kuahirisha baadhi ya vitu ikiwemo michezo na shughuli zingine mbali na masomo.

Daktari kutoka Muhimbili, Theresia Venance, amesema muda ambao huchukua kusoma masomo ya sayansi na teknolojia huwafanya wengi wayakatie tamaa. 

Mbali na ukweli wa kwamba masomo hayo yanahitaji bidii na juhudi tangu ukiwa kidato cha kwanza, yatahitaji uendelee kujifunza kila siku ya maisha yako.

Daktari huyo amesema ni wazi kuwa teknolojia inabadilika kila siku hivyo utahitaji kujisasisha na wasichana wengi ni aidha hawako tayari kwa hilo ama hawana motisha ya kufanya hivyo.

“Udaktari huhitaji miaka mitano na bado haujawa mbobezi, uhandisi ni mitano au zaidi, kwa msichana hapo anawaza muda wa kuanzisha familia na mengineyo hivyo wanaona ni bora wachukue masomo ya muda mfupi,” amesema Dk Venance ambaye alisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Bayolojia (PCB).


Soma zaidi:


Wakati mwingine nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi za teknolojia, huwa kikwazo kwa wanawake kujipenyeza kwa sababu wanaona siyo sehemu sahihi kwao 

Mwanafunzi wa Shahada ya uzamili ya sayansi ya takwimu kutoka Chuo cha Teknolojia cha Georgia nchini Marekani Neema Kafwimi katika mahojiano yake na Nukta Habari amesema uwepo wa wanaume wengi katika tasnia ya teknolojia ni sababu ya wanawake kukata tamaa katika kazi hizo.

Mtakwimu huyo mtarajiwa ameweka wazi kuwa wanawake hushindwa kujisikia vyema pale anapokuwa amezungukwa na wanaume wengi katika maeneo ya kazi na hilo husababisha hata waliokuwa na moyo wa kazi hizo kushindwa kuendelea.

“Wanawake wengine hawapati fursa kwa sababu wanaume wengi wapo katika sekta ya teknolojia. Hata mwanamke anapotuma maombi, baadhi hushindwa kuwakubalia wakiwa na mawazo hasi juu ya utayari wao,” amesema Kafwimi.

Binti huyo amesema uwepo wa dhana potofu ikiwemo kuwa na majukumu ya kifamilia huwafanya wanaume kushindwa kuwapa nafasi wanawake.

“Muda mwingine kazi za teknolojia huhitaji kufaya kazi kwa saa nyingi, kwa msichana anayeishi nyumbani au mwenye familia, huenda asifae kwa kazi hizo,” Kafwimi ameeleza hayo akisisitiza kuwa hizo ni nadharia potofu miongoni mwa wanaume wenye nguvu ya kuajiri. 

Kwa upande wake Mwanzilishi wa kampuni ya Work Nasi, Edgar Mwampinge amesema mifumo mingi ambayo inasaidia programu mbalimbali za teknolojia inasimamiwa na wanaume jambo ambalo linawafanya wanawake kujihisi ni wasindikizaji.

Kuondoa hilo Mwampinge amesema jambo la muhimu kuzingatia ni wanawake kujiamini na kuamini uwezo wao kwani hakuna mtu asiyeona kitu kama ni kizuri na kinatatua changamoto za jamii kama yalivyo malengo ya teknolojia.

Watoto wa kikehupewa midoli ya kuchezea utotoni huku wakiume wakipewa magemu na maroboti kuchezea. Hilo huathiri matamanio ya mtoto huyo hata masomoni. Picha| freepik.com

Ni tatizo la dunia

Wanawake kutokujihusisha na masuala ya teknolojia sio tatizo lililopo Tanzania pekee bali ni  mada inayozungumziwa ulimwenguni kote.

Changamoto ni kutokuwepo kwa usawa maeneo ya kazi hasa za kiteknolojia na hata kutokuwepo kwa usimamizi sawa kutoka kwa wazazi.

Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii ya wanawake wanaojihusisha na masuala ya ujuzi na ubunifu wa programu na teknolojia ya mawasiliano (ICT) Code Lady, Rafia Ramadhan amesema watoto wa kike tangu utotoni hawapewi vitu vinavyohusiana na masuala ya teknolojia ikiwemo midoli ya kuchezea. 

Mara nyingi huhusishwa na kupika, malezi na kadhalika.

“Mtoto wa kiume hupewa gemu la video za magari, maroboti na mengineyo ambayo humtambulisha katika ulimwengu wa teknolojia wakati mtoto wa kike anatambulishwa katika ulimwengu tofauti,” amesema Ramadhan.

Jambo hilo humsababisha mtoto wa kiume kuwa na moyo wa kuendelea na masomo ya sayansi hata anapoingia shuleni kwani siyo ulimwengu mpya kwake.

Ramadhan amesema ni wakati wa mazungumzo katika jamii ili kuchochea mabadiliko kwenye jamii na kuondoa ubaguzi wa kijinsia sehemu za kazi na jamii kukubali kuwa msichana anaweza kujihusisha na teknolojia.

Jambo hilo litawasaidia wanawake kukabiliana na changamoto zinazowahusu ambazo wanaume hawawezi kuzielewa.