Una kipi cha kujivunia miaka 10 kuzaliwa WhatsApp?
Mtandao huo ulianzishwa rasmi mwaka 2009 na unatarajia kutanua huduma zake kuwaunganisha watu wengi zaidi katika sekta ya mawasiliano na maendeleo
- Mtandao huo ulianzishwa rasmi mwaka 2009 na unatarajia kutanua huduma zake kuwaunganisha watu wengi zaidi katika sekta ya mawasiliano na maendeleo.
- Katika miaka 10 imefanya mabadiliko mbalimbali na kufanikiwa kuwaunganisha watumiaji zaidi ya bilioni 1.5 duniani.
Wakati mtandao wa kijamii wa WhatsApp ukiadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, umesema utaendelea kufanya maboresho mbalimbali na kujitanua ili kuwafikia watu wengi na kurahisisha huduma za mawasiliano duniani.
Mtandao huo uliasisiwa mwaka 2009 na waliowahi kuwa wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Yahoo Inc, Jan Koum na Brian Acton na ilipofika February 2014 programu hiyo tumishi iliuzwa kwa Dola za Marekani 19.3 bilioni kwa mmliki wa Facebook, Mark Zuckerberg.
WhatsApp yenye watumiaji zaidi ya 1.5 bilioni imejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuwawezesha watu kuwasiliana kwa ujumbe mfupi wa maneno, kupiga simu za sauti na video wakiwa wameunganishwa na mtandao wa intaneti duniani.
Katika taarifa iliyolewa Februari 25, 2019, mtandao huo umeeleza kuwa utaendelea kuboresha huduma zake ili kuwauunganisha watu wengi zaidi duniani kwa shughuli za mawasiliano na maendeleo.
“Tunahamasika kuendelea kutengeneza programu ambazo zitaifanya WhatsApp kufanya kazi kwa urahisi na kupatikana kwa kila mtu,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, WhatsApp imesema inajivunia kuangiza sokoni programu tumishi ya biashara (WhatsApp Business App) iliyoanzishwa mwaka 2018 ambapo wafanyabiashara wanapata fursa ya kuonana na wateja na kujua kwa undani mwenendo wa biashara siku kwa siku.
Soma zaidi:
- Uunganishwaji wa WhatsApp, Facebok bado sana
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- Wadau mtandaoni watoa neno WhatsApp kudhibiti habari za uongo
Oktoba, 2018 mtandao huo uliamua kujisogeza zaidi kwa watumiaji na kuanzisha njia mpya ya mawasiliano ya stika. Stika hizo zenye muonekano tofauti zinasaidia kuonyesha hali ya mtu, jambo ambalo huwezi kulifanya kwa kuandika kwa maneno. Pia watumiaji wanaweza kutengeneza stika zao wenyewe kuelezea hali na matukio wanayofanya kila siku.
Ujio wa WhatsApp unatajwa kuwa ni mapinduzi ya teknolojia ya utumaji ujumbe mfupi wa maneno kwasababu imechukua sehemu kubwa ya ujumbe (SMS) unaotumwa kwa simu za mkononi ambao hauihitaji kuungwanishwa na mtandao wa intaneti.
Wakati mtandao huo unaanzishwa Januari 24, 2009, mtumiaji alikuwa ana uwezo wa kutuma ujumbe tu, lakini ilipofika Desemba mwaka huohuo ikaongezwa programu nyingine ya kubadilishana picha na video (Photos and video sharing).
Mwaka mmoja baadaye yaani Juni 2010, ikaboreshwa zaidi na kipengele cha mahali alipo mtumiaji kikaongezwa (Location sharing). 2011 soga za kwenye makundi zikaruhusiwa (Group Chat) ambapo mpaka sasa ujumbe wa watu 1 bilioni hutumwa kila siku.
Kwa sasa WhatsApp inachuana vikali na Twitter na Instagram; mitandao ya kijamii iliyojiimarisha zaidi katika sekta ya mawasiliano duniani. Picha|Mtandao.
2013 ukawa ni mwaka wa wateja kutumia ujumbe wa sauti (Voice messages) na mwaka uliofuata wa 2014 mtandao huo ukafikisha watumiaji milioni 500 na rasmi ukawa chini ya Facebook ya Mark Zuckerberg.
Watumiaji wa kompyuta nao walikumbukwa mwaka 2015 na kuiwezesha WhatsApp kufunguka katika mfumo wa tovuti ikiwa imeungwanishwa na simu (WhatsApp Web). Mwaka uliofuata ukawa wa maboresho zaidi, watumiaji wakawezeshwa kupiga simu za video (video calling) na kuanzisha kwa App ya WhatsApp kwenye kompyuta.
Kuelekea 2017, kipengele kingine cha ‘Status’ kikaongezwa kuwawezesha watumiaji kuonyesha hali na maoni binafsi kulingana na nyakati wanazopitia katika maisha ya kila siku. Ilipofika 2018, simu za makundi (Group calling) na stika kwa ajili ya mawasilino zikazinduliwa.
Na sasa ni 2019, WhatsApp inaadhimisha miaka 10 ya kutoa huduma za mawasiliano. Una lipi la kujivunia katika matumizi yako ya WhatsApp katika kipindi ambacho mtandao huo unashtumiwa kwa kuwa kinara wa usambazaji wa habari za uongo?