Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi wa matibabu ya figo Muhimbili
Matumizi ya teknolojia hiyo yataokoa gharama za matibabu kwa wagojwa kwa takriban mara tano ikilinganishwa na matibabu yanayotolewa nje ya nchi
Madaktari wakati wa kazi ya upasuaji wa figo uliofanyika April 19 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni moja ya mambo yaliyoweza upasuaji huo. Picha na MNH.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba ameitaka serikali kusomesha wataalamu wengi na iongeze vifaa vya kisasa na teknolojia ya kutibu magonjwa ya figo nchini ili kupunguza gharama za kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
Ushauri huo wa kamati unakuja katika kipindi ambacho ulimwengu unawekeza zaidi katika teknolojia katika utatuaji wa matatizo mbalimbali ya afya ya binadamu na wanyama.
“Kamati inashauri Serikali kuendelea kusomesha wataalamu wetu na kuhakikisha kunakuwepo na vifaa vya kisasa ili huduma bora ziweze kupatikana nchini, hivyo kupunguza gharama ambazo taifa limekuwa likiingia kupeleka wagonjwa wa figo nje ya nchi,” alisema Serukamba katikati ya wiki bungeni Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake juu ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka 2018/2019.
Pia, ushauri wa kamati hiyo unakuja siku chache baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kufanya upasuaji kwa mara ya pili na kupandikiza figo kwa wagonjwa wanne ikiwa ni matibabu ya kihistoria kufanyika nchini tangu huduma hiyo ilivyoanza kutolewa Novemba mwaka jana.
Upandikizaji wa figo ulifanywa na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Muhimbili kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya BLK ya nchini India ambapo wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji na kuwekewa figo mpya wanaendelea vizuri.
Soma: Michael Tumaini: Mwanafunzi wa shule ya kata aliyetengeneza ‘AC’, Power Bank ya simu
StraightBook: Mwokozi wa wajasiriamali asiyefahamika
Tukio hilo lilikuwa la kihistoria ikizingatiwa kuwa watu wengi ambao walikuwa wanasumbuliwa na matatizo ya figo walikuwa wanapelekwa nchini India kwa ajili ya kuwekewa figo mpya ili waendelee kuishi.
Kwa mujibu wa hospitali ya MNH matibabu au upandikizaji wa figo unagharimu Sh21 milioni ikiwa mgonjwa atapata huduma hiyo nchini ikilinganishwa na wastani milioni 80 hadi milioni 100 kwa mgonjwa anayepelekwa India.
Mafanikio hayo katika sekta ya afya nchini yatasaidia kupunguza fedha ambazo Serikali ilikuwa inatumia kuwatibu wagonjwa nje ya nchi. Pia ni mapinduzi makubwa ya teknolojia katika sekta ya afya ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za matibabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru amesema watahakikisha huduma ya kupandikiza na kutibu magonjwa ya figo inakuwa endelevu.
“Shughuli hii inatuonyesha kwamba hospitali sasa inaweza kupandikiza figo na lengo letu ni kuhakikisha huduma hii inakuwa endelevu ili kuokoa fedha za serikali kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na pia kuwafikia watanzania wengi ambao wanahitaji kupandikizwa figo.”
Prof. Museru amesema MNH inakusudia kujenga jengo kubwa ili kupanua wigo wa huduma ya matibabu na kwamba kila mwezi wagonjwa watano watakuwa wanafanyiwa upasuaji ili kupunguza idadi ya wagonjwa ambao wanasubiri kwenda kutibiwa nchini India.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za figo kutoka hospitali ya BLK, Dk. Prakash Sunil amesema ndoto yake ni kuona Tanzania inakuwa kitovu cha huduma bora za upandikazaji wa figo katika nchi za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya figo kutoka hospitali ya MNH, Dk. Onesmo Kisanga amewataka watanzania kuzingatia ulaji unaofaa wa vyakula na kufanya mazoezi ili kuepuka maradhi ya kisukari na shinikizo la damu ambayo yana mchango mkubwa kwa matatizo ya figo.
Ameongeza kuwa kama watanzania watazingatia mtindo mzuri wa maisha na kuepuka visababishi vya magonjwa ya figo, uwezekano wa wagonjwa wa figo kupungua nchini utakuwa mkubwa.
Hali halisi ya ugonjwa wa figo nchini
Ugonjwa wa figo (Chronic Kidney Disease) ni tatizo kubwa la kiafya duniani na husababisha figo kushindwa kufanya kazi na matokeo yake huleta vifo vya mapema.
Kisukari kimebainika kuwa sababu kubwa ya maradhi ya figo ambapo asilimia 44 ya maradhi mapya ya figo husababishwa na kisukari. Wataalamu wanaeleza kuwa unene uliokithiri, shinikizo la juu la damu ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia watu wengi kuugua ugonjwa huo.
Watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa ya figo
Hatari ya kupata Ugonjwa wa figo ni kubwa zaidi kwa wanawake kuliko ilivyo kwa wanaume. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ugonjwa wa figo unawakumba zaidi wanawake tofauti na wanaume ambapo hatari kwa wanawake kupata ugonjwa huo ni asilimia 14 na wanaume ni asilimia 12.
Shirika la Afya Duniani (WHO linakadiria kuwa kila mwaka maradhi hayo huchangia asilimia 10 ya vifo vyote duniani. Pia huathiri wanawake milioni 195 duniani kote na kwa sasa ni sababu ya nane inayosababisha vifo vingi vya wanawake ambapo husababisha vifo karibu 600,000 kila mwaka, kwa mujibu wa takwimu za WHO za mwaka 2018.
Hata hivyo, katika orodha ya matibabu idadi ya wanawake ni ndogo kuliko wanaume na hii inaweza kuelezwa kwa sababu kuu tatu. Kwanza ikiwa ni madhara ya ugonjwa wa figo huchelewa kuonekana ndani ya wanawake tofauti na ilivyo kwa wanaume.
Vikwazo vya kisaikolojia na kijamii kama uwezo mdogo wa kutambua ugonjwa mapema ambao hupelekea wanawake kuchelewa au kutoonekana kabisa kwenye matibabu. Pia ukosefu wa huduma bora za afya ni sababu nyingine inayozidisha tatizo katika maeneo mbalimbali duniani.