October 7, 2024

Tabia zinazoangamiza betri la kompyuta yako

Ni pamoja na kutumia kompyuta kitandani, kwenye makochi na sehemu zingine zinazotunza joto.

  • Ni pamoja na kutumia kompyuta kitandani, kwenye makochi na sehemu zingine zinazotunza joto.
  • Pia kuiacha kompyuta kuishia chaji kabisa.
  • Utunzaji wa betri la kompyuta utakuepushia gharama zisizo za lazima.

Dar es Salaam. Wahenga walisema hakuna kinachodumu milele lakini kitu huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kina matunzo. 

Matunzo hayo huanzia jinsi unavyobeba kitu, unavyokisafisha na hata kukipatia muda wa kupumzika. Matunzo hayo yanaweza kuwa ya simu, kompyuta na hata bidhaa zingine zinazoendana na hizo.

Kama wewe ni mtumiaji wa kompyuta, huenda umewahi kusikia kuharibika kwa betri la kompyuta mpakato (laptop) lakini hufahamu kiini chake.

Hizi ni baadhi ya tabia zinazochochea uharibifu wa betri ya kompyuta yako kwa haraka bila wewe kufahamu:

Matunzo yako yana mchango gani katika maisha ya betri?

Wapo watu wanaotumia laptop wakiwa kitandani, kwenye makochi na sehemu zingine zinazotunza joto.

Kwa mujibu wa Mtaalamu wa masuala ya masoko na teknolojia kutoka kampuni ya Bigkom Marketing, Charles Peter, wadau wanaotumia kompyuta zao katika mazingira kama hayo husababisha kompyuta zao kuchemka na hivyo “kuua betri” 

Mdau huyo ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, ili kuepukana na shida hiyo, tumia kompyuta yako mezani na epuka kuiziba na vitu pembeni au sehemu ambazo feni za ya kompyuta yako ipo.

Ukiwa makini na matunzo ya kompyuta yako, itakuepushia gharama sa kununua betri mpya na hata kompyuta mpya kwa ujumla. Picha| Supima Techologies.

Zuia kompyuta yako kuishiwa chaji kabisa

Wapo watu wanaodhani kutumia kompyuta zao hadi pale zinapomaliza chaji ndiyo wazichaji tena ndiyo matumizi mazuri ya kompyuta lakini haipo hivyo.

Tovuti ya dondoo za teknolojia ya lifehacker inabainisha kuwa, betri zimetengenezwa zikiwa na kikomo cha mara ngapi zinatakiwa kuchajiwa baada ya kuishiwa chaji. 

Hivyo ni kusema, kadri unaposubiri betri lako liishe chaji ndiyo ichaji, ndivyo unavyopunguza maisha ya betri lako.

Unashauriwa endapo unatumia kompyuta yako mbali na chanzo cha umeme, pale inapokupatia onyo la kuishiwa chaji, hifadhi kazi zako na kisha izime hadi utakapopata sehemu ya kuchajia kompyuta yako.


Soma zaidi:


Kama hatumii kompyuta yako izime

“Hybernating” ni kitendo cha kuigandisha kompyuta yako kipindi ambapo hauitumii au inapokuashiria kuwa inakaribia kuishiwa moto na upo mbali na chanzo cha umeme na hautaki kupoteza kazi zako. 

Unapo “hybernate”, komopyuta yako inazima lakini itakumbuka shughuli zako pindi utakapoiwasha.

Baadhi ya watu huwa na tabia ya kuifunika kompyuta na kisha kuiweka kwenye begi baada ya matumizi na kisha hufunga safari kuelekea wanakokujua wao.

Wengine hubonyeza kitufe cha kuzimia kompyuta kuiweka mashine hiyo katika hali ya “sleep” na kisha kuifunga jambo ambalo huifanya kompyuta iendelee kufanya kazi hata kama haitumiki.

Hii ni miongoni mwa tabia zinazochangia kuua betri la kompyuta taratibu bila kujua. Kama huwezi kuhybernate ni vema uzime kabisa kompyuta yako.

Endapo ukiepukana na tabia hizo, betri ya kompyuta yako ikaendelea kuwa nguvu kwa muda mrefu ili kukuepushia gharama au kuwa na betri ambayo ina tabia ya pasi yaani inafanya kazi pale inapochomekwa kwenye umeme tu.