October 6, 2024

Unataka kupunguza gharama za maisha? Tumia feni za juu

Zinaongeza mvuto kama pambo linalopendezesha nyumba na hazihitaji matengenezo ya mara kwa mara.

  • Zinaongeza mvuto kama pambo linalopendezesha nyumba na hazihitaji matengenezo ya mara kwa mara.
  • Zinatumia umeme mdogo kutoa utendaji ulio sawa na ule wa kawaida, mzuri na urahisi. 
  • Zinaweza kusababisha kelele na kupotea kwa umeme ikiwa mota (motors) zitafanya kazi kupita kiasi.  

Dar es Salaam. Wakati ukiwaza kupata hewa safi na hali ya utulivu inayoendana na mwili wako katika nyumba yako ni muhimu pia kufikiri jinsi ya kupunguza gharama za maisha wakati ukitumia vifaa vya umeme.

Leo katika teknolojia ya vifaa vya kielektroniki tunaangalia matumizi ya feni zinazofungwa kwenye dari la nyumba (Ceiling fan); yanavyoweza kupunguza gharama za maisha kwa watu wanaotumia nyumbani na ofisini.  

Kwa watu wanaoishi katika maeneo yenye joto kubwa kama Dar es Salaam, matumizi ya feni au viyoyozi hayaepukiki.  Lakini uchaguzi wa kifaa kinachotumia umeme mdogo ni muhimu katika kuhakikisha kipato chako kinakuwa endelevu na kutumika katika mambo ya msingi ya maendeleo. 

Ufanisi wa nishati ya umeme katika nyumba yako ni kutumia nishati kidogo kutoa utendaji ulio sawa na ule wa kawaida, mzuri na urahisi. 

Chama cha Taifa cha Ujenzi wa Nyumba  (National Association of Home Builders) cha nchini Marekani kinaeleza kuwa matumizi ya feni yanaweza kukupunguzia gharama ya pesa ya kulipia bili ya umeme kwa asilimia 30 hadi 40.   

Licha kupunguza gharama, feni ya juu inaongeza mvuto kama pambo linalopendezesha nyumba na vilevile feni ya juu inakupa nafasi ya kuchagua matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati unaotaka.  

Mwongozo wa mpangaji wa kutunza nishati na maji wa nchini Australia unaeleza kuwa feni ya kwenye dari inagharamu karibu asilimia moja ya umeme kwa saa inapokuwa inafanya kazi na inazalisha gesi ndogo chafu kuliko ile ya viyoyozi.


Zinazohusiana: 


Feni ya juu pia inaweza kutumika kipindi cha baridi kutengeneza hali ya unyevunyevu na kukupunguzia baridi kutokana na mota ambayo inazunguka muda muda wote. Hii inakuepusha kutumia vifa vya kuongeza joto ambavyo vinatumia umeme mwingi.

“Feni zinasaidia kusambaa hewa na zinaweza kutumika kuboresha ufanisi wa mifumo ya baridi ya hewa ikiwa ni pamoja na kusambaa hewa ya moto na kuboresha ufanisi katika majira ya baridi,” unaeleza Mwongozo wa mpangaji wa kutunza nishati na maji.

   

Feni ya juu ya kisasa yenye taa ambazo unaweza zitumia chumbani au sebuleni kwako. Picha| www.sears.com

Watumiaji wa feni za juu hapa nchini wanakiri kuwa feni hizo zinarahisha gharama na hazina usumbufu wa kuziamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Uhitaji kuhamishahamisha ili kupata mwelekeo mzuri wa upepo,” anasema Gulaton Masiga, mkazi wa Jijini Dar es Salaam

Masiga anasema feni hizo hazihitaji matengenezo ya mara kwa mara kama ilivyo kwa feni za kuhamisha na viyoyozi.

Licha ya faida hizo za feni za juu, taasisi ya Hammond Power Solution ya nchini Marekani inaeleza kuwa feni hizo ni chanzo cha kelele na zinaweza kusababisha kupotea kwa umeme ikiwa mota (motors) zitafanya kazi kupita kiasi.  

Zinaweza kuwa ni chanzo cha kueneza magonjwa ya mfumo wa upumuaji ikiwa nyumba unayoishi inapitisha vumbi na hewa chafu.

“Ina vumbi sana na kelele hiyo ndo shida ya hizi feni za juu,” asema Ipyana Francis, mkazi wa Dar es Salaam.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa matumizi ya feni hutegemea aina ya nyumba na mazingira ilipo lakini feni nzuri ni ile inayokupunguzia gharama za maisha.