November 24, 2024

Serikali yaokoa zaidi ya Sh700 bilioni ikiachana na umeme wa mafuta

Dk Magufuli amesema kwa sasa Tanzania inawekeza katika uzalishaji wa umeme wa maji ambapo inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo mradi mkubwa wa bwawa la Julius Nyerere katika bonde la Mto Rufiji.

  • Fedha hizo zimeokolewa baada ya kuzimwa kwa mitambo iliyotumia mafuta kuzalisha umeme.
  • Mitambo iliyozimwa ni ya IPTL, Aggreko na Symbion. 
  • Rais magufuli amesema kuokolewa kwa fedha hizo kumesaidia Tanesco kujiendesha.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali imeokoa kiasi cha Sh719 bilioni baada ya kuzima mitambo inayotumia mafuta ya dizeli kuzalisha umeme nchini Tanzania ikiwemoya kampuni ya Symbion. 

Dk Magufuli amesema kiasi hicho kilichookolewa kimelipatia Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco) uwezo wa kujiendesha lenyewe.

“Tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kuzima mitambo ya kuzalisha umeme ya mafuta. Kwa mfano, kwa kuzima mitambo ya IPTL (Independent Power Tanzania Limited), Aggreko na Symbion, tumeokoa Sh719 bilioni kwa mwaka,” amesema Dk Magufuli wakati akifunga Bunge la 11 jijini Dodoma leo (Juni 16, 2020). 

Dk Magufuli amesema kwa sasa Tanzania inawekeza katika uzalishaji wa umeme wa maji ambapo inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo mradi mkubwa wa  bwawa la Julius Nyerere katika  bonde la Mto Rufiji.

“Tumeanza kutekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere kwenye bonde la Mto rufiji. Mradi huu ulipigwa vita sana. Lakini tumefanikiwa na gharama ya mradi huu ni Sh6.5 trilioni na fedha zote zinatolewa na Watanzania,” amesema Magufuli.


Zinazohusiana:


Magufuli amesema mradi huo utakapokamilika utazallisha megawati 2, 115 ambazo zitasaidia kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi mabaya ya kuni na mkaa.

Aidha, amesema Serikali imefanikiwa kuongeza idadi ya vijiji vilivyofikishiwa umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwezi Aprili 2020 na kubakiza vijiji 3,153. 

Kuvunjwa kwa Bunge la Tanzania leo kunahitimisha safari ya miaka mitano ya Wabunge kutumika wananchi kupitia muhimili huo tangu Dk magufuli alipozindua Novemba 20, 2015. 

Wabunge watakuwa na kibarua kigumu kurudi katika vyama vyao ili kupata ridhaa ya kupitishwa ili kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.