November 24, 2024

Teknolojia sasa kutumika utunzaji wa mazingira Tanzania

Teknolojia hiyo inatarajiwa kuondoa changamoto za kimazingira zainazosababishwa na shhughuli za binadamu.

  • Ni kupitia miradi ya mazingira ambayo inatarajiwa kuanzishwa nchini.
  • Miradi hiyo inategemewa kupunguza ukataji wa miti na kuboresha ardhi iliyoharibiwa na uchimbaji wa madini.

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Jumuiya ya Urafiki ya Urusi ipo mbioni kuingia makubaliano na Tanzania kuanzisha miradi ya kutunza mazingira kwa kutumia teknolojia ili kutokomeza tatizo hilo ikiwemo ukataji miti.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa ulimwenguni yanayokabiliwa na changamoto za kimazingira zinazotokana na ukataji miti pamoja na shughuli za kibanadamu zikiwemo kilimo na uchimbaji madini.

Mkuu wa Jumuiya ya Kijiografia ya Urusi, Yuri Korobov amesema katika taarifa ya jumuiya hiyo kuwa uharibifu huo ndio “sababu ya kuchoka kwa ardhi ya kilimo, kuharibika kwa vyanzo vya maji katika baadhi ya sehemu za Tanzania na kupotea kwa wanyamapori.”

Mjiografia huyo amesema baadhi ya changamoto hizo zinaweza kutatuliwa na teknolojia na ndio sababu ya jumuiya hiyo kushirikiana na wadau wa mazingira ikiwemo Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) ili kurahisisha shughuli za uokoaji na utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa Jumuiya ya Kijiografia ya Urusi, Yuri Korobov (kushoto) akiwa na Rais wa Umoja wa Waafrika Wanaoishi nchi za nje (Diaspora) nchini Russia, Prof Zenebe Kinfu Tafesse (kulia). Picha| Jumuiya ya Urafiki ya Urusi.

Korobov amesema ukataji wa miti pamoja na migodi iliyotelekezwa ndio sababu kuu za changamoto za kimazingira na hazina budi kutatuliwa.

“Shida zote hapo zinaweza kupunguzwa kwa gharama ya teknolojia zilizopo nchini Urusi. Ndio sababu tumepanga kufanya mafunzo ya pamoja na kubadilishana wataalamu, wanamazingira, wahandisi, wakemia na wanaojitolea,” amesema Korobov.

Jumuiya ya Urafiki ya Urusi na Tanzania zinatarajiwa kutia saini makubaliano yao ya kwanza na mwishoni mwa Juni 2021. Kama sehemu ya makubaliano, vyama vitaunda baraza la biashara, ambalo litajumuisha watumishi wa umma na wajasiriamali.

“Kwa pamoja tutafanya kazi na kutekeleza uelewa wa jinsi miradi inapaswa kutekelezwa kila mahali, hata katika miradi ya kibiashara, ambayo tutashiriki kama washauri na kutoa msaada wa habari, kuna mwelekeo wa mazingira,” amesema Korobov.