October 6, 2024

Startups 12 za Tanzania kuchuana shindano la dunia la Seedstars

Nne zinatoka Visiwani Zanzibar, nane za Tanzania bara. Mshindi atapata fursa ya kushindania mtaji wa Dola za Marekani milioni 1 (Sh2.3 bilioni) na tuzo zingine za uwekezaji.

  • Nne zinatoka Visiwani Zanzibar, nane za Tanzania bara.
  • Zitawasilisha kazi zao mbele ya majaji na mshindi wa kwanza atapata fursa ya kushiriki mkutano wa Seedstars nchini Uswisi. 
  • Pia itapata nafasi kushindania mtaji wa Dola za Marekani milioni 1 (Sh2.3 bilioni) na tuzo zingine za uwekezaji.

Dar es Salaam. Kampuni 14 changa (startups) za Tanzania, kesho zinatarajia kuchuana ili kupata nafasi ya kushiriki katika shindano la dunia la Seedstars litakalofanyika nchini Uswisi ili kupata nafasi kujishindia mtaji wa Dola za Marekani 500,000 (takribani Sh1.1 bilioni) na tuzo zingine za uwekezaji. 

Shindano hilo linalofanyika kila mwaka ni mahususi kwa startups zinazotatua changamoto za jamii kwa kutumia teknolojia katika kutoa huduma na bidhaa. 

Kati ya kampuni hizo, nne zinatoka Visiwani Zanzibar, nane za Tanzania bara ambapo kesho (Agosti 23, 2019) zitawasilisha kazi zao mbele ya majaji katika ofisi za Seedspace Dar es Salaam ambayo ni tawi la kampuni mama ya Seedstars World ambapo mshindi wa kwanza atatangazwa. 

Startups za Zanzibar zilizopenya katika fainali hiyo ni Zanzibar Health Innovation, Nyumbani Care, Drone Wings na Zanzibit.

Kwa upande wa Tanzania bara, startups nane za Mtabe App, MyHI, Sheria Kiganjani, Kilimo Fresh Foods na Noobites zimefanikiwa kuingia katika fainali hiyo. Nyingine ni Nuru, EX-Africa Tanzania, na MITZ Innovations. 


Soma zaidi:


Mshindi wa Tanzania atapata fursa ya kushiriki mkutano wa Seedstars wa Afrika na ule wa dunia utakaofanyika Uswisi ambapo mshindi wa dunia atapata mtaji wa Dola za Marekani 500,000 (takribani Sh1.1 bilioni) na tuzo zingine za uwekezaji.

Hii ni mara ya tano kwa kampuni ya Seedstars kuandaa shindano hilo Tanzania likilenga kampuni changa ambazo zimekua mstari mbele kutumia teknolojia katika shughuli zao.

“Tumefurahi sana kurudi tena Dar es salaam kwa mara ya tano! Tunajua kuna kampuni nchini Tanzania zinazoendeleza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu. Tunatafuta bora zaidi na tutakwenda naye Uswisi 2019,” amesema Meneja Kanda ya Afrika wa Seesstars, Claudia Makadristo.

Mwaka uliopita wa 2018, Tanzania iliwakilishwa na App ya NALA Money; inayomuwezesha mtu  kufanya miamala yote akiwa popote bila kusubiri muunganiko wa mtandao wa intaneti au kupanga foleni benki na kwenye vibanda vya kutolea pesa.

Shindano hilo limekuwa likiratibiwa kwa ushirikiano wa jopo la watalaam kutoka Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania.