Ufahamu mlima uliotengenezwa kwa taka za kielektroniki
Aliyeubuni amesema mlima huo utawakumbusha viongozi na dunia kwa ujumla uharibifu wamazingira unaotokana na taka za kielektroniki.
- Mlima huo watengenezwa ili kuwakumbusha watu uharibifu unaosababishwa na teknolojia.
- Mbali na taka, mlima huo una sura za viongozi wa mataifa saba yaliyoendelea zaidi katika viwanda.
- Hadi sasa taka zaidi ya tani 50 zimezalishwa duniani.
Joe Rush, mbunifu kutoka Uingereza, ametengeneza mlima kwa kutumia taka za kielektroniki akiwa na lengo la kukumbusha watu na nchi zilizoendelea kwa sekta ya viwanda kurejelea taka ambazo zinatokana na bidhaa wanazozizalisha ikiwemo simu, kompyuta na deki.
Mlima huo wa taka uliopo nchini Uingereza umetengenezwa kwa kutumia malighafi ya plastiki, nyaya na mabaki ya bidhaa za kielektroniki ambazo zimeharibika na hazina kazi tena.
Mlima huo uitwao “Recyclemore” ambao kwa tafsiri ya Kiswahili ni “rejelea zaidi” umetengenezwa ukiwa na mfanano wa sura saba za viongozi wanaotokea katika nchi zilizoendelea kiviwanda duniani ikiwemo Ufaransa, Japan, Italia, Canada, Marekani na Ujerumani.
Viongozi hao ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Marekani, Joe Biden.
Mlima huo umetengenezwa kwa mfanano wa sura za viongoozi wa mataifa saba ambayo yameendelea kiuchumi (G7) akiwemo Rais wa Marekani Joe biden. Picha| Mtandao.
Rush amesema mlima huo utawakumbusha viongozi hao na dunia kwa ujumla uharibifu ambao umefanywa na unaendelea kufanywa na taka za kielektroniki.
Mlima “Recyclemore” umetengenezwa kuhamasisha nchi zilizoendelea kiviwanda kutengenza bidhaa zinazokaa kwa muda mrefu, zinazoweza kurejelewa na kupunguza uzalishaji wa matoleo mapya.
Mlima huo umechukua nguvu ya watu 12 kuujenga ndani ya wiki sita.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa (UN) imesema zaidi ya tani milioni 53 za taka za kielektroniki zimetelekezwa duniani hadi kufikia mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya tani milioni tisa zilizozalishwa mwaka 2014.
“Recyclemore” utawakumbusha viongozi na dunia kwa ujumla uharibifu wa kimazingira unaosababishwa na bidhaa za kielektroniki. Picha| Mtandao.