October 6, 2024

Ukosefu wa taarifa unavyowanyima fursa wabunifu wa teknolojia

Maboresho ya mfumo wa utoaji taarifa za fursa kiteknolojia ni muhimu kuwafikia wabunifu wengi

Related image

Ubunifu nyenzo muhimu ya kukua vipaji vya vijana hasawanapokutana na kubadilishana mawazo. Picha|http://ipeyeblog.com/buni-hub-innovation-tanzania/


  • Bado vituo vya kukuza ubunifu haviwafikii vijana wengi waliopo vijijini.
  • Maboresho ya mfumo wa utoaji taarifa  za fursa kiteknolojia ni muhimu kuwafikia wabunifu wengi.
  • Ni wakati wa kuwaangalia upya wabunifu wa kiteknoloja ili waweze kuikomboa nchi katika sekta ya Tehama.

 Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kupiga hatua katika kuimarisha teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), bado idadi kubwa ya vijana hawajaweza kutumia kikamilifu vituo vya ubunifu na uvumbuzi kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka.

Hali hiyo inajitokeza kutokana na upokeaji mdogo wa fursa za ubunifu wa zinazoelekezwa kwa vijana, kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa upatikanaji wa taarifa na vituo hivyo kujengwa katika maeneo machache ambayo hayafikiwi na vijana wote.   

Baadhi ya vituo hivyo ni Buni Hub, Jenga Hub, Ndoto Hub, DTBi, Sahara Ventures vilivyopo katika Jiji la Dar es Salaam na mara nyingi huwakutanisha wabunifu kujadili na kutafuta suluhisho la teknolojia kwa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.   

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Geofrey Karokola anasema hakuna mgawanyo mzuri wa vituo vya ubunifu na vingi viko kwenye majiji makubwa au miji inayokua haraka, jambo linalowanyima fursa vijana waliopo vijijini kutumia vipaji na uwezo wao kuboresha maisha.

“Fursa za ubunifu zinawafikia watu wachache sana, hasa wale waliopo mijini, au wenye connection (kujuana na watu), kwa mfano kwa upande wa teknolojia angalau tuna kituo kilichopo COSTECH (Tume ya Teknolojia na Sayansi) cha DTBi (Atamizi ya Teknohama ya Dar es Salaam), sio wote wenye wanafikiwa na kituo hicho,” anasema Dk Karokola.

Dk Karokola anasema ni muhimu vituo vya kuwainua wabunifu viwepo kila wilaya nchini ili kufungua milango ya fursa kwa vijana wabunifu kushiriki na kujifunza na kutumia rasilimali zinazowazunguka kuleta mabadiliko.

Wataalam wengine wa Tehama wanabainisha kuwa licha ya uhaba wa vituo vya kunoa ubunifu bado vijana hawana mwamko wa kuchangamkia fursa chache zinozojitokeza wakati wakisubiri vituo hivyo kupelekwa katika maeneo yao.

 “Changamoto ni vijana wanahisi fursa zinawafuata badala ya wao kuzifuata,” anasema Paul Mandele, Msimamizi wa kituo cha Buni kinachendeshwa na COSTECH.

Mandele ameeleza kuwa licha ya kituo hicho kuwakutanisha wabunifu na wajasiriamali na wabunifu bado mwitikio wa walengwa ni mdogo ukilinganisha na fursa zilizopo.

“Sisi tunavyoita vijana mara nyingi lengo ni kuwakutanisha  na kuona jinsi gani tunaweza kuwasaidia waweze kuendeleza au kuboresha mawazo yao,” anasema Mandele.


Zinazohusiana: 


Vituo hivyo ni majukwaa muhimu yanayowakutanisha watu kada mbalimbali kuibua hoja na mawazo mbadala na kubadilisha uzoefu wa kushughulikia matatizo yaliyopo katika jamii.  

Pia ni fursa kwa wabunifu kusaidiana ili kuendeleza sekta ya Tehama nchini ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo rasilimali fedha na utashi wa kisiasa.

Dk Karokola anasema ikiwa vituo hivyo vitajengewa uwezo na kusambaa katika maeneo yote nchini vitakuwa chachu ya kuvutia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya Tehama nchini.

“Faida nyingine ni kuweza kupata wadhamini wa kufadhili miradi ya mbalimbali ya wabunifu,” anasema Dr Karokola.

Wakati wasomi wakihimiza vijana kuchangamkia fursa cha Tehama, ripoti mpya ya utafiti wa Ushindani Duniani imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kwa kasi ndogo ya matumizi ya tehama jambo linalofanya ishindwe kutumia ipasavyo fursa zitokanazo na sekta hiyo katika kuleta maendeleo.

Ripoti hiyo kwa Kiingereza ‘Global Competitiveness Index 2018’ iliyotolewa na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) juma lililopita imeiweka Tanzania katika nafasi ya 135 katika ya nchi 140 zilizofanyiwa utafiti huo. Mwaka 2017, Tanzania ilishika nafasi 122 kati ya nchi 137 zilizofanyiwa utafiti.