Serikali mbioni kuipatia hospitali ya Mwananyamala mashine ya CT-Scan
Mashine hiyo itaongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaofuata huduma hiyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
- Mashine hiyo itaongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaofuata huduma hiyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
- Hospitali zote za rufaa za mikoa kupata mashine za CT-Scan.
- Wizara ya afya kugawa upya wafanyakazi kulingana na mahitaji ya hospitali nchini.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wizara yake inakusudia kufunga mashine mpya ya CT-SCAN katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala ili kuiongezea ufanisi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaofuata huduma hiyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Waziri Ummy amezungumza hayo bungeni leo (Mei 21, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Said Mtulia aliyetaka kujua ni lini Serikali itanunua mashine za CT-Scan na MRI (Magnetic resonance imaging) kwa ajili ya hospitali ya Mwananyamala ili kupunguza msongamano katika hospitali ya Muhimbili na kuongeza ufanisi katika hospitali hiyo.
“Kutokana na mabadiliko hayo, Serikali inakusudia kufunga mashine ya CT-Scan katika hospitali ya mkoa ya Mwananyamala ambapo utekelezaji wake umeshaanza,” amesema Ummy.
Amesema kusudio hilo la Serikali linatokana na mabadiliko yaliyofanyika katika mwongozo wa kutengeneza vifaa vya radiolojia nchini (Standard medical radiology and equipment guidelines) mwaka 2018 ambapo awali huduma za CT-Scan na MRI hazikuwepo katika hospitali za rufaa za mikoa.
Waziri huyo amesema mabadiliko hayo yalisukumwa na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hizo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mashine hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa kupima magonjwa mbalimbali katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala. Picha|Mtandao.
Kwa sasa huduma za za CT-Scan zitakuwa zinapatikana katika hospitali za rufaa za mikoa huku huduma za MRI zitakuwa zinapatikana katika hospitali za rufaa za kanda na Taifa.
Kufungwa kwa mashine ya CT-Scan katika hospitali hiyo kutasaidia kuongeza ufanisi wa kuwahudumia wagonjwa na kupunguza msongamano katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo imekuwa ikipata wagonjwa wengi wanaohitaji huduma hiyo.
Inayohusiana: Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amesema wizara yake inafanya mchanganuo wa watumishi wa afya katika hospitali za rufaa za mikoa, wilaya, zahanati na vituo vya afya ili watumishi hao waweze kugawanywa upya kulingana na mahitaji ya hospitali husika.
Mgawanyo huo utaisaidia hospitali ya rufaa ya Mwananyamala ambayo inahudumia wagonjwa wengi kwa mwaka ukilinganisha na hospitali nyingine nchini, jambo linaloleta changamoto kwa madaktari na wahudumu kutoa huduma bora za afya.
“Hata ukiangalia takwimu za wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali zetu za rufaa za mikoa 28, Mwananyamala inaona wagonjwa kwa mwaka takriban 300,000 ukilinganisha na Mount Meru inaona wagonjwa 24,000 kwa mwaka, Manyara 27,000,” amesema Ummy.
Kwa takwimu hizo za Waziri Ummy, Mwananyamala inabeba wagonjwa wengi mara 10 zaidi ya wale wanaoonwa katika Hospitali ya Mount Meru ya mkoani Arusha.