November 24, 2024

Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya Taifa

Unatoa fursa lukuki zinazotegemea umeme kwa watu waliopo mbali na gridi ya Taifa.

  •  Ni chanzo cha matumaini kwa watumiaji wa umeme majumbani.
  •  Inatoa ajira na kuongeza kipato kwa wakazi waliokuwa hawana tegemeo la umeme 

Kilomita 10 kaskazini mwa kisiwa maarufu cha Ukerewe katika Ziwa Victoria, wanaishi wakazi wa kisiwa kingine cha Ukara ambao hawajafikiwa na umeme.  Kwa jinsi eneo la Ukara lilipo ilikuwa ni ngumu kuufikisha umeme wa gridi ya Taifa katika kisiwa hicho cha pili kwa ukubwa katika ziwa hilo.

Kwa wakazi wa kisiwa hicho, ili wapate umeme hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kutumia umemejua au majenereta ya mafuta ya petroli yanayomilikiwa na watu wachache wenye kipato cha kati au wavuvi na wakulima wenye uwezo wa kupata fedha nyingi kwa msimu fulani wa mwaka.

Hata hivyo, nishati jadidifu imekuwa ni mkombozi kwa wakazi hao baada ya kusambaa kwa kasi umemejua ambao umekuwa mbadala wa kusubiri majaliwa ya umeme wa gridi ya Taifa unaosambazwa na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).

Tofauti na wale wanaotumia paneli moja ya umemejua kwa kila nyumba, katika kata ya Bwisya, Ukara kuna mwekezaji amefunga umeme wa gridi ndogo ambapo wanakijiji wanajiunga na kunufaika na umeme huo.

“Zamani ilikuwa ikifika saa 2:00 usiku tu biashara za maduka zilikuwa zimeshafungwa ila kwa sasa watu hadi saa 6:00 usiku mtu anaweza  ndio akawa anafunga biashara,” anasema Boniventure Erick, Mkazi wa Ukara.

Awali biashara zilizokuwa zinatumia umeme hazikuwa nyingi sana kutokana na gharama kubwa za mafuta ya jenereta lakini baada ya kuwepo kwa umeme huo watu wengi wameanza kukimbilia kufungua biashara.

“Biashara kama kuchajisha simu, kuuza ‘Ice cream’au mabarafu, kufanya kazi kwa muda mrefu kwa kutumia umeme na gharama nafuu ni faida tulizozipata kutokana na umeme wa jua,” anaelezea Boniventure huku akionyesha tabasamu la kuwa na matumaini na umeme wa jua uliokuwa nuru kisiwani humo.

Umeme kwa njia nishati jadidifu au mbadala umekuwa kimbilio la kupata umeme kwa wale ambao ambao hawajabahatika kufikiwa na umeme wa gridi ya Taifa.

         Moja ya matumizi ya umeme wa jua katika sehemu kusipokuwa na gridi ya Taifa| Picha ya Mtandao 

Kwa mujibu wa ripoti ya hiyo The Global Innovation Index (GII) ya mwaka 2018 inakadiriwa kuwa watu bilioni 1.2 duniani  hawana umeme huku watu bilioni 2.8 wanaishi bila kuwa na mazingira safi na salama ya kupikia.Maeneo mengi yanayopitiwa na umeme wa maji ni yale kwa kiasi kikubwa yalikaliwa na wakoloni kutokana na kuwarahisishia mawasiliano kipindi cha ukoloni.

Hii imesababisha kuwepo na maeneo yenye umeme na yasiyo na umeme. Sehemu kubwa ya maeneo yasiyo na umeme yapo mbali na mji au vijijini.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 kampuni za umeme wa nishati ya jua zilianza kuingia katika maeneo mbalimbali nchini ambayo hayajafikiwa kabisa na umeme kama mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Manyara, Kigoma.

Miaka 30 baadaye, wawekezaji wengi zaidi wameendelea kujikita katika utoaji wa huduma ya umeme wa jua kwa bei rahisi ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa umeme nchini hasa walio nje ya gridi.

                                                                   Vifaa vya kuunganisha umeme wa jua

Kampuni kama Mobisol,Trend Solar, Agenergies, Sunking na nyingine nyingi zimejikita katika uuzaji wa vifaa vinavyotumia umemejua na usambazaji ili waweze kuwafikia watu maeneo mbalimbali yanayohitaji umeme huo.

“Upatikanaji wa umeme wa jua kama nishati jididifu hauna gharama kubwa bali inategemea na mahitaji yako. Mara nyingi unaanzia Sh10,000 na kuendelea kulingana na matumizi na kuna wanaotumia kwa ajili ya mwanga, kuchaji simu na wengine kwa biashara,” anaeleza Sisty Basil, Mratibu wa  Shirika la Energy Change Lab Tanzania.

Umeme wa kutumia nishati ya jua umekuwa mwanga hata kwa watu ambao walikuwa wamepoteza kabisa tumaini la kutumia baadhi ya vitu, na imefungua mipaka ya biashara hasa katika kipindi hiki ambapo karibu kila mahali kuna matumizi ya vifaa vya kielektoniki.

Ripoti ya hiyo ya GII imeitaja Tanzania kama mojawapo ya nchi ambayo inafanya vizuri katika uzalishaji wa umeme katika maeneo yaliyo nje ya mfumo wa gridi ya Taifa.

“Hapa kuna baadhi ya kampuni zenyewe wanazalisha umeme wa jua na wana gridi ndogo ambazo zinasambaza umeme katika maeneo kama vile wanavyosambaza umeme wa kawaida na watu wanalipa ankara zao kwa mwezi,” anasema Sitsty.