October 6, 2024

Tanzania ivute subira matumizi ya teknolojia ya utambuzi uso kwa binadamu

Kampuni ya teknolojia ta Microsoft imekataa kuuza teknolojia ya utambuzi wa uso kwa kampuni ya kisheria pamoja na nchi ambazo zote hazikutambulika kwa majina

  • Maoni hayo yametolewa baada ya kampuni ya mirosoft kukataa kuuza teknolijia hiyo kwa kampuni ya kisheria ya jijini California ya Marekani kwa kuhofia usalama wa watu hasa wanawake na watoto. 
  • Wamesema kwa sasa Tanzania haina changamoto za kubwa za usalama ukilinganisha na nchi zilizoendelea kama China na Marekani. 

Dar es Salaam. Kufuatia kampuni ya teknolojia ya Microsoft kukataa kuuza teknolojia ya utambuzi wa uso “facial recognition” kwa kampuni ya kisheria ya jijini California na nchi ambazo hazikutambuliwa kwa majina, baadhi  ya watalaam wa tehama wamesema hawaoni haja kwa teknolojia hiyo kuanza kutumika Tanzania. 

Teknolojia ya utambuzi wa uso wa binadamu hutumika zaidi katika kulinda usalama hasa katika maeneo ya mikasanyiko ya watu na ofisi kwa kuskani sehemu ya mbele ya uso ili kupata taarifa muhimu za muhusika. 

Microsoft ilifikia uamuzi huo ili kulinda haki za binadamu na matumizi mabaya ya teknolojia hiyo ambayo yanaweza yakasababisha kuwaweka hatiani raia wema hasa akina mama na watoto.

Rais wa kampuni ya Microsoft, Brad Smith wakati akizungumza katika mkutano wa uliofanyika jana (Aprili 17,2019) katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani amesema kampuni hiyo ya kisheria ilitaka kufunga teknolojia hiyo kwenye magari ya maofisa wa polisi ikiambatanisha teknolojia ya kuskani mwili ambayo ingetumika kuskani mtu yeyote ambaye angesimamishwa na askari hao wanaotumia teknolojia hiyo.

Smith ameeleza kuwa kwasababu intelijensia ya teknolojia hiyo imefanyiwa majaribio zaidi kwa watu weupe (wazungu), inaweza ikaleta tafrani kwa baadhi ya makundi ya watu wakiwemo  wanawake na watoto.

Pia, Microsoft yenye makao yake makuu nchini Marekani imekataa kuweka teknolojia hiyo kwenye kamera za mji mkuu wa nchi hiyo ambayo haikutajwa baada ya shirika la masuala ya uhuru wa kujieleza la Freedom House  kusema nchi hiyo haina uhuru thabiti.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, Smith amenukuliwa na Wanahabari katika mkutano huo akisema ilikua rahisi kwa Microsoft kuuza teknolojia hiyo kwa gereza la Marekani kwani haitaleta shida kwa watu ambao hawahusiki na eneo la magereza na teknolojia hiyo itatumika kwa watu wa eneo la magereza pekee.

Amebainisha kuwa tayari wameiomba Serikali ya Marekani kuwapa kibali kwa ajili ya majaribio ya teknolojia hiyo kwa watu wote ili kuepusha ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kuyaomba makampuni yote yanayotumia teknolojia hiyo kuitumia kwa makini.

Teknolojia ya utambuzi wa sura inasaidia kupata taarifa za muhusika ambazo zinaweza kutumika katika masuala ya usalama. Picha|Mtandao.

Ni wakati muafaka kwa Tanzania kutumia teknolojia hiyo?

Mtaalam wa programu za kompyuta, Emmanuel Evance  amesema haoni kama Tanzania inahitaji teknolojia hiyo kwasababu inaweza kusababisha taarifa za watu kuzagaa katika maeneo mbalimbali hata kuingia katika mikono isiyo salama.  

Amesema teknolojia hiyo ni nzuri kwa nchi zilizoendelea ambazo zinakabiliwa na tishio la usalama kutokana na muingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi za kiuchumi.

“Teknolojia ya kutambua uso ni nzuri kwa nchi kama China ambayo ina maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia na ina watu wengi hivyo huenda wakahitaji kwaajili ya masuala ya kiusalama. Kwa Tanzania teknolojia hii bado haihitajiki,” amesema Evance.

Evance ambaye amewahi kufanya kazi na kampuni inayowaunganisha wananchi na teknolojia ya Code for Africa amesema taasisi zilizopo nchini ikiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Tume ya Uchaguzi (Nec) ambazo zinatunza taarifa za watu hasa picha, saini na alama za vidole zinatosha katika utambuzi wa watu.