July 8, 2024

Thamani ya miamala mtandaoni yaongezeka Tanzania licha ya watumiaji kupungua

Thamani ya miamala inayofanywa kupitia huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi imeongezeka kwa Sh711.5 bilioni ndani ya mwezi mmoja licha ya idadi ya watumiaji wa huduma hiyo kupungua.

  • Mwezi Machi pekee thamani ya miamala ya fedha iliyofanywa katika simu za mkononi ilifikia Sh9.01 trilioni kutoka Sh8.30 trilioni iliyorekodiwa Februari mwaka huu.
  • Idadi ya wanaotumia huduma hizo imeshuka hadi milioni 26.4 mwezi Machi kutoka milioni 26.6 waliorekodiwa Februari. 
  • Vodacom yaendelea kumiliki soko la huduma hizo Tanzania.

Dar es Salaam. Thamani ya miamala inayofanywa kupitia huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi imeongezeka kwa Sh711.5 bilioni ndani ya mwezi mmoja licha ya idadi ya watumiaji wa huduma hiyo kupungua.

Ripoti hiyo ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  ya robo ya kwanza ya mwaka 2020, inabainisha kuwa mwezi Machi pekee thamani ya miamala ya fedha iliyofanywa katika simu za mkononi ilifikia Sh9.01 trilioni kutoka Sh8.30 trilioni iliyorekodiwa Februari mwaka huu.

Hiyo ni sawa na kusema thamani ya miamala ya fedha imeongezeka kwa Sh711.5 bilioni au asilimia 8.5 ndani ya mwezi mmoja.

Zaidi ya nusu ya miamala hiyo ya Machi ilifanyika kupitia M-Pesa inayomilikiwa na kampuni ya mawasilino ya simu ya Vodacom Tanzania. 

Thamani ya miamala hiyo iliyofanyika kupitia M-Pesa ilikuwa Sh5.08 trilioni ya fedha zote zilizunguka kupitia simu za mkononi. 

Katika mwezi huo wa Machi watumiaji wa huduma hiyo walifanya miamala milioni 256.2 ikiwa ni juu kutoka miamala milioni 239.4 ya Februari.


Soma zaidi:


Wakati thamani ya miamala ya fedha na miamala ikiongezeka, idadi ya watumiaji wa huduma hizo imepungua kwa asilimia 1.1 ndani ya mwezi mmoja.

Idadi ya watu hao wanaotumia huduma za kifedha kwa njia ya simu Tanzania imeshuka kidogo hadi watumiaji milioni 26.4 mwezi Machi kutoka milioni 26.6 waliorekodiwa Februari mwaka huu. 

Hata hivyo, katika kuhamasisha watu kutumia huduma hizo, hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliziagiza kampuni zinazotoa huduma za kifedha mtandaoni kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka Sh3 milioni hadi Sh5 milioni.

Pia, kampuni hizo zinatakiwa kuongeza kiwango cha ukomo wa akiba kwa siku kutoka Sh5 milioni hadi Sh10 milioni ili kupunguza matumizi ya fedha taslim. 

Huduma za kifedha za kwenye simu zinasaidia kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kutatua changamoto mbalimbali za kibenki ikiwemo kuweka fedha, kukopa na kulipia huduma na bidhaa mbalimbali mahali popote. 

Vodacom bado yashika usukani

Hata wakati idadi ya watumiaji ikishuka, bado M-Pesa ndiyo inamiliki sehemu kubwa ya soko la huduma za kifedha kwa njia ya simu ikifuatiwa na Tigo Pesa (Tigo) na Airtel Money ya kampuni ya Airtel.