November 24, 2024

Sanaa inavyobadili fikra potofu dhidi ya ubunifu Tanzania

Wadau wamesema ubunifu ni zaidi ya kazi za teknolojia lakini ni namna ya kufikiria ili kupelekea matokeo mazuri kwenye jamii kwa gharama nafuu.

  • Ubunifu ni dhana mtambuka inayogusa maeneo yote ikiwemo sanaa inayotumika katika shughuli za burudani na utamaduni. 
  • Wadau wamesema ubunifu ni zaidi ya kazi za teknolojia lakini ni namna ya kufikiria ili kupelekea matokeo mazuri kwenye jamii kwa gharama nafuu.

Dar es Salaam. Mshangao ulitawala uso wake baada tu ya kuambiwa kwamba wasanii chipukizi wa maigizo na muziki wameungana kuandaa igizo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki Ya Ubunifu 2019.   

Huyo ni Scola Joseph mkazi wa Magomeni Jijini Dar es Salaam ambaye alifikiri ubunifu umetawaliwa na vijana wanaoibukia katika teknolojia kuonyesha mitambo, mashine na hata mifumo mbalimbali ambayo wameigundua kwa lengo la kusaidia jamii.

“Mimi sikutarajia kama wiki ya ubunifu ingehusisha sanaa lakini kwa igizo nililoliona, nimeachwa na bumbuwazi kwani limenigusa kwa namna ya pekee,” amesema Scola ambaye ni alihudhuria igizo fupi la usawa wa kijinsia lililofanyika Little Theatre Oysterbay jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Wiki ya Ubunifu kwa mwaka huu inafanyika 25-30 Machi, 2019 katika jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ambapo ni jukwaa maalum linakalowakutanisha wabunifu kuonyesha kazi zao na kutambuliwa rasmi kutokana na mchango wao kwenye jamii. 

Tukio hilo limeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Costech.

Huenda Scola hayuko peke yake katika fikra za kuamini ubunifu unagusa sekta ya teknolojia na sayansi tu, wako watu wengi ambao wana fikra kama hizo lakini ni dhana mtambuka inayogusa sekta mbalimbali za utendaji na uzalishaji.

Baadhi ya wasanii walioshiriki katika igizo fupi la usawa wa kijinsia lililofanyika Little Theatre Oysterbay jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha| Unleashed academy.

Makamu Kiongozi Mkuu wa HDIF, Joseph Evarist amesema ubunifu huja kwa namna nyingi na sanaa nayo inahitaji nguvu ya ubunifu ndani yake ambapo teknolojia, mashine na mengineyo ni magurudumu tu huku ubunifu ni namna ya kufikiria ili kupelekea matokeo mazuri kwa gharama nafuu.

“Sanaa ni dhana yenye nguvu katika mawasiliano na inaweza kutumika kupata jumbe zenye umuhimu kwa watu kwa namna ya kufurahisha na yenye ubunifu,” amesema Evarist.


Soma zaidi:


Igizo nalo lilikuwa la aina yake

Akizungumzia igizo hilo, Mkurugenzi wa kampuni inayojihusisha na maendeleo ya vijana ya Unleashed Africa, Khalila Mbowe (Kellz) ambaye pia ni muigizaji mkuu kwenye igizo la usawa wa jinsia amesema lengo la igizo hilo ni kuhamasisha sanaa kuwa na mchango katika maendeleo ya jamii hasa katika masuala mtambuka.

Amesema anapenda kuona sanaa yake inatumika katika maendeleo ya jamii hasa kuwa msaada kwa wanawake kwani swala zima la kukosekana usawa wa jinsia linaathiri maisha ya watu wote.

“Kwanini viungo vyangu vilivyompendeza Mungu vinifanye duni kuliko wewe? Kama wanawake wanashindwa kufanya kazi kuna uwezekano maendeleo yakawa yataratibu ama yakakosekana kabisa,” amesema Kellz katika  igizo lake.

Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kazi za sanaa na ubunifu ili kuwapa fursa ya kutoa mchango wao katika shughuli za maendeleo. Picha|Unleashed academy.

Naye Evarist amesema wanawake na wasichana wanatengeneza asilimia 51 ya watanzania hivyo hakuna njia yoyote ya kuleta maendeleo itakayofanikiwa na kuleta matokeo makubwa bila kuwahusisha.

“Hakuna njia yeyote ya maendeleo itakayokuwa na maana bila kuwahusisha kuanzia kwenye utengenezaji hadi ufanikishaji. Haiwezi kutokea kama wanawake wanaendelea kuonekana kama wananchi daraja la pili na ndio maana mazungumzo ya usawa lazima wahusike,” amesema.

Wadau wengine waliohudhuria katika Wiki ya Ubunifu, wamesema wasanii waende mbali zaidi na kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ajira na haki za watoto katika kazi zao za sanaa ili kuifikia jamii kulingana na mahitaji yake. 

“Wengi tunasahau juu ya suala zima la wafanyakazi wa ndani, kuna uhitaji sanaa itazame pia huko,” amesema Tulanana Bohela, Muandaaji wa vipindi vya kidijitali kutoka taasisi ya Ona Stories.