October 6, 2024

Tunayofahamu kuhusu Infinix Note 10 na Note 10 Pro

Ni zilizozingatia uwiano wa kamera, uwezo wa kumbukumbu na wa betri.

  • Ni simu ya uchumi wa kati inayouzwa kuanzia Sh450,000 hadi Sh600,000.
  • Uhifadhi wake na kamera ni nzuri na zinafaa kwa matumizi.
  • Betri lake linaweza kudummu kwa siku mbili kwa mtumiaji wa wastani.

Dar es Salaam. Kampuni zinazotengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki ikiwemo kompyuta na simu janja zimekuwa mashuhuri katika kusasisha teknolojia kwa kuingiza sokoni matoleo mapya ya simu ambapo hadi sasa tumeshuhudia Tekno, Samsung, Oneplus na Sony wakiingiza simu mpya sokoni kwa mwaka 2021. 

Kwa hali ya ukuaji wa dijitali, teknolojia zinahitaji kusasishwa ili kuongeza ufanisi na kumridhisha mtumiaji lakini pia kuimarisha usalama. 

Hata hivyo, sasa ni zamu ya kampuni ya Infinix Mobile inayotengeneza simu za Infinix kuingiza mzigo mpyaa sokoni baada ya kuachia matoleo yake ya Infinix Note 10 na Note 10 pro ambazo kwa Tanzania, zimezinduliwa Juni 4, 2021.

Ni nini kipya katika simu hizo? Haya ndiyo tunayoyafahamu:-

Uwezo wake wa betri

Kwa mwaka 2021, simu nyingi zilizotoka zina uwezo wa betri la mAh 4,500 hadi mAh 5,000, betri ambalo lina uwezo wa kumvusha mtu siku nzima. Infinix nao wamecheza mule mule kwa simu zake zote yaani Note 10 na Note 10 pro kuwa na betri za mAh 5,000.

Kwa kawaida, betri hilo lina uwezo wa kudumu kwa siku mbili kwa mtumiaji wa wastani asiyependa kutazama video au kucheza michezo ya kwenye simu (games) mara kwa mara. 

Uwezo huo ni zaidi ya Samsung Galaxy A52 ambayo betri lake ni mAh 4,500 na ni sawa na Tecno Camon 17 ambayo pia ina betri la mAh5,000.

Infinix Note 10 na Note 10 pro zina betri za mAh 5,000. Picha| TechEngage.

Ukubwa wa simu na sifa za ziada

Simu hizi zimetengenezwa kwa ajili ya kukaa mfukoni na kutumika kwa urahisi katika viganja vya mikono hivyo zinakuja katika ukubwa wa inchi 6.80 kwa 3.08 ( Note 10 Pro) na inchi 6.82 kwa 3.10 (Note 10).

Pia, simu zote zinatumia laini mbili na zina sehemu kwa ajili ya kuweka kadi ya kumbukumbu yenye uwezo wa hadi.

Hata hivyo, haijawekwa bayana kima cha juu cha uwezo wa kadi ya kumbukumbu ambayo inaendana na simu hizi. 

Kingine kilichoboreshwa kuhusu simu hizi ni usalama wa njia ya alama za vidole ambao umekuja kwa namna tofauti.

Simu nyingi huweka sehemu ya kuweka alama za vidole nyuma ya simu huku zingine zikiweka sehemu hiyo kwenye skrini ikiwemo i Phone 12 na Samsung Galaxy S 21. Kwa Infinix sehemu hiyo kwa sasa ipo kwenye kibonyezeo cha kuwashia simu upande wa kulia wa simu sambamba na sehemu ya kuongeza na kupunguzia sauti.

Simu hizi zinachajiwa na chaja aina ya Type C na zina sehemu kwa ajili ya kuchomekea “earphones” za Jack 3.5mm ambazo ni rahisi kupatikana kwenye maduka ya vifaa vya elektroniki Tanzania. 

Uhifadhi na kamera

Hakuna sababu ya kuwa na simu yenye kamera nzuri kisha ikakosa uhifadhi. Infinix wameliona hilo na ndiyo sababu ya kuwa na kamera nne kwa Infinix Note 10 pro na kamera tatu kwa Note 10.

Uwezo wa kamera hizo ni Mega Pixel (MP) 64 kwa kamera kuu ya Note 10 pro ambayo inaambatana na kamera zingine za MP 8, 2 na 2 ambazo zinatumika kuiga picha za mapana na za karibu. 

Kwa Note 10, kamera yake ina ukubwa wa MP48 kwa kamera kuu na Mp 2 na 2 kwa kamera za mapana na picha za karibu.

Simu zote zina kamera ya mbele yenye uwezo wa MP 16.

Note 10 pro inaambatana na uhifadhi wa Gigabytes (GB) GB 64 hadi GB 256 kwa uhifadhi wa kawaida na GB6 hadi GB 8 kwa uhifadhi wa ndani (RAM) huku Note 10 ikiwa na uhifadhi wa kuanzia GB64 hadi Gb 128 za uhifadhi wa kawaida na uhifadhi wa RAM ukiwa ni kuanzia GB 4 hadi GB 6.


Soma zaidi:


Kutoboa mfuko

Kuipata simu hiyo, siyo jambo dogo japo inapatikana kwa bei tofauti kulingana na uhifadhi. Kwa Note 10, itahitaji Sh450,000 kumiliki simu hiyo huku Note 10 pro ikihitaji Sh600,000, bei ambazo kutokana na sifa zake na malighafi yaliyotumika, ni rafiki hasa kwa mtumiaji wa uchumi wa kati.

Hata hivyo, iwapo unahitaji simu janja ya kawaida, unaweza kupata kwa bei nafuu zaidi kuliko bei hizi. 

Kwa mujibu wa Infinix, rangi za simu ya Note 10 pro ni nyeusi, dhambarau na “Nordic Secret”. Note 10 yenyewe inapatikana katika rangi nyeusi, dhambarau na “Emerald Green”.

Huenda usipende haya

Kwa simu za mwaka 2021, wadau wengi wanatengemea maboresho katika muundo na muonekano. Kwa infinix Note 10 na Note 10 pro, simu hizo zina kioo mbele yaani kwenye skrini huku plastiki ikichukua nafasi zaidi ikiwemo sehemu ya nyuma ya simu.

Plastiki katika simu siyo jambo baya lakini kwa simu nyingi zinazotumia malighafi hayo huwa ni rahisi kupata michubuko na kupauka endapo mtumiaji wake hatotumia jarada. 

Wadau wengine wa teknolojia akiwemo Eric Okafor kupitia chaneli yake ya Youtube amesema simu hizi zinachemka haraka hasa pale zinapokuwa katika matumizi mazito ikiwemo kucheza michezo ya kielektroniki au kuvinjari mtandaoni kwa muda mrefu.

Zaidi, kamera za simu hii ni nzuri pale kunapokuwa na mwanga lakini gizani, huenda mtumiaji wake asipate matokeo yanayoridhisha.