October 6, 2024

Trump bado bado sana kufunguliwa YouTube

YouTube imesema itaondoa zuio la akaunti ya Trump iliyofungwa Januari 12 mwaka huu mpaka ijiridhishe kuwa hakuna hatari ya kufanyika kwa vurugu.

  • YouTube imesema itaondoa zuio la akaunti ya Trump mpaka ijiridhishe kuwa hakuna hatari ya kufanyika kwa vurugu.
  • YouTube ilizuia kufanya kazi kwa akaunti ya Trump Januarii 12 baada ya kutokea vurugu kwenye Bunge la Marekani. 
  • Facebook na Twitter nazo bado zimemuwekea ngumu rais huyo wa zamani wa Marekani. 

Mkurugenzi Mtendaji wa YouTube, Susan Wojcicki amesema mtandao huo utairuhusu akaunti ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuendelea kufanya kazi baada kujiridhisha kuwa hatari ya kufanyika vurugu imepungua.

Mtandao huo ambao unamilikiwa na kampuni ya Google ya Marekani ulizuia akaunti ya Trump Januari 12 mwaka huu baada ya kutokea vurugu katika Bunge la Marekani ambazo zinadaiwa kuchochewa na rais huyo wa zamani wa nchi hiyo.

Vurugu hizo zilitokea ili kupinga ushindi wa Rais wa sasa Joe Biden ambaye alimshinda Trump katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 2020 na kuapishwa Januari 20 mwaka huu. 

YouTube ilizuia akaunti ya Trump kufanya kazi kwa siku saba kwa kile ilichodai alijaribu kupakia video ambayo inakiuka sera za mtandao huo, lakini iliongeza muda wa zuio hilo mpaka sasa.

“Sitaki kuthibitisha kuwa tutaondoa zuio la chaneli…mpaka tutakapobaini kuwa hatari ya vurugu imepungua,” alinukuliwa Wojcicki na vyombo vya habari vya kimataifa wiki iliyopita. 

“Tuliposimama leo ni vigumu kwangu kusema ni lini itatokea, lakini niweke wazi kuwa mpaka sasa bado kuna viashiria vya vurugu,” amesema mwanamama huyo. 


Soma zaidi: 


Wojcicki amesema wataangalia viashairia mbalimbali vitakavyosaidia kubaini kama hatari ya vurugu imebadilika ikiwemo matamko na tahadhari kutoka serikalini, utekelezaji wa sheria na mifumo ya ufuatiliaji ya YouTube.

Pia mitandao ya Twitter na Facebook nayo ilizuia akaunti za Trump huku Twitter ikisema haina mpango wa kuiachilia akaunti ya rais huyo kuendelea kufanya kazi. 

Facebook nayo imesema italifikisha jambo hilo la kuzuiliwa kwa akaunti ya Trump katika bodi huru inayosimamia maudhui ya mtandao huo kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho