July 8, 2024

Uber yatoa masharti mapya kwa madereva wake

Imeanza kutekeleza agizo lake linalowataka madereva wake kujipiga picha inayoonyesha wamevaa barakoa kabla ya kuwabeba abiria ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona wakati wanatumia usafiri huo.

  • Dereva hataruhusiwa kubeba abiria mpaka awe amevaa barakoa.
  • Pia anatakiwa kuwa na kitakasa mikono na kunawa mikono mara kwa mara. 
  • Abiria nao wanatakiwa kuvaa barakoa wakati wote wa safari.

Dar es Salaam. Kampuni ya usafiri wa mtandaoni ya Uber leo imeanza kutekeleza masharti mapya yanayowataka madereva wake kujipiga picha inayoonyesha wamevaa barakoa kabla ya kuwabeba abiria ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona  wakati wanatumia usafiri huo. 

Picha hiyo inatakiwa kupigwa kwa kutumia programu ya simu (App) ya Uber ambayo itathibitisha kuwa dereva anaweza kumbeba abiria. 

Uber katika taarifa yake iliyotolewa Jumatano Mei 13, 2020 imeeleza kuwa hiyo ni sehemu ya mambo muhimu ambayo dereva anatakiwa kutekeleza kabla hajatumia app hiyo kila siku.

“Kwa sasa majiji yameanza kufunguliwa tena na watu wameanza shughuli zao, Uber inaendelea kuchukua tahadhari  na kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu kumsaidia kila mmoja kuwa salama kiafya akiwa anasafiri,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Uber. 

Madereva wa Uber wanatakiwa kuthibitisha kuwa hawana dalili za Corona, wana vitakasa mikono (sanitizers), wanaosha mikono mara kwa mara. 

Pia, abiria wanaotumia usafiri wa Uber (taxi, bodaboda na bajaji) wanatakiwa kuthibitisha kuwa wamevaa barakoa au kifunika uso kabla ya kuita gari.


Zinazohusiana:


Wao hawatakiwi kujipiga picha (selfie) lakini Uber wamesema wanatarajia kuona madereva na abiria wanawajibishana katika kuchukua tahadhari ya kujikinga na COVID-19. 

Ikiwa dereva na abiria hawajavaa barakoa au kifunika uso, safari yao haitahesabika kwenye app ya Uber kwa sababu wataondolewa mtandaoni kwa wakati huo. 

Hata hivyo, hakutakuwa na faini ya kukiuka masharti yaliyowekwa na Uber.

Kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Marekani imesema masharti hayo yatadumu hadi mwezi Juni kabla hayafanyiwa tathmini kulingana na mwenendo wa ugonjwa wa COVID-19. 

Aidha, Uber imesema imetenga dola za Marekani 50 milioni (Sh115.7 bilioni) kwa ajili ya kununua vifaa tiba zikiwemo barakoa, vitakasa mikono, sabuni na vifaa vya kuoshea magari kwa ajili ya madereva wake.