Ufanye nini kupata fursa mtandaoni?
Eleza kwa ufasaha wasifu wako, fahamu kwa undani fursa unayoomba na mahitaji yake ili kujiweka katika nafasi ya kuipata.
- Eleza kwa ufasaha wasifu wako, fahamu kwa undani fursa unayoomba na mahitaji yake ili kujiweka katika nafasi ya kuipata.
- Jitofautishe na wengine kwa kuonyesha uzoefu wako kwa jambo unalofanya na kuhakikisha unatumia vizuri lugha kuwasilisha mawazo yako.
Dar es Salaam. Licha ya vijana kuchangamkia fursa za mtandaoni lakini sio wote wanaofanikiwa kuzipata kutokana na kutokujua mambo ya kuzingatia wakati wanapoomba fursa hizo.
Fursa za mtandaoni zinaweza kuwa za masomo, mafunzo au hata kupata mtandao wa watu unaoweza kufanya nao biashara au kazi. Lakini kila fursa ina masharti na vigezo vyake ambavyo unatakiwa kutimiza kikamilifu ili kupata kile unachokitaka.
Baadhi ya wazoefu na waliofanikiwa katika kupata fursa mtandaoni wamekuwa wakitoa mbinu ambazo zitasaidia vijana wenye shauku ya kukua kibiashara na kitaaluma na hatimaye kuanza kutengeneza faida.
Katika wasilisho maalum kwa wajasiriamali Februari 21, 2019, Mkurugenzi wa kampuni ya StartUp Grind Dar es Salaam, Cynthia Bavo, ambaye ni mmoja wa vijana walionufaika na fursa za mtandaoni kutoka kwa Taasisi ya Tony Elumelu Foundation ya nchini Nigeria alieleza mambo muhimu unayotakiwa kufanya wakati unatafuta fursa mtandaoni.
Jielezee vizuri wewe ni nani
Katika kuomba fursa za mtandaoni, Bavo anawashauri vijana umuhimu wa kujielezea wewe ni nani na sio kuishia kwenye jina na umri. Bali eleza wasifu wako kwa undani, wewe ni nani kama binadamu na ni vitu gani vinakufanya uwe jinsi ulivyo.
“Unapojieleza hakikisha unajiuza vizuri kwasababu wenzako wanajieleza kwa upana zaidi, amesema Bavo.
Kuwa makini wakati unajaza fomu yako ya maombi ya fursa zilizopo mtandaoni. Picha| Idealistcareers
Eleza uzoefu kwa kitu unachoomba
Bavo anashauri vijana wanaoomba fursa za mtandaoni kuhakikisha wanaeleza kwa undani juu ya uzoefu walionao kulingana na fursa wanayoomba. Kama ni biashara elezea uzoefu wako labda ina muda gani, umefanya nini kuikuza na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Hata kama upo kwenye hatua za mwanzo za biashara yako basi hakikisha umefanya hata utafiti kuhusu hilo jambo ili uonekane unahitaji hiyo fursa na unajua nini unakifanya.
“Hakikisha unafanya utafiti wa kutosha na tumia sana ushahidi kama takwimu au mwingine kuonyesha ulifanya kazi yako kabla ya kuomba,” anasema Bavo.
Jifunze kuomba msaada wa mawazo unaposaka fursa za mtandaoni ili kujiweka katika nafasi ya kufanikiwa. Picha| digitalblogger.com
Jitofautishe na wengine
Sina maana ujitofautishe na wengine kwa kuwadharau ama kutoshirikiana nao katika mambo mbalimbali. Maana ya kujitofautisha ni namna ya kufanya mambo kwa utofauti na uweledi wa hali ya juu.
Anawashauri vijana kabla ya kuomba inapaswa wafanye kazi ya ziada kujitafakari na kufanya kazi ya kutosha ya kujitofautisha na mwingine. Hasa kama ni fursa za kibiashara, onyesha tofauti yako na mtu mwingine ili kukufungulia mlango wa kukubalika zaidi.
“Elezea mafaniko yako binafsi na kwa jinsi gani ukipata hiyo fursa utayatumia ili yaweze kuleta manufaa kwako na kwa jamii kwa ujumla,” amesema Bavo.
Zinazohusiana: Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Wahitimu vyuo vikuu wakumbushwa kuchangamkia fedha za halmashauri
Tumia lugha rasmi
Lugha hapa inaweza kuwa ya kuongea au maandishi, pangilia vizuri mawazo yako kabla ya kuwasilisha ili kuleta maana kwa mtu anayesoma.
Jieleze vizuri na hakikisha unamudu vizuri lugha unayoitumia. Kama ni Kiingereza basi jitahidi kukielewa vizuri ili uaminiwe na watu unaotaka kufanya nao kazi.
“Ukiandika lugha vibaya bila kuzingatia uandishi ni njia ya kwanza ya kufeli,” anasema Bavo na kuongeza kuwa kabla hujatuma maombi ya kupata fursa, mpe rafiki yako ahariri na kuondoa
makosa.